Wednesday, May 9, 2018

WATUMISHI WANAWAKE ILALA WAANZA KAMPENI KUFANIKISHA UJENZI CHOO CHA MTOTO WA KIKE

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
WATUMISHI Wanawake katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam wameamua kuanzisha kampeni maalumu ya ujenzi wa Choo cha mtoto wa kike kwa kuanza na shule zote za msingi katika manispaa hiyo.

Hivyo uzinduzi wa kampeni hiyo unatarajiwa kufanyika Oktoba 11 mwaka huu na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema na imani yao ni kwamba wadau mbalimbali wataungana na watumishi hao katika kufanikisha ujenzi wa choo cha mtoto wa kike.

Mratibu wa kampeni hiyo ambaye pia ni Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala Tabu Shaibu amesema leo jijini Dar es Salaam kuwa watumishi wanawake wa manispaa hiyo wanatambua na kuthamini jitihada kubwa za Serikali na wadau wa maendeleo za kukabiliana na changamoto za mtoto wa kike.

Akitoa sababu za ujenzi wa choo cha mtoto wa kike, Shaibu amesema kila ifikapo Oktoba 11 ya kila mwaka ni siku ya Kimataifa ya Mtoto wa kike duniani na lengo la maashimisho hayo ni kuilimisha na kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kutetea haki za mtoto wa kike.

"Tafiti zimefanyika kuhusu sababu zinazochangia mahudhurio hafifu ya mtoto wa kike darasani hasa  wa darasa la saba na takwimu zao zinabainisha wasichana wa darasa la saba hawahudhurii shuleni kati ya siku nne hadi tano kila mwezi.Vyoo visivyofaa kwa matumizi hasa kwa wasichana wanaoingia hedhi huleta changamoto kubwa kwao.

"Kutokana na changamoto hiyo watumishi wanawake wa Manispaa ya Ilala wameona wanao wajibu wa kuunga mkono juhudi za Serikali na kuendelea kuihamasisha jamii na wadau kujenga choo bora cha kisasa kitakachokuwa rafiki kwa mtoto huyu wa kike,"amesema Shaibu.

Amefafanua watumishi wanawake kupitia michango yao wameamua kujenga choo cha mfano katika Shule ya Msingi Chanika na kusisitiza hamasa ya kujenga choo cha mtoto wa kike itaongozwa na kauli mbiu inayosema hivi "Binti makini mwavuli wangu stara".

Shaibu amesema binti makini ni yule anayejitambua na kujua thamani yake kwa kuwa na maadili mazuri na hodari wakati mwamvuli unatoa tafsiri ya kifaa cha kujikinga na changamoto mbalimbali ikiwemo ya miundombinu ya choo , hivyo mwamvuli katika kauli mbiu yao inawakilisha choo.

Pia amesema stara ni neno lialoaminisha kusitiri hivyo choo cha kisasa kitampa mtoto wa kike stara ya kutosha ili binti huyo aweze kufikia malengo yake.

"Uwepo wa choo maalum cha mtoto wa kitamuwezesha kukaa shuleni muda mrefu na kushiriki  masomo kikamilifu badala ya kubakia kukaa nyumbani wakati wa hedhi hali inayoathiri mtiririko wa mahudhui ya yale yaliyofundihswa na kusababisha matokeo duni ya kitaaluma.

"Kampeni ya ujenzi wa choo cha mtoto wa kike itaanza kwenye shule 120 za msingi zilizopo kwenye manispaa ya Ilala na kuendelea katika shule za sekondari.Choo kitakachojengwa kitakuwa na matundu 10 , maji ya kutosha , masinki ya kunawia mikono , kabati la kuhifadhi taulo la kike ,kioo na sehemu ya kuchomea taka.Gharama za choo hiki zinakadiriwa kufikia Sh.milioni 20,"amesema Shaibu.

Ametoa ombi kwa wadau mbalimbali kuchangia fedha kupitia akaunti CRDB Miscleneous deposit account no 0150251270500 Municipal Council.Mbali ya michango ya fedha pia wanapokea vifaa vya aina mbalimbali vya ujenzi ambapo tayari kuna baadhi ya wadau wameanza kuunga mkono kampeni hiyo kwa kuchangia.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa kampeni hiyo ambaye pia ni Ofisa Elimu Msingi Manispaa ya Ilala Elizabeth Thomas amesema ujenzi wa vyoo hivyo utakwenda sambamba na utoaji elimu kwa wananchi itakayosaidia kutunzwa kwa miundombinu ya shule.

Amesema kuna baadhi ya watu wamekuwa na utamaduni wa kuharibu miundombinu ya shule kwa kuharibu milango kwa kuchukua mbao kwenda kuchomea samaki au kupikia na zipo baadhi ya shule ambazo ni mpya lakini milango tayari imeharibiwa.

Hivyo ametoa rai kwa wananchi kila mmoja kuona  na kuamini kuwa miundombinu ya shule ni mali ya kila Mtanzania na inapaswa kutunzwa.Kuhusu kampeni ya choo cha mtoto wa kike amesisitiza umuhimu wa wadau kujitokeza na kuchangia fedha na vifaa vya ujenzi ili kuifanikisha.
Mratibu wa Kampeni cha ujenzi cha choo cha Mtoto wa kike ambaye pia ni Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, Tabu Shaibu (katikati) akizungumzia maandalizi ya uzinduzi rasmi wa kampeni hiyo unaotarajia kufanyika Oktoba 11 mwaka huu katika hoteli ya Lamada. Kulia ni Mwenyekiti wa kampeni hiyo na Ofisa Elimu Msingi manispaa ya Ilala Elizabeth Thomas na kushoto ni moja ya wajumbe wa kampeni hiyo.

No comments: