Saturday, May 5, 2018

SERIKALI YAELEZA FURSA YA UFUGAJI WA NYUKI HAPA NCHINI - NAIBU WAZIRI JAPHET HASUNGA

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (katikati) akizungumza na wadau wa sekta ya ufugaji nyuki nchini katika kikao alichokiitisha kujadili maendeleo ya sekta hiyo ikiwemo marekebisho ya kanuni za ufugaji nyuki za mwaka 2017 katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo. Kushoto ni MKuu wa Kitengo cha Masoko, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Mwanahamisi Mapolu na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara hiyo, Deosdedit Bwoyo.

Na Hamza Temba - Dodoma
.............................................................

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa kubwa iliyopo hapa nchini ya ufugaji nyuki na uwepo wa masoko ya ndani na nje ya nchi kwa kuongeza uzalishaji wa mazao yake na kuyaongezea thamani ili kuinua uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Ametoa wito huo leo mbele ya wadau wa sekta ya ufugaji nyuki kutoka mikoa yote nchini katika mkutano aliouitisha kujadili maendeleo ya sekta hiyo ikiwemo marekebisho ya kanuni za ufugaji nyuki za mwaka 2017 katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.

Amesema kwa sasa mchango wa sekta ya nyuki katika pato la taifa bado ni mdogo ukilinganisha na fursa zilizopo za ufugaji nyuki hapa nchini ambazo zikitumiwa ipasavyo zitasaidia kuinua pato la wananchi na taifa kwa ujumla.

Amesema mbali na kuongeza uzalishaji, mazao hayo pia yanatakiwa kuongezewa thamani na kuwekewa ngazi za ubora ili yaweze kuhimili masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ameongeza kuwa, ili kuimarisha sekta hiyo Serikali itashirikiana na wadau kutatua changamoto zilizopo ikiwemo kutafuta masoko, kuimarisha uwekezaji na kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata mazao ya nyuki ikiwemo asali na nta ambayo ina soko kubwa nje ya nchi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa wizara hiyo, Deosdedit Bwoyo amesema Tanzania ni moja kati ya nchi 50 duniani zenye utajiri mkubwa wa rasilimali za misitu ambazo zinatoa fursa pana ya ufugaji nyuki nchini.

Amesema eneo la misitu ni takriban hekta milioni 48.1 ambalo ni asilimia 54 ya ukubwa ardhi yote ya Tanzania ambayo ikitumiwa ipasavyo na wananchi itawawawezesha kujiajiri na kuongeza uzalisahaji wa mazao ya nyuki na mapato.

Amesema ili kulinda mazalia ya nyuki na kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki nchini, Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS, imeanzisha hifadhi za nyuki 11 huku Serikali za vijiji zikianzisha hifadhi za nyuki 14.

Wadau walioshiriki mkutano huo ambao ni wazalishaji, wachakataji na wasafirishaji wameishukuru Serikali kwa kuandaa mkutano huo na kuiomba kusaidia katika tafiti, elimu kwa wananachi wanaojihusisha na ufugaji nyuki hususan maeneo ya vijijini na utafutaji wa masoko ya uhakika.Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kushoto) akizungumza na wadau wa sekta ya ufugaji nyuki nchini katika kikao alichokiitisha kujadili maendeleo ya sekta hiyo ikiwemo marekebisho ya kanuni za ufugaji nyuki za mwaka 2017 katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo.Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Deosdedit Bwoyo akiwasilisha hotuba yake kwa wadau hao.Mkurugenzi Msaidi wa Uendelezaji Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Allen Richard akitambulisha meza kuu katika mkutano huo.Wadau wa Misitu na Nyuki wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi ambaye ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (hayupo pichani). Katikati ni Magdalena Muya wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Stephen Msemo kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (kulia).Baadhi ya wadau walioshiriki mkutano huo.Mmoja ya wadau wa sekta ya ufugaji nyuki nchini akitoa maoni yake.Mmoja ya wadau wa sekta ya ufugaji nyuki nchini akitoa maoni yake.Picha ya pamoja ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga na wadau wa sekta ya ufugaji nyuki nchini wakati wa kikao alichokiitisha kujadili maendeleo ya sekta hiyo ikiwemo marekebisho ya kanuni za ufugaji nyuki za mwaka 2017 katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo.Picha ya pamoja ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga na wadau wa sekta ya ufugaji nyuki nchini wakati wa kikao alichokiitisha kujadili maendeleo ya sekta hiyo ikiwemo marekebisho ya kanuni za ufugaji nyuki za mwaka 2017 katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo.

No comments: