Watendaji wa Halmashauri pamoja na wafanyabiashara wadogo wa Mkoa wa Njombe wameelimishwa juu ya urasimishaji wa wafanyabiashara hao ili waweze kutambulika rasmi na kuchangia pato la taifa ikiwa ni katika muendelezo wa Kampeni ya utoaji wa Huduma, Elimu na usajili wa walipakodi wapya.
Akizungumza wakati wa semina kwa watendaji na wafanyabiashara hao wilayani Njombe na Makambako, Mkuu wa Wilaya ya hiyo Bi. Ruth Msafiri amewataka wafanyabiashara hao kuchangia mapato ya Serikali kwa kulipa kiasi cha kodi watakachopangiwa ili kuweza kusaidia kuboresha miundombinu pamoja na huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo shule, huduma za afya, maji safi na salama, umeme pamoja na barabara.
“Tukumbuke kuwa, kila kitu tunachokifanya kinahitaji fedha kwa mfano kuwa na miundombinu na wataalam wa kutoa huduma za afya ni gharama, kuwa na shule pamoja na sehemu safi za kufanyia biashara ni gharama pia. Hivyo basi, kila mmoja achangie kwa kulipa kodi ili kuweza kuendeleza huduma hizi muhimu”. Alisema Ruth.
Aliongeza kuwa, katika kutafuta maendeleo kitu kikubwa ambacho kila mwananchi anatakiwa kuwa nacho ni uzalendo, utayari na kuelewa kwamba kila mmoja ana mchango wake katika maendeleo husika.
Aidha alisisitiza kwamba, lengo la semina hiyo ni kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wadogo wadogo wa Mkoa wa Njombe wanapokea na kutekeleza maagizo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwarasimisha rasmi ambapo hadi sasa Wilaya ya Njombe imekwisha orodhesha jumla ya wafanyabiashara 589 na wengine wanaendelea kujiorodhesha ili baadaye waweze kupatiwa vitambulisho maalum vya wafanyabishara wadogo.
Naye Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard Kayombo, aliwataka wafanyabiashara hao kutoa ushirikiano kwa watendaji wa Halmashauri ili waweze kuwatambua na kurahisisha zoezi zima la usajili pindi litakapofika mkoani Njombe.
“Tumefanya zoezi la utambuzi wa wafanyabiashara wadogo wadogo katika Mkoa wa Mwanza, Arusha na Morogoro hivyo ni matumaini yangu kuwa wafanyabiashara wa Njombe mtaitikia zoezi hili kwa kiasi kikubwa pindi tutakapofika mkoani hapa”. Alisema Kayombo.
Kayombo aliongeza kuwa, huduma mbalimbali za kijamii kama shule, hospitali pamoja na miundombinu zimechangiwa kwa kiasi kikubwa na walipakodi wakubwa na walipakodi wa nchi rafiki wa Tanzania hivyo basi imefika wakati kwa wafanyabiashara wadogo kuchangia kiasi kidogo wanachikipata ili kusaidia maendeleo ya nchi.
“Wananchi wengi wamekuwa wakiamini barabara zetu zinatengenezwa kwa misaada ya wahisani, jambo hili siyo kweli isipokuwa Serikali imekuwa ikipokea mikopo yenye masharti nafuu ambayo kodi za wananchi ndizo zimekuwa zinalipa madeni hayo” aliongeza Kayombo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wafanyabiashara hao, Sifael Msigalla aliishukuru TRA kwa kuhakikisha inafikisha elimu ya kodi kwa wafanyabiashara wadogo ambayo itasaidia wafanyabiashara hao kuweza kwenda sawa na malengo ya Taifa katika kukuza Uchumi wa Viwanda.
“Elimu waliyoipata leo itasaidia sana wafanyabiashara hawa kulipa kodi na hivyo kupelekea kufanya biashara zao huku wakiwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi,” alisema Msigalla.
Jumla ya wafanyabiashara wadogo 200 wamehudhuria semina hiyo iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania ambapo Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Ruth Msafiri alikuwa Mgeni Rasmi.
No comments:
Post a Comment