Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Dkt. Jacqueline Shoo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya wagonjwa wawili; Suzana Athanas John (22) na Asha Atuman Kisabengo (28) kupandikizwa figo kila mmoja na kuruhusiwa kurejea nyumbani leo. Kutoka kushoto ni mtaalamu katika vyumba maalumu vya wagonjwa wa waliopandikizwa figo, Elizabeth Sephen, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Dkt. Onesmo Kisanga na Dkt. Muhidini.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma na Huduma kwa Wateja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha akitoa maelezo ya awali kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu upandikizaji figo kwa wagonjwa wanne. Upandikizaji huo ulianza tarehe 16-18 Aprili, 2018.
Asha Kisabengo (28) akiwashukuru madaktari na wataalamu wengine kwa mwezesha kurejea katika hali yake ya kawaida baada ya kupandikizwa figo katika hospitali hiyo.
Mtaalamu kwenye vyumba maalumu vya wagonjwa wa waliopandikizwa figo, Elizabeth Stephen akieleza jinsi walivyokuwa wakitoa huduma maalumu kwa ndugu waliotoa figo na kwa wagonjwa waliopandikizwa figo hadi kufanikiwa kuruhusiwa kurejea nyumbani leo.
Asha Kisabengo akilia kwa furaha baada ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kupandikiza figo na kurejea katika hali yake ya kawaida baada ya figo zake kushindwa kufanya kazi.
utoka kulia ni Suzana Athanas John (22) na Asha Atuman Kisabengo(28) wakiwa katika picha ya pamoja.
Wauguzi, ndugu waliotoa figo na waliopandikizwa figo wakiwa katika picha ya pamoja.
Dar es salaam, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeweka mipango ya muda mrefu na muda mfupi ili kuhakikisha huduma ya upandikizaji figo inakuwa endelevu, na imedhamiria kupandikiza figo kwa wagonjwa zaidi 200 kwa mwaka.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dare es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa MNH, Aminiel Aligaesha wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuruhusiwa wagonjwa wawili ambao wamepandikizwa figo Aprili mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Amesema katika mpango wa muda mfupi, kila mwezi hospitali hiyo itapandikiza figo wagonjwa watano, hivyo kwa mwaka itakuwa imefanikiwa kupandikiza figo wagonjwa 60.
“Mipango ya muda mrefu ni kuwa na sehemu maalum ya upandikizaji figo na hivi karibuni MNH itaanza ujenzi wa jengo jipya la ghorofa saba na katika jengo hilo tutatenga sehemu maalum ya upandikizaji figo , kila siku mgonjwa mmoja atapandikizwa figo, kwa wiki tutakuwa tumepandikiza figo wagonjwa watano, kwa mwezi wagonjwa 20 na kwa mwaka tutafanikiwa kupandikiza figo wagonjwa 240,’’ amesema Aminiel.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Magonjwa ya Figo Muhimbili , Dkt. Jacqueline Shoo amesema tukio hilo ni la kihisoria kwani mwaka jana hospitali ilifanikiwa kupandikiza figo mgonjwa mmoja na Aprili mwaka huu hospitali hiyo imepandikiza figo wagonjwa wanne kwa mfululizo.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH, Dkt. Onesmo Kisanga amesema takribani wagonjwa 800 nchini wanasubiri huduma ya upandikizaji figo na kati ya hao 50 tayari wameandaliwa.
Kwa upande wao wagonjwa waliopandikizwa figo na kuruhusiwa leo, Bi. Suzana John na Bi. Asha Athuman Kisebengo wameishukuru Hospitali ya Taifa Muhimbii pamoja na waaalam wake kwa kuwapatia matibabu ya ubingwa wa juu ambayo awali hayakuwepo nchini.
No comments:
Post a Comment