Wednesday, April 18, 2018

Wadau wa dawa na vifaa tiba nchini watakiwa kuchangamkia fursa

Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Mhe. Josephat Kandege amewataka wauzaji, waagizaji, wasambazaji na wadau wote wa dawa pamoja na Vifaa Tiba Nchini kuchangamkia fursa inayotolewa na Serikali ya kuwa Mshitiri mteule ‘Prime Vendor’ kusaidia katika utoaji wa dawa katika Mikoa yote Tanzania.

Kandege ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha Wadau wa dawa  ‘Vendors Forum’ kilichoandaliwa na Ofisi ya Rais Tamisemi kwa kushirikiana na wadau wa Afya ‘HPSS’ chenye lengo la kuweka uelewa wa pamoja kuhusu uanzishwaji na utekelezaji wa mfumo wa Mshitiri.

Amesema “mfumo huu utatumika kupata mahitaji ya bidhaa za Afya pale ambapo vituo vya kutolea huduma za Afya vya Umma vitakosa au kupata kiwango pungufu toka Bohari Kuu ya Dawa na pia utasaidia kupunguza kero za Afya ikiwemo uhaba wa upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya”.

Sasa basi ninyi kama wazabuni muhimu katika sekta hii ya Afya wenye Uzalendo na nia njema na Nchi ya Tanzania mnatakiwa kujitokeza katika mchakato wa kumpata Mshitiri (Prime Vendor) wa kila Mkoa ambaye atakidhi vigezo kwa mujibu wa taratibu manunuzi alisema Mhe. Kandege.

Wakati huo huo Naibu Waziri Kandege aliwafahamisha wadau wa dawa kuwa Serikali imagatua mipango na bajeti kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya na inapeleka Fedha moja kwa moja kwenye akaunti za benki zilizofunguliwa katika kila kituo hii itasaidia katika kufanya manunuzi ya dawa hizo na kurahisha mchakato wa malipo.

“Hivyo niwahakikishie kuwa utaratibu wa malipo utakua ni rahisi na wa haraka zaidi kwa kuwa Hospital, Vituo vya Afya na Zahanati husika zitahusika kuagiza dawa kwa Mshitiri pale mahitaji ya dawa hizo zitakapokosekana kutoka MSD” alisema Mhe. Kandege.

Alimalizia kwa kuwataka Wadau wote wa Dawa kutumia kikao hiki kuelewa kwa undani kuhusu utaratibu huu na kujitokeza kwa wingi katika mchakato wa kumpata Mshitiri Mteule kwani zoezi hili litaendeshwa kwa uwazi na kwa usindani mkubwa.

Mkurugenzi wa Afya Ofisi ya Rais Tamisemi Dr. Ntuli Kapologwe amesema hivi sasa wako katika uwekezaji Mkubwa katika Sekta ya Afya kwa kuzingatia kuwa Bajeti ya Dawa imeongezwa kutoka Bil 31 kwa mwaka 2015/16 hadi kufikia Bil 269 kwa mwaka 2017/18 hivyo ongezeko hili la bajeti linatakiwa kwenda sambamba na uhakika wa upatikanaji wa dawa na zenye ubora chini ya usimamizi makini wa wataalamu wa Afya.

Dr. Ntuli alisema mpango huu utaleta manufaa kwa wananchi wote ambao watakua chini ya mpango wa Tele kwa Tele na wale wanaopata huduma kupitia mfuko wa Bima ya Afya iliyoboreshwa; Tunataka kila mmoja apate dawa anayoihitaji kwa wakati.

Naye Mfamasia toka Ofisi ya Rais Tamisemi Regina Richard alisema mfumo wa Mshitiri Mteule umeanzishwa kwa sababu ya changamoto zilizoonekana awali za kutumia mzabuni kama vile taratibu za manunuzi kuchukua muda mrefu na gharama za manunuzi kuwa kubwa na zinazotofautiana kati ya Halmashauri moja na nyingine ndani ya Mkoa mmoja.

Changamoto zingine alizozibainisha ni kubadilika kwa bei mara kwa mara kila manunuzi yanapofanyika, kutokuwa na uhakika wa ubora wa bidhaa kutokana na kuhifadhiwa na kusafirishwa katika mazingira mbayo si salama na zaidi baadhi ya wazabuni na watumishi kutokuwa waaminifu.

Matumizi ya mfumo huu umeelekezwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Sera ya Afya ya Taifa ya mwaka 2007, Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya na Sera ya Mashirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi.
Kikao hiki cha wadau wa dawa ‘Vendor Forum’ kimefanyika kwa mara ya kwanza na kimehusisha wadau kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.
 Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Josephat Kandege(mbele) akifungua kikao cha wadau wa Afya ‘Vendor Forum’ kilichofanyika katika Ukumbi wa Dodoma Hotel.
  Mkurugenzi wa Afya Ofisi ya Rais Tamisemi Dr. Ntuli Kapologwe akitoa maelezo ya awali kabla hajamkaribisha mgeni rasmi kufungua kikao cha wadau wa Afya Vendor Forum.
 Mfamasia Mwandamizi  toka Ofisi ya Rais Tamisemi Regina Richard akielezea malengo la kikao cha Wadau wa Dawa ‘Vendor Forum’ kilichofanyika katika ukumbi wa Dodoma Hotel mapema leo.
  Wataalam toka Idara ya Afya Ofisi ya Rais-TAMISEMI pamoja na wadau wa Dawa wakiwa katika kikao maalum cha wadau wa dawa.


Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Josephat Kandege(mbele katikati) katika picha ya pamoja na baadhi ya wataalamu na wadau wa dawa.

No comments: