Thursday, June 28, 2018

JAFO ATOA WITO KUSAIDIA WANAFUNZI WASIOJIWEZA ILI KUINUA ELIMU

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Mhe. Selemani Jafo akitoa hotuba fupi kabla ya kukabidhi msaada wa vifaa vya shule kwa wanafunzi wasiojiweza kwa shule za msingi na sekondari Kata ya Sejeli wilayani Kongwa mkoani Dodoma leo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Mhe. Selemani Jafo akitoa msaada kwa baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kata ya Sejeli kama sehemu ya kampeni ya
Nipe kalamu na daftari na mimi nisome
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Mhe. Selemani Jafo akipokea msaada wa daftari na penseli kutoka kwa wawakilishi wa walimu wazalendo kutoka chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) ambapo walichangia daftari 120, kalamu 115 na penseli 70
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Mhe. Selemani Jafo akiongea na walimu wazalendo kutoka chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) waliofika kijijini Mbande wilayani Kongwa Dodoma kuunga mkono kampeni ya nipe daftari na peni na mimi nisome.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Mhe. Selemani Jafo akipokea msaada wa daftari kutoka kwa Viongozi wa Chama cha Waganga wa Tiba Asilia Tanzania (UWAWATA (T)) waliochangia madaftari elfu mbili katika kuunga mkono kampeni ya nipe daftari na peni name nisome kijijini Mbande wilayani Kongwa leo.
Rosemary Chimya mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya sekondari Sejeli kijiji cha Mbande akisalimiana na waziri Jafo baada ya kutoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo kwa msaada wa vifaa vya kusomea, ameiomba Serikali kuwajengea mabweni ili kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shuleni pia kuwaongezea walimu wa masomo ya sayansi.


Na. Zulfa Mfinanga na Fred Kibano,

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo, leo amekabidhi msaada wa vifaa vya shule kwa wanafunzi wasiojiweza wa shule ya msingi na sekondari za Kata ya Sejeli kijijini Mbande wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Msaada huo utanufaisha zaidi ya wanafunzi mia tisa ni pamoja na madaftari 9,000, kalamu 4,000, penseli 2,800, vifutio 1,200 na vichongeo 1,200 vyote vikiwa ni msaada kutoka kwa watumishi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Makao makuu kwa lengo la kuunga mkono Programu ya  “Nipekalamunadaftarinamiminisome” iliyozinduliwa mwezi Februari mwaka huu na Mhe Jafo ili kuwasaida wanafunzi wanaotoka katika familia duni.

Akikabidhi msaada huo katika shule ya sekondari Sejeli Mhe Jafo amesema licha ya kuwa serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia elimu lakini gharama za vifaa vya shule pamoja na sare za shule zinatakiwa kugharamiwa na wazazi au walezi, hivyo baada ya kuona kuna changamoto ya kipato kwa baadhi ya familia ndio sababu pekee ya kuanzisha Programu hiyo.

“Leo wadau wameamua kurudisha fadhila kwa watoto ambao wazazi ama walezi wao hawana uwezo, hili jambo ni kubwa sana tena ni jambo la Ibada, nina kila sababu ya kuwashukuru na kuwaombea, niwasihi watanzania wote waunge mkono jitihada hizo ili Sera ya Elimu Bila Malipo isaidie kuondoa tofauti kati ya wanaojiweza na wasio jiweza” Alisema Mhe Jafo.

Katika hatua nyingine Mhe. Jafo alipokea msaada wa vifaa kama hivyo kutoka kwa Chama cha Umoja wa Waganga wa Tiba Asilia Tanzania (UWAWATA (T)) waliochangia madaftari elfu mbili, huku walimu wazalendo kutoka chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) wakichangia daftari 120, kalamu 115 na penseli 70 pamoja na ahadi ya daftari 4,400 kutoka ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kongwa pamoja na madiwani wa halmashauri hiyo.

Aidha, Waziri Jafo ametoa agizo kwa maafisa wa ofisi yake na halmashauri ya Kongwa katika mwaka ujao wa fedha kujenga walau mabweni mawili ya kuanzia kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu kwa baadhi ya wanafunzi wa sekondari ya Sejeli.


Awali Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ambaye pia ni Afisa Elimu Sekondari wilaya ya Kongwa Bwana Nelson Milanzi alisema kuwa wilaya hiyo ina wanafunzi 87,185 wa shule za msingi na sekondari kati ya hao wanafunzi 3,523 sawa na asilimia 4.637 wa shule za msingi wana uhitaji wa vifaa vya shule na kusema kuwa kuanzishwa kwa Programu hiyo kutasaidia kuongeza mahudhurio pamoja ufaulu wa wanafunzi.

Naye, Mratibu wa Kitaifa wa Programu ya NIPE DAFTARI NA KALAMU NAMI NISOME, Dkt. Ombeni Msuya amesema wanalengo la kufika nchi nzima lakini pia kuwafundisha wanafunzi suala la uzalendo ili hapo baadaye nao wawasaidie watu wengine wenye mahitaji.

“Tuna lengo la kufika nchi nzima sanjari na kuanzisha kambi maalumu ya kuchangia elimu ili kuwafikia wanafunzi wote wenye uhitaji huu, lakini pia tutakuwa tunatoa elimu ya uzalendo ili vijana wetu waje kuwa wazalendo hapo baadaye ili likitokea jambo kama hili wawe mstari wa mbele kama wanavyofanya wadau wengine”

Akitoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Rosemary Chimya mwanafunzi wa kidato  cha pili shule ya sekondari Sejeli iliyopo Mbande, mbali na kumshukuru Waziri Jafo kwa kuanzisha programu hiyo lakini aliiomba serikali iwajengee mabweni kwa ajili ya kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shuleni pamoja na kuwaongezea walimu wa sayansi,vitabu na madawati.

No comments: