Saturday, June 23, 2018

NILIJUA TU KUNA SIKU CHAKA CHAKA ATANITAFUTA...SASA LEO KIKO WAPI?

MWENYEZI Mungu ambaye ni mwingi wa rehema na mwingi wa ukarimu amekuwa nami siku zote.Ahsante Mungu kwa kunipenda na kunifanikisha kila ninachotamani.

Baada ya utangulizi huo iko hivi ujue katika makuzi yangu au sijui ndio niseme katika kukua kwangu moja ya wanamuziki ambao wananivutia sana katika Bara la Afrika ni pamoja na Vyone Chaka Chaka.

Ni mwanamuziki maarufu sana nchini Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla.Unajua kwanini nilianza kumpenda kitambo?

Jibu ni hivi siku za nyuma nilikuwa muumini sana wa kuangalia sinema katika vibanda.Tena hiyo ilikuwa huko kwetu Kimamba wilayani Kilosa mkoani Morogoro.Zamani kidogo.Basi bwana kila nikienda kuangalia sinema kabla ya kuwekwa picha la Komandoo Kipesi au Bluce Lee ama Check Norisi basi tukawa tunapata nafasi ya kuangalia nyimbo za wanamuziki mbalimbali.

Mwanamuziki Chaka Chaka alinivutia sana ingawa kwenye viuno pamoja na udogo wangu kwa wakati ule kura zangu nilimpa Yondo Sister.Sijui hata yuko wapi siku hizi huyu dada.Hata hivyo leo sina sababu ya kumzungumzia.Leo nipo kwa Chaka Chaka.

Ukweli Chaka Chaka alinivutia sana tangu wakati huo, sasa kwa ujinga wangu nikawa natamani siku moja nikutane naye.Hata hivyo kwa ukabwela wangu huu nikawa najiuliza nitakutana naye wapi?Nikawa najipa moyo na matumaini ipo siku Mungu atamleta karibu yangu.

Unajua kilichotea?Acha nikupe umbea juzi nikapata nafasi ya kushiriki kwenye katukio fulani hivi ambacho kilifanyika Hyatt Regency The Kilimanjaro. Kuna kampuni ilikuwa inazindua jina jipya.

Ile naingia kwenye ukumbi nikaanza kujisikia moyo, mwili na akili vyote vinafuraha.Nikaanza kujiuliza kuna nini leo? .Kabla sijajijibu ile nataza mbele tu macho yangu ana kwa ana na macho ya mwanamama Chaka Chaka.Nikasema si ndio nilikuwa namtafuta siku zote?

Ni kweli ni yeye ?Mbona amejileta mwenyewe? Kwanini leo?Kwanini iwe Dar es Salaam?, Nikajikuta naropoka tu bila aibu leo niliyekuwa namtafuta nimempata kiuarahisi.Mungu ana maajabu yake.

Nikaona isiwe tabu nikamsogela mama wa watu(Mzuriii).Hata hivyo kwa namna ambavyo nilikuwa namuangalia inaonesha naye alikuwa ananitafuta siku nyingi.

Basi bwana nikamsalimia na cha kwanza kumwambia ni kwamba Chaka Chaka nimekuwa nikitamani kukuona na hatimaye leo nimekuona.Akanijibu ahsante...nikaaza kumtajia baadhi ya nyimbo zake ambazo zilinifanya nivutiwe nawe.

Nikumbushe tu Yvonne Chaka Chaka jina lake halisi ni Yvonne Machaka na alizaliwa mwaka 1965.Wengi wanamuita Malkia wa Afrika", Chaka Chaka amekuwa mstari wa mbele katika muziki.

Basi ndugu yangu nimtajia ile nyimbo yake ya I'm Burning Up, I'm in Love With a DJ, I Cry for Freedom, Makoti,Motherland na ile ambayo ikuwa inanivutia sana ya Umqombothi yaani Pombe Ya Afrika.

Baada ya kumtajia akaniambia kweli una haki ya kunitafuta.Akaongeza kwa kuniambia kweli mimi nishabiki yake.Kimya kimya tena nikiwa pembeni yake nikasema hapo sawa sasa mambo si ndiyo haya. Kwa ujasiri mkubwa kimoyo moyo nikawa najiseme mwenyewe nilijua tu kuna siku Chaka Chaka utanitafuta ...sasa leo kiko wapi?Sikutaka kusema kwa nguvu asikie.

Kwa kuwa teknolojia imekuwa basi nikachukua kasimu kangu cha Smat phone na kisha nikampa jamaa yangu mmoja tukapiga picha.Ndio kama unavyoiona? Unachochote cha kuniambia? karibu

No comments: