Tuesday, May 22, 2018

Riadha Tanzania wampongeza Mkurugenzi mpya MultiChoice

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limempongeza Mkurugenzi wa MultiChoice Tanzania, Maharage Chande kwa kuteuliwa kuwa Mkurugenzi mpya wa MultiChoice Kanda ya Afrika Mashariki na Magharibi.

Mei 20 mwaka huu, Kampuni ya MultiChoice Africa Limited, ilithibitisha uteuzi wa Wakurugenzi wawili, ambako Mtanzania Maharage Chande ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania, anakuwa Mkurugenzi mpya wa Kanda ya Afrika Mashariki na Magharibi.

Uteuzi huo uliotangazwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa MultiChoice Africa, Brand de Villiers, unabainisha kuwa Maharage anachukua nafasi ya Stephen Isaboke aliyekuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki ambaye sasa anakuwa Mkuu wa Mamlaka (Group Executive Head of Regulatory). Uteuzi ambao unaanza Juni Mosi mwaka huu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa MultiChoice Africa, Brand de Villiers, amesema uteuzi wa Maharage umezingatia uwezo na upeo wake mkubwa aliyouonyesha katika kipindi alipoiongoza MultiChoice Tanzania tangu alipojiunga nayo Juni 2016.

Rais wa RT, Anthony Mtaka, amesema familia ya Riadha Tanzania imepokea kwa furaha uteuzi huo wa Maharage, hasa ukizingatia katika uongozi wake, MultiChoice Tanzania kupitia DStv, imekuwa mshirika mkubwa katika kuchangia maendeleo ya mchezo wa Riadha hapa nchini.

“Sisi kama Riadha Tanzania, tumepokea kwa faraja kubwa kupanda kwa cheo kwa Mtanzania mwenzetu Maharage Chande, hakika tutamkumbuka kwa mengi katika kusapoti maendeleo ya Riadha hapa nchini….Tunamtakia kila la heri katika majukumu yake mapya na bila shaka mapenzi yake katika mchezo wa Riadha atayaendeleza,” alisema Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.

Mtaka, alibainisha baadhi ya mchango wa MultiChoice Tanzania chini ya Maharage katika Riadha Tanzania, ni kutayarisha timu na wachezaji wa Riadha katika mashindano mbalimbali.

“Ni uthubutu wa Mkurugenzi Mtendaji Maharage Chande aliamua kumdhamini Mwanariadha Alphonce Felix Simbu baada ya mashindano ya Olimpiki Rio de Jeneiro Brazil alipoibuka namba 5 na hatimaye kuja akiwa namba 3 katika mashindano makubwa ya Dunia huko London 2017.

“Maharage akiwa Mtendaji Mkuu wa MultiChoice Tanzania, ameendelea kuunga mkono Timu ya Riadha Tanzania ambapo mwaka huu kampuni yake ilitoa fedha za maandalizi kwa ajili ya mashindano ya Jumuiya ya Madola,” alisema Mtaka na kuongeza.

Na hivi majuzi Maharage amempa udhamini mchezaji mwingine wa Riadha ili aweze kufanya maandalizi ya mashindano ya Dunia yatakayofanyika nchini Qatar 2019.

“Ukiacha hilo, MultiChoice Tanzania pia ilikuwa bega kwa bega na RT katika kuimarisha ushirikiano wa wanafamilia ya Riadha na Wadau wake wakiwamo waandaaji wa matukio mbalimbali ya mchezo wa Riadha,” alisema Mtaka na kuongeza.

Sisi kama Riadha Tanzania tunampongeza na kumtakia heri katika majukumu yake tukiamini heshima ya nchi yetu Tanzania katika kampuni hii kubwa duniani itaendelea kuaminika na kuheshimika, na zaidi sisi kama familia ya Riadha tunaahidi kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa MultiChoice Tanzania.

No comments: