Thursday, June 28, 2018

NSSF YAKABIDHI MASHINE 12 ZA KUPIMA SHINIKIZO LA DAMU KATIKA HOSPITALI YA TEMEKE

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam limetoa mashine za kupima shinikizo la damu 12 zenye thamani ya Sh.5,000,000 kwa Hospitali ya Wilaya ya Temeke kwa lengo la kuboresha utoaji huduma hospitali hapo.

NSSF imesema vifaa tiba hivyo vitatumika kwa Watanzania wote watakaofika kupata tiba Hospitali ya Wilaya ya Temeke.Pia vitatumika kutoa huduma kwa wanachama wao wapatao 4000 ambao wanatibiwa hapo.

Akizungumza leo katika hosptali hiyo baada ya kukabidhi mashine hizo Kaimu Meneja Kiongozi wa NSSF Mkoa wa Temeke Barnabas Ndunguru amesema wametoa msaada huo kutokana na maombi ya hospitali hiyo.

Pia amesema msaada huo ni moja ya jukumu la NSSF katika kurudisha fadhila kwa jamii ikiwa ni jitihada za kuisaidia Serikali katika juhudi za kuboresha sekta ya afya nchini.

Amefafanua NSSF Mkoa wa Temeke idadi ya wanachama wake wanaopatiwa huduma katika hospitali hiyo ni 4000 na kwa mwezi wanatoa fedha Sh.milioni 42 kwa ajili ya kulipia matibabu hayo."Hivyo tunaamini kutoa msaada huu wa BP Mobile Machine utasaidia katika kuwatibu wanachama wetu pamoja na wananchi wote ambao watakwenda kupata tiba,"amesisitiza.

Ameongeza msaada huo si mwisho na kuahidi kuendelea kusaidia kadri watakavyoweza kulingana na nafasi yao na kueleza wamekuwa wakisaidia jamii katika maeneo mbalimbali.Pia Ndunguru amesema NSSF wanalo fao la matibabu na kinachofurahisha zaidi wanachama wao wamekuwa wakipata huduma za afya za magonjwa yote isipokuwa TB na Ukimwi ambayo hayo huduma zake Serikali inatoa bure.

Ameongeza hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa wanachama wao kwani wanapohitaji huduma za matibabu ya afya wanayapata kwa wakati na ya kiwango cha kuridhisha.Akizungumzia zaidi msaada huo amesema kuwa sekta ya afya nchini inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo ya uhaba wa vifaa tiba. ufanisi. 

"Suala la uboreshaji sekta ya afya nchini si jukumu la Serikali peke yake bali ni la Watanzania wote kwa ujumla kuhakikisha wanasaidia Serikali kuimarisha sekta ya afya,"amesema.Kwa upande wa Katibu wa Hospitali ya Temeke Lilian Mwanga amesema mashine hizo za kupima shinikizo la damu zimekuja wakati muafaka kwani hivi sasa robo ya wagonjwa wanaowapokea kwa siku wanasumbuliwa na shinikizo la damu.

"Kupatikana kwa mashine hizi 12 inafanya tuwe ne jumla ya mashine 27 kwani tulipata msaada wa mashine 15 siku za karibuni.Katika hospitali yetu tunapokea wagonjwa wengi wenye shinikizo la damu."Wengi wao ni wazee lakini nishauri tubadilishe mwenendo wa maisha yetu, tufanye mazoezi na tusiwe tunakula vyakula vyenye mafuta mengi,"amesema.

Amewapongeza NSSF kwa msaada huo na kwamba wanatoa ombi tena na kwa NSSF kuendelea kuwasaidia vifaa tiba.

Kaimu Meneja Kiongozi wa NSSF Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam Barnabas Ndunguru (wa pili kulia) akimkabidhi Ofisa Muuguzi wa Hosptali ya Temeke,Deodata Msoma vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi  milioni tano
Picha ya pamoja
Kaimu Meneja Kiongozi wa NSSF Mkoa wa Temeke jijini Dar es Salaam Barnabas Ndunguru (kulia) akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kukabidhi vifaatiba kwenye Hosptal ya Wilaya ya Temeke vyenye thamani ya shilingi Milioni tano .(Picha na Emmanuel Massaka wa Globu ya jamii)

No comments: