Monday, April 16, 2018

WAZIRI MWAKYEMBE: TATUENI KERO ZA WADAU KWA HARAKA NA UFANISI

 Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi Bw. Makoye Alex Nkenyenge akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi (Hayupo katika picha) wakati wa ufunguzi wa kikao cha13 cha  Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika leo Mkoani Dodoma katika Ukumbi wa Ofisi za Waziri Mkuu
 Mwenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa kufarijiana Bw. Mussa Varisanga akiwasilisha taarifa kuhusu mfuko huo wakati wa kikao cha 13 cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ,kilichofanyika leo Mkoani Dodoma.
 Afisa Ushirika kutoka Manispaa ya Dodoma Bw.Greyson Masawe akiwasilisha mada kuhusu uanzishaji wa Chama cha Kuweka na Kukopa Akiba (SACCOSS) katika  kikao cha 13 cha Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kilichofanyika leo Mkoani Dodoma.
 Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakisikiliza uwasilishwaji wa mada na taarifa mbalimbali wkatika kikao cha 13 cha Baraza hilo.
 Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakisikiliza uwasilishwaji wa mada na taarifa mbalimbali katika kikao cha 13 cha Baraza hilo.
 Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Wizara hiyo baada ya kufungua rasmi kikao cha 13 cha  Baraza la Wafanyakazi lkilichofanyika leo Mkoani Dodoma, (Picha na Lorietha Laurence, Dodoma).
Waziri wa Habari ,Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akisoma risala wakati wa ufunguzi wa kikao cha 13 cha  Baraza la Wafanyakazi lililofanyika katika Ukumbi wa Waziri Mkuu leo Mkoani Dodoma.
 

Na Anitha Jonas – WHUSM,Dodoma.


Watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wamehimizwa kutumia muda wao wa kazi kuwahudumia wananchi kwa kujibu hoja na kutatua kero zao kwa haraka na ufanisi.

Hayo yamesemwa leo Mkoani Dodoma na Waziri Mhe. Dkt. Harisson Mwakyembe alipokuwa akifungua kikao cha 13 cha Baraza la Wafanyakazi cha Wizara hiyo, ambacho hufanyika mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali za watumishi.

“Ni wajibu wa kila mtumishi kuzingatia maadili na weledi katika kuhakikisha utumishi wa umma unaheshimika na kuwajibika kwa wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa kazi zetu” amesema Dkt. Mwakyembe. Aidha Dkt. Mwakyembe ameziagiza mamlaka zinazosimamia nidhamu katika Wizara hiyo kutosita kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wasiotimiza wajibu wao ili kuimarisha utendaji wa kazi.

“Serikali ya awamu ya tano ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ipo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha taratibu za kiutendaji zinafuatwa na kuzingatiwa” amesema Dkt. Mwakyembe. Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Susan Mlawi alimshukuru mgeni rasmi kwa kuwafungulia kikao hicho ambacho kipo kwa mujibu wa sheria, na kuwasisitiza watumishi kuyafanyia kazi yale yote waliyoelezwa.

“Nawaomba watumishi kuzingatia na kutekeleza wajibu wenu katika majukumu yenu ya kila siku,kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizoainishwa katika mikataba ya ajira” amesema Bibi.Susan.

Naye Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi Bw.Makoye Alex Nkenyenge alimshukuru mgeni rasmi kwa niaba ya wajumbe wote na kuhaidi kuyafanyia kazi yale yote aliyoyaeleza katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. 

No comments: