Tuesday, May 22, 2018

MSHAMBULIAJI AZAM AKIRI MAJERAHA YA NYONGA YAMEPUNGUZA KASI ALIYONAYO MSIMU ULIOPITA

Na Zainab Nyamka, Globu ya jamii

MSHAMBULIAJI wa Azam Shaaban Idd, amekiri kuwa nje ya dimba kwa takribani miezi saba akiuguza majeraha ya nyonga kulimwaribia kuendeleza kasi aliyokuwa nayo msimu uliopita.

Shaaban aliweza kuiongoza Azam FC kuichapa Tanzania Prisons mabao 4-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) akifunga hat-trick na jingine likitupiwa wavuni na kiungo Frank Domayo.

Mara baada ya Shaaban kukosa raundi ya kwanza ya ligi kutokana na majeraha aliyopata mwishoni mwa msimu uliopita, hivi sasa amerejea vema kabisa baada ya hat-trick hiyo kumfanya akikishe mabao nane kwenye ligi msimu huu, huku akiandika rekodi ya kufunga mabao sita ndani ya mechi nne zilizopita.

Mabao hayo nane yamemfanya kuvunja rekodi yake ya msimu uliopita alipopandishwa timu kubwa akitokea Azam B, na kufunga mabao sita kwenye msimu wake wa kwanza wa ligi.

Akizungumzia mchezo uliopita, Shaaban alisema ilimlazimu kuvuta subira ili kurejea kwenye ubora wake na anamshukuru Mwenyezi Mungu hivi sasa ameanza kufanya vizuri huku akiahidi makubwa zaidi msimu ujao.

“Mimi sikuanza msimu kwenye raundi ya kwanza ila nimerudi raundi ya pili, nimekaa nje ya dimba zaidi ya miezi sita kwa hiyo nipate ile kasi yangu ambayo nilimaliza nayo msimu ulioisha ilibidi ichukue muda na lazima iwe hivyo kwa sababu mpira ni mchezo unaohitaji utulivu wa akili, utimamu wa mwili.

“Miezi sita si midogo kwa sababu sikuruhusiwa hata kugusa mpira, haikuwa na maana kwamba kiwango changu kimeshuka bali nilikuwa kwenye njia ya kunifanya mimi nifanye kazi kwa bidii ili kurejea katika kiwango ambacho nilikuwa nacho, namshukuru Mungu nimejitahidi na ndio kama unavyoona nimechanganya kwenye mechi za mwisho,” alisema.

Mshambuliaji huyo ambaye mpaka sasa msimu huu ameshafunga mabao tisa kwenye mashindano yote, hakusita kuelezea furaha yake baada ya kuwa na muendeleza mzuri wa kufunga mabao, katika mechi nne zilizopita akiwa ametumbukia nyavuni mara sita.

“Ni rekodi nzuri pia mwenyewe nimeifurahia, kila mchezaji ambaye anapenda maendeleo yake na timu yake lazima acheze kwa rekodi inshallah Mungu akijalia naahidi kufanya kazi nzuri zaidi kwa ajili ya timu yangu,” alisema.

Shaaban amebakisha bao moja tu kufunga ili kufikia rekodi yake ya msimu uliopita, alipomaliza akiwa amefunga mabao 10 kwenye mashindano yote, sita kwenye ligi, moja Kombe la Mapinduzi na matatu Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) akimaliza nyuma ya aliyekuwa Nahodha wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor, aliyefunga 12 na kuwa kinara wa ufungaji ndani ya Azam FC.

No comments: