NA JOHN MAPEPELE, MWANZA
WAKUU wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria wamekosoa vikali tabia ya baadhi ya wanasiasa kuipaka matope dhamira njema ya Serikali ya kupambana na uvuvi haramu ulioshamiri katika ziwa hilo na kutaka viongozi wa aina hiyo kutangaza masilahi yao kwenye eneo la uvuvi kabla ya kuwashambulia viongozi wanaosimamia zoezi hilo kwa misingi ya kisheria.
Wakizungumza kwenye kikao cha tathmini ya operesheni sangara awamu ya pili iliyowahusisha Wakuu wa Mikoa,Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Makamanda wa Polisi wa mikoa na Wakuu wa Idara ya Usalama wa Taifa wa mikoa yote inayozunguka Ziwa Victoria jijini Mwanza jana viongozi hao wametaka hatua zaidi zichukuliwe ili kunusuru rasilimali hizo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka alielezea kuchukizwa na tabia inayoanza kuota mizizi ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuipaka matope dhamira nzuri ya Serikali ya kukabiliana na uvuvi haramu na kutaka viongozi wa aina hiyo watangaze masilahi yao kabla ya kuanza kuwashambulia viongozi wanaosimamia operesheni hiyo inayotekelezwa kwa mujibu wa sheria .
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akihutubia hadhara ya kikosi kazi cha watu 260 alichokiunda kwa ajili ya operesheni Sangara 2018 na Wakuu wa Mikoa mitano inayozunguka Ziwa vicktoria wakati wa mkutano wa kufanya tathimini ya Operesheni hiyo. Picha na John Mapepele
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akihutubia hadhara ya kikosi kazi cha watu 260 alichokiunda kwa ajili ya operesheni Sangara 2018 na Wakuu wa Mikoa mitano inayozunguka Ziwa vicktoria wakati wa mkutano wa kufanya tathimini ya Operesheni hiyo. Picha na John Mapepele
Viongozi wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliokaa wakiwa katika picha ya pamoja na makamanda wakuu wa Operesheni Sangara 2018 (waliosimama) wakati wa mkutano wa kufanya tathimini ya Operesheni hiyo.
“Viongozi wanaopinga operesheni ya kupambana na uvuvi haramu ni muhimu watangaze kwanza masilahi yao kuhusu eneo la uvuvi ili wasiendelee kuchafua taswira za viongozi wanaosimamia wizara hii”alisema Mtaka.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela alisema kumekuwepo na dhana zinazojengeka kwamba viongozi wa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria hawaungi mkono mapambano ya kukabiliana na uvuvi haramu operesheni jambo ambalo alisema ni upotoshaji mkubwa na kwamba Serikali ya mkoa iko mstari wa mbele na kuwabana watendaji wa ngazi zote watakaobanika kufadhili uvuvi haramu.
Alisema ni muhimu operesheni hiyo iwe endelevu na kubainisha kuwa suala la uvuvi haramu haliwezi kumalizika kama hakuna dhamira ya dhati miongoni mwa wasimamizi wa sheria na kwamba uongozi wa mkoa huo hautakubali kuendelea kuwa na watumishi wazembe wataoshindwa kusimamia suala hilo.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina alitangaza kuanza kwa awamu ya tatu ya Operesheni Sangara yenye lengo la kupambana na uvuvi haramu katika Ziwa Victoria sambamba na kutangaza operesheni katika maziwa yote na kuagiza viongozi wakuu wa mikoa na wilaya kuwachukulia hatua kali viongozi wa chini wanaobanika kujihusisha na kufadhili uvuvi haramu.
Viongozi wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliokaa wakiwa katika picha ya pamoja na sekretarieti ya Operesheni Sangara 2018 (waliosimama) wakati wa mkutano wa kufanya tathimini ya Operesheni hiyo.
Pia alitangaza kuunda kanda mpya ya udhibiti na usimamizi rasilimali za uvuvi katika wilaya za Ukerewe na Sengerema huku akiunda ofisi mpya ya Kanda jijini Mwanza itakayokuwa inaratibu shughuli zote katika kanda hizo saba ili kuongeza usimamizi madhubuti wa rasilimali hizo.
Aidha Mpina aliongeza kuwa katika awamu ya tatu ya operesheni hiyo itahusisha pia Mahakama zinazotembea ili kuweza kutoa hukumu huko huko ziwani hali itayowezesha kuondokana kabisa na uvuvi haramu.
Aidha aliwataka watu wote wanaopinga operesheni ya uvuvi haramu wasome takwimu ili kujua ukubwa wa tatizo katika Ziwa Victoria ambapo jumla ya watuhumiwa 3,284 wamekamatwa kujihusisha na uvuvi haramu huku samaki wasioruhusiwa kilo 326,751 , mabondo kilo 5,142 zilikamatwa zikitoroshwa kwenda nje ya nchi na nyavu haramu 566,497 nazo zilikamatwa na kuteketezwa. Pia magari 257, mitumbwi 1278 , pikipiki 269 na injini za mitumbwi 564 vilikamatwa vikihusishwa na makosa ya uvuvi haramu.
Alisema katika baadhi ya maeneo ya Bushengere wilayani Ukerewe wazazi wamewaonya watoto wao kutotumika na mafisadi kwenye uvuvi haramu kwani wakikamatwa wao ndio wanaopata tabu na kutelekezwa ambapo wameweka azimio la kukataa kutumika tena kwenye jambo hilo.
Alisema kutokana na operesheni hizo zinazoendelea za kupambana na uvuvi haramu hadi kufikia mwezi Disemba mwaka huu watu wote wanaopinga na hata kuwaombea mabaya viongozi wa operesheni watapata aibu kubwa kwani idadi ya samaki itaongezeka huku akitoa wito kwa viongozi wa ngazi zote wenye mapenzi mema na nchi kuunga mkono vita hiyo kwa manufaa ya Taifa.
Katibu Mkuu Uvuvi, Dk. Yohana Budeba alisema wizara hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha sekta ya uvuvi inatoa mchango mkubwa katika pato la Taifa na kwamba operesheni hiyo itaendelea hadi pale uvuvi haramu utakapokoma.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera alisema wamekuwa wakipokea malalamiko mengi kuhusu operesheni hiyo lakini kila walipofuatilia kupata ushahidi wa malalamiko hayo waliukosa jambo ambalo wamebaini kuwa ni njama za makusudi za kutaka kuhujumu nia njema ya Serikali ya kupambana na kutokomeza uvuvi haramu.
Kamanda Mkuu wa operesheni hiyo kutoka Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Hassan Shelukindo alisema katika operesheni hiyo jumla ya watuhumiwa 22 wakiwemo wenyeviti wa vijiji na vitongoji na viongozi wa BMU wamefungwa jela huku wengine 17 mashauri yao yakiwa yanaendelea Mahakamani kwa makosa ya kujihusisha na uvuvi haramu.
Shelukindo alisema pia watumishi 6 walikuwa kwenye operesheni hiyo waliondolewa kwa makosa mbalimbali ikiwemo ukiukwaji wa maadili ya kazi ambapo watumishi hao watachukuliwa hatua za kinidhamu na taasisi zao huku jumla ya sh. bilioni 7.5 zikikusanywa kutokana na faini pamoja mauzo ya mabondo,samaki na kayabo.
No comments:
Post a Comment