Saturday, May 5, 2018

Wizara ya Mambo ya Nje yajipanga kutekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda


Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wametakiwa kufanya kazi kwa weledi ili kutimiza malengo ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Kauli hiyo ilitolewa leo jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Waziri Mahiga alieleza kuwa Wizara inatakiwa kuweka Sera na mikakati ya utekelezaji kwa kuzingatia miongozo na maelekezo ya Viongozi wa juu akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. “Sera ya Serikali ya awamu ya tano ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, hivyo Sera yetu ya Mambo ya Nje lazima ijikite katika diplomasia ya uchumi wa viwanda”. Dkt. Mahiga alieleza.

Dkt. Mahiga alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka watumishi kuhakikisha kuwa Wizara inatekeleza majukumu yake kwa kujiwekea ratiba ya kuyakamilisha kwa kuzingatia hotuba za Mhe. Rais Magufuli alizozitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kikao cha Mabalozi na Mhe. Rais Magufuli na kikao cha watumishi wa Wizara na Mhe. Rais Magufuli. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Wizara yake imejipanga ipasavyo kuhakikisha kwamba jukumu la kuchochea uchumi wa nchi kupitia Sera ya Mambo ya Nje inayojikita katika diplomasia ya uchumi inatekelezwa kikamilifu.

Prof. Mkenda alisema Wizara kwa kushirikiana na ofisi zake za Ubalozi, licha ya changamoto mbalimbali inazokutana nazo, lakini imekuwa ikitafuta fursa za uwekezaji, mitaji, masoko, utalii na elimu na kuzileta nchini ili kufikia azma ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020.

Alizitaja Balozi chache zilizoleta wafanyabiashara wakubwa kwa ajili ya kutafuta fursa za uwekezaji nchini kuwa ni pamoja na Balozi za Tanzania nchini China, Ufaransa, Korea Kusini, Kenya, Ujerumani na Israel. "Balozi wetu China, Mhe. Mbelwa Kairuki ametafuta taasisi za kifedha kwa ajili ya kuzikopesha benki za Tanzania ili zikuze mitaji ya kutoa mikopo kwa wawekezaji. Aidha, Serikali ya Ujerumani imefungua ofisi maalum kwa ajili ya kuratibu na kusaidia shughuli za kibiashara na uwekezaji hapa nchini" Prof. Mkenda alisema.

Prof. Mkenda alisifu jitihada zilizofanywa na Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya hivi karibuni za kuandaa maonesho ya bidhaa za viwanda vya hapa nchini yaliyofanyika jijini Nairobi tarehe 25 - 28 Aprili 2018. Alisema maonesho hayo ya kipekee yalikuwa na mafanikio makubwa ambapo wafanyabiashara walioshiriki waliingia makubaliano na wafanyabiashara wa Kenya ya kupeleka bidhaa zao nchini Kenya. 

"Tunatakiwa tuondoe vikwazo vya kufanya biashsra, kuondoa vikwazo hivyo haina maana Tanzania iwe gulio la kuuzia bidhaa kutoka nje, bali wafanyabiashara wetu wanatakiwa kuchangamkia masoko ya nje ili wauze bidhaa zao kwa wingi nje ya nchi", Katibu Mkuu alisisitiza.

Katibu Mkuu alisema ili watumishi waweze kutimiza malengo ya Wizara yakiwemo ya kuvutia wawekezaji kutoka nje, Wizara imejipanga kuwawezesha watumishi kupata elimu, ujuzi, teknolojia na uzoefu unaohitajika kutimiza majukumu hayo.

Kuhusu suala la kupeleka watumishi kwenye vituo vya Ubalozi, Katibu Mkuu alieleza kuwa Wizara itatekeleza jukumu hilo kwa haki kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa ambavyo ni weledi, ujuzi na mahitaji ya Balozi husika. “Wizara haitapeleka watumishi vituoni kutokana na shinikizo au kuangalia sura, kabila na dini ya mtu ili kuondoa malalamiko yaliyokuwepo kwa muda mrefu Wizarani. 


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 
Dar es Salaam
05 Mei, 2018

No comments: