Wednesday, April 18, 2018

CCM DAR YASHAURI WALIOZIBA NJIA ZA MAJI WAONDOLEWE, YATOA POLE KWA WALIOPOTEZA NDUGU KWASABABU YA MVUA

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM), Mkoa wa Dar es Salaam kimetoa pole kwa familia ambazo zimepoteza ndugu zao kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha huku kikitoa ushauri kwa Serikali kuwaondoa waliojenga kwenye njia za maji kwa lengo la kupunguza maafa.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Cylivia Katekamba amewaambia leo waandishi wa habari kuwa chama hicho kinatoa pole kwa wote ambao wamefikwa na maafa na kuomba wenye uwezo wa kusaidia walioathrika na mvua hizo kujitokeza kusaidia.

" Mkoa wa Dar es Salaam umekumbwa na mafuriko na kusababisha baadhi ya wananchi kupoteza maisha.CCM mkoa tunatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki kutokana na kuondokewa na ndugu zetu kutokana na mvua.

"Tunafahamu matatizo ya mafuriko yametokea kwetu na hata maeneo mengine duniani nayo wakati mwingine hukumbwa na mafuriko.Kubwa ni kuendelea kushikamana na kusaidia kwenye kipindi hiki.CCM tunatoa pole,"amesema Katekamba.

Pia ametoa mwito kwa walio maeneo hatarishi ni vema wakaondoka maeneo hayo na kufafanua kutokana kuzibwa kwa mitaro na njia za maji imesababisha hata maeneo ambayo huwa hayapati mafuriko safari hii maji yamejaa.

Amefafanua yapo maeneo ambayo watu wamejenga lakini kiuhalisia ni maeneo ambayo yapo kwa ajili ya kupitisha maji na matokeo yake yanakosa pakupita na kwenda kwenye makazi ya watu na kusababisha maafa.

Ameshauri watu wa mipango miji kuangalia namna ya kuondoa changamoto hiyo na kuongeza kamati ya siasa ya Mkoa wa Dar es Salaam jana usiku imekutana kujadili hali ya mafuriko."Moja ya jambo tulilokubaliana maeneo ambayo yanatakiwa kubaki wazi ili maji yapite lazima mipango miji kuangalia namna ya kufanya,"amesema na kuongeza ni vema wananchi wa wakazingatia utunzaji wa mazingira kwa kutoziba njia za maji na kutokata miti ovyo.

Alipoulizwa kuhusu waliojenga kwenye njia za maji, Katekamba amejibu kuwa kazi ya Chama ni kuisimamia Serikali na hivyo moja ya jambo ambalo wanataka kuona linafanyika ni kuwaondoa waliojenga maeneo hayo.

Pia ameomba wananchi kuibua na kuwabainisha watu ambao wamejenga kwenye mifereji ya kupitisha maji badala ya kukaa kimya huku akielezea CCM Mkoa wa Dar es Salaam walikuwa na sherehe yao ya familia ya Wana-CCM Aprili 21 mwaka huu ambayo Mwenyekiti wake ni Idd Azan lakini wameiahirisha kutokana na mafuriko ya mvua na athari zilizotokea. 

Hata hivyo, Katekamba pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali ya mkoa wamefanya ziara ya kukagua mitaa iliyokumbwa na mafuriko na kuona hali halisi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Dar es Salaam Cylivia Katekamba(wa kwanza kushoto) akizungumza ma waandishi wa habari leo jijini wakati anatoa pole kwa waliokumbwa na mafuriko na familia ambazo zimepoteza wapendwa wao kwasababu ya mvua zinazonyesha.

No comments: