Tuesday, March 13, 2018

WAZIRI MIPANGO AWASILISHA MAPENDEKEZO YA SERIKALI YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA YA KIWANGO NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2018/2019


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango  (Mb)   akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019 Bungeni Dodoma.
IMG_9411
Baadhi ya Wabunge wakifuatilia kwa makini mawasilisho ya Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019 Bungeni Dodoma.
IMG_9467
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb)   akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019 ambapo miongoni mwa vipaumbele ni kujenga uchumi wa viwanda.
IMG_9578
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango  (Mb)  (katikati) akisikiliza jambo kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Mhe. Jitu Soni, nje ya Bunge baada ya mawasilisho ya Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019 Bungeni Dodoma.
IMG_8975
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akizungumza jambo na Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) baada ya kuwasilishwa kwa Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019 Bungeni Dodoma

IMG_9585
Mbunge wa Busega Dkt. Raphael Chegeni (kushoto) akimpongeza Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) baada ya kuwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/2019 Bungeni Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango
…………………
WIZARA YA FEDHA NA MPANGO

UTANGULIZI

  • Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai na afya. Aidha, tunamshukuru kwa kutuwezesha kukutana tena hapa mjini Dodoma, kupokea mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19, kwa mujibu wa Kanuni ya 97 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari 2016.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuteuliwa kwao kuwa wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kuanzia sasa. Aidha, niwapongeze Wenyeviti wote na Makamu wao ambao wamechaguliwa kushika dhamana ya kuziongoza Kamati hizo. Ni matumaini yangu  kuwa Waheshimiwa Wabunge katika nafasi zenu kwenye Kamati, bila kujali itikadi, mtaisaidia kuishauri Serikali ipasavyo katika kuijenga nchi yetu kwa manufaa ya Watanzania wote.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muhtasari, matokeo ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Tano ni pamoja na: nchi yetu kuendelea kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi ya wastani wa asilimia 7.0 kwa mwaka ambayo inatafsiri Pato la wastani la kila mtu kuwa shilingi 2,131,299 mwaka 2016 kutoka shilingi 1,918,930.9 mwaka 2015; kupungua kwa mfumuko wa bei kufikia asilimia 4.1 Februari 2018; kuongezeka kwa mapato ya ndani kufikia wastani wa shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi kutoka wastani wa shilingi bilioni 850; kuimarika kwa utoaji wa huduma za jamii hususan elimu msingi bila ada, kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma kwa ngazi zote ikiwemo huduma za matibabu ya kibingwa, kuimarika usambazaji wa maji mijini (kufikia wastani wa asilimia 78) na vijijini (wastani wa asilimi 55.5), umeme mijini na vijijini kufikia wastani wa uunganishaji wa asilimia 67.5 kitaifa na kuweka mazingira wezeshi kwa ujenzi wa viwanda ambapo viwanda vipya 3,306 vimejengwa.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/19 ni mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano, shughuli na miradi mingi iliyopangwa kutekelezwa ni ile ambayo haijakamilika na hivyo utekelezaji wake utaendelea katika mwaka ujao wa fedha. Aidha, maeneo mengine yaliyozingatiwa ni yale yatakayoongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango na kutoa majibu endelevu kwa kero na mahitaji ya msingi ya wananchi walio wengi.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/19 vimeweka mkazo katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini na kuimarisha uzalishaji, tija na uhakika wa masoko kwa sekta pana ya kilimo (ikijumuisha uzalishaji wa mazao, mifugo na bidhaa za mifugo, uvuvi na misitu) kuwezesha upatikanaji wa chakula na malighafi za kutosha kwa uzalishaji viwandani na ongezeko la idadi ya watu. 
  •  
  •  Msukumo pia umewekwa katika kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unakuwa jumuishi. Katika hili, msukumo umewekwa katika kuendeleza ujenzi wa miundombinu wezeshi katika sekta za uchukuzi, usafirishaji, nishati, kilimo na mawasiliano; na uboreshaji wa sekta ya huduma za fedha. Katika kulinda tunu kuu za Watanzania, yaani amani na umoja, msukumo umewekwa pia katika kuimarisha ulinzi na usalama, upatikanaji wa haki, utawala wa sheria na utawala bora na upatikanaji wa huduma za msingi kwa ustawi wa jamii.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla, utayarishaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2018/19 umezingatia: azma ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; sera na malengo ya kisekta; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015-2020; makubaliano ya kikanda (EAC na SADC); Ajenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika; na Ajenda ya Dunia ya Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030. Aidha, umezingatia mapitio ya hali ya uchumi kwa mwaka 2017 na mwelekeo kwa mwaka 2018 kitaifa, kikanda na Dunia na hali halisi ya utekelezaji wa Mpango wa mwaka 2017/18 hadi Februari, 2018.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii ina sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza inatoa tathmini ya mwenendo wa uchumi na ustawi wa Jamii; Sehemu ya pili inaelezea Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa ya mwaka 2018/19; na Sehemu ya tatu ni mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya 2017/18 na mapendekezo ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19.
SEHEMU YA KWANZA
TATHMINI YA MWENENDO WA UCHUMI NA USTAWI WA JAMII KWA MWAKA 2017
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Uchumi wa nchi yetu umeendelea kushamiri katika viashiria vingi. Katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba 2017, Uchumi ulikua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 6.8, kiwango ambacho kilikuwa cha juu zaidi ikilinganishwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki: Kenya (asilimia 6.1), Rwanda (asilimia 6.0), Uganda (asilimia 5.5), Burundi (asilimia 0.0) na Sudani Kusini (asilimia hasi 6.3). Kwa kulinganisha na nchi zote za bara la Afrika, kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania ulikuwa wa tatu baada ya Ethiopia (asilimia 8.2) na Ivory Coast (asilimia 7.6).
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi kikubwa, ukuaji huu ulichangiwa na ongezeko la shughuli za: Uchimbaji Madini na Mawe (asilimia 20.3); Habari na Mawasiliano (asilimia 13.1); Usafirishaji na Hifadhi ya Mizigo (asilimia 11.9); Uzalishaji Viwandani (asilimia 9.8); na Ujenzi (asilimia 9.5). Ukuaji wa sekta ya kilimo ulikuwa asilimia 3.3 katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2017 ikilinganishwa na asilimia 2.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta ya kilimo kwa maisha na uchumi wa wananchi wengi, Serikali kupitia mpango huu, itaendelea kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, upatikanaji wa pembejeo za kilimo, huduma za ugani, na maghala ya kuhifadhi mazao na upatikanaji wa masoko. Msukumo pia umewekwa katika kufungamanisha sekta ya kilimo na sekta ya viwanda kwa lengo la kuongeza thamani na faida ya shughuli za kilimo.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwaka 2017, mwenendo wa mfumuko wa bei ulikuwa tulivu kutokana na kuimarika kwa upatikanaji wa chakula nchini, utulivu wa bei za nishati hasa mafuta katika soko la ndani na nje ya nchi na usimamizi thabiti wa sera za fedha na za bajeti. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2017 mfumuko wa bei ulikuwa wastani wa asilimia 5.3 na umeendelea kupungua na kufikia asilimia 4.1 mwezi Februari, 2018.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Akiba ya fedha za kigeni katika kipindi kinachoishia Desemba 2017, ilifikia Dola za Marekani milioni 5,906.2 ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 4,325.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Kiasi hicho kilichofikiwa mwezi Desemba 2017 kilikuwa kinatosheleza kugharamia ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 6.0 na hivyo kuzidi kiwango cha angalau miezi 4.5 kilichowekwa kukidhi matakwa ya hatua za mtangamano wa Umoja wa Fedha kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka ulioishia Desemba 2017, mwenendo wa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani uliendelea kuwa wa kuridhisha. Katika kipindi cha mwezi Desemba 2017, Dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,230.1 ikilinganishwa na wastani wa shilingi 2,172.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2016, ikiwa ni tofauti ya wastani wa shilingi 57.4. Mwenendo huu ulitokana na kuboreshwa kwa usimamizi, pamoja na utekelezaji wa sera thabiti za bajeti na fedha (prudent fiscal and monetary policies) sanjari na mwenendo mzuri wa urari wa mapato ya fedha za kigeni.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka unaoishia Desemba 2017, wastani wa riba za amana uliongezeka kufikia asilimia 9.6 kutoka wastani wa asilimia 8.8 Desemba 2016. Viwango vya riba za amana za mwaka mmoja vilipungua kutoka asilimia 11.0 Desemba 2016 hadi asilimia 10.9 Desemba 2017. Hata hivyo, viwango vya riba za mikopo ya hadi mwaka mmoja viliongezeka kufikia asilimia 18.2 Desemba 2017 kutoka wastani wa asilimia 12.9 Desemba 2016. Hii ilitokana na mabenki kuchukua tahadhari kubwa kwa wateja wanaoshindwa kurejesha mikopo. Hata hivyo, riba katika soko la fedha baina ya mabenki ilipungua na kufikia wastani wa asilimia  3.3 Desemba 2017 kutoka asilimia 13.5 Desemba 2016. Riba kwenye dhamana za Serikali ilipungua kutoka asilimia 15.1 Desemba 2016 hadi asilimia 8.2 Desemba 2017.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuongeza ukwasi katika uchumi na ukuaji wa mikopo yenye gharama nafuu kwa sekta binafsi. Hatua hizo ni pamoja na: kupunguza kiwango cha chini cha sehemu ya amana za benki za biashara kinachotakiwa kuhifadhiwa Benki Kuu (SMR)kutoka asilimia 10 hadi 8 mwezi April 2017; Kupunguza kiwango cha riba cha benki za biashara kukopa Benki Kuu kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12 na kwa mara nyingine hadi asilimia 9 mwezi Agosti 2017, lengo lilikuwa kuyawezesha mabenki kukopa na kukopesha kwa riba nafuu; mabenki na taasisi za fedha kutakiwa kutumia taarifa zitolewazo na mfumo wa upatikanaji wa taarifa za wakopaji (credit refence system) kufanya maamuzi sahihi katika ukopeshaji; na  hivi karibuni Benki Kuu imeelekeza mabenki ya biashara kufanya marekebisho ya muda wa marejesho ya mikopo na kuanzisha kitengo cha ufuatiliaji wa madeni. Kufuatia hatua hizo zilizochukuliwa na Serikali za kuimarisha sekta ya fedha, mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi umeanza kuongezeka kutoka kiwango cha ukuaji hasi wa asilimia 1.5 mwezi Oktoba 2017 hadi ukuaji chanya wa asilimia 2.0 mwezi Januari 2018. Aidha, mikopo chechefu imeanza kupungua kutoka asilimia 12.5 ya mikopo kwa sekta binafsi mwezi Septemba  2017 hadi kuwa asilimia 11.2 mwezi Desemba 2017.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Desemba 2017, deni la Serikali lilifikia dola za Marekani milioni 21,308.7 sawa na shilingi bilioni 47,756.3 ikilinganishwa na dola za Marekani 19,957 milioni Juni, 2016. Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni dola milioni 15,237.0, sawa na shilingi bilioni 34,148.6, ikiwa ni asilimia 71.5 ya deni lote. Deni la ndani lilikuwa shilingi bilioni 13,607.7 sawa na asilimia 28.5 ya deni lote. Ongezeko la deni kwa kipindi cha Juni 2016 hadi Desemba, 2017 lilitokana na mikpo mipya na mabadiliko ya kiwango cha ubadilishaji fedha (exchange rate fluctuations). Tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika mwezi Novemba 2017 kwa kipindi kilichoishia Juni, 2017 inaonesha kuwa deni ni himilivu kwa kipindi cha muda wa kati na muda mrefu. Uwiano wa deni la ndani na nje kwa Pato la Taifa kwa mwaka 2017/18 ni asilimia 34.4 ikinganishwa na ukomo wa asilimia 56, hivyo deni bado lipo chini ya kiwango cha hatari. Aidha, uwiano wa deni la nje na mauzo ya nje ni asilimia 81.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150. Hii inamaanisha kuwa uwezo wetu wa kulipa deni bado ni imara.
SEHEMU YA PILI
MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA YA MWAKA 2018/19
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2017/18
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Januari 2018 ni kama ifuatavyo:
  1. Mradi wa kuzalisha umeme wa maji Rufiji (Rufiji Hydropower Project): shilingi bilioni 3.2 zimetumika kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa mradi. Mchakato wa kumpata mkandarasi wa ujenzi unaendelea na ujenzi wa njia ya usafirishaji umeme wa msongo wa kV 33 kutoka Dakawa hadi eneo la mradi (km 53) ambapo km 8.5 zimesimikwa nguzo za miti, na kukamilika kwa matayarisho ya km 36 zitakazosimikwa nguzo za zege;
  2. Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge: Kwa ujumla utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 8 na unatarajiwa kufikia asilimia 15 ifikapo Juni 2018. Kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro, shilingi bilioni 4.04 zimetolewa kwa kazi ya usanifu wa mradi na tathmini ya muundo wa ardhi (soil structure). Aidha, ili kulipa fidia uthaminishaji wa mali zitakazoathiriwa na ujenzi wa mradi unaendelea. Mkandarasi wa ujenzi amelipwa shilingi bilioni 415.14 ambapo ujenzi wa kambi za Dar es Salaam umekamilika kwa asilimia 99, Soga asilimia 89 na Ngerengere asilimia 67 na uinuaji wa tuta la reli umefikia asilimia 15. Kwa kipande cha Morogoro – Makutupora tayari mkandarasi wa ujenzi amepatikana na kulipwa malipo ya awali ya shilingi bilioni 492.6;
  3. Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: shilingi bilioni 7.85 zimetolewa kutekeleza mkataba wa ununuzi wa ndege, ambapo ndege mbili za aina ya Bombadier CS 300 zimelipiwa kwa asilimia 30 na ndege moja kubwa ya masafa marefu, Boeing 787, kwa asilimia 52;
  4. Ujenzi wa barabara za kuunganisha makao makuu ya mikoa na zile zinazounganisha Tanzania na nchi jirani: barabara za Dodoma – Babati (sehemu ya Mayamaya – Mela – Bonga km 188.15), Sumbawanga-Kanazi (km 75.0), Kanazi-Kizi-Kibaoni (km 76.6), Kyaka-Bugene (km 59.1), Kaliua – Kazilambwa (km 58.9), Magore – Turiani (km 48.8), Uyovu – Bwanga (km 45) zimekamilika kwa kiwango cha lami na ujenzi wa madaraja ya Kilombero na Kavuu umekamilika. Vile vile, ujenzi wa barabara ya juu ya TAZARA umefikia asilimia 70 na ile ya Ubungo Interchange imeanza kujengwa;
  5. Ujenzi wa jengo la abiria pamoja na miundombinu yake katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Julius Nyerere umefikia asilimia 68;
  6. Ujenzi wa ukuta katika machimbo ya Tanzanite – Mererani umekamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 5.42;
  7. Shamba la Miwa na Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi: hekta 300 tayari zimepandwa miwa na ujenzi wa boma la kiwanda cha sukari umekamilika, kuwezesha hatua za kuagiza mitambo;
  8. Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi Tanga-Tanzania: upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya kupakulia mafuta umekamilika na wananchi wa Chongoleani – Tanga watakaopisha ujenzi wa bomba wamelipwa fidia;
  9. Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili – kampasi ya Mloganzila kimezinduliwa rasmi na Mhe. Dkt. John P. Magufuli, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Novemba, 2017 na shilingi bilioni 4 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi unaoendelea wa mabweni na majengo mengine ya kufundishia;
  10. Shilingi bilioni 80 fedha za ndani zimetumika kununua na kusambaza dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa vituo vya kutolea huduma nchi nzima; na
  11. Shilingi bilioni 3 fedha za ndani na milioni 800 fedha za nje zimetumika kununua chanjo za kudhibiti magonjwa mbalimbali; kulipa mchango wa Serikali katika Shirika la GAVI kwa ajili ya chanjo; na kutolewa kwa mafunzo ya namna ya kukabiliana na saratani ya kizazi.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafanikio mengine yaliyopa-tikana ni pamoja na: (i) Kuendelea kugharamia elimumsingi bila ada; (ii) Kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika shule 180 za msingi na 110 za sekondari; (iii) Kukamilika kwa ukarabati wa vituo vya afya 204 na miundombinu yake nchi nzima. Vile vile, kupitia Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Korea (KOICA) ukarabati wa zahanati 28, vituo vya afya 21, hospitali ya wilaya 1 na ya mkoa 1 umekamilishwa; (iv) Ununuzi wa mitambo na vifaa vya kufundishia na kujifunzia vya uhandisi umeme katika vyuo vya ufundi stadi vya Mtwara, Morogoro, Njombe na Dodoma unaendelea; (v) Kukamilika kwa visima 19 katika maeneo ya Kimbiji na Mpera, Dar es Salaam; (vi) Kukamilika kwa mradi wa kupeleka maji katika miji ya Mwadui, Kishapu, Kolandoto na Maganzo ambapo wakazi 58,155 wamenufaika; na kuendelea na ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege, kiungio na maegesho ya ndege katika kiwanja kipya cha ndege cha Geita.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa viwanda vipya vilivyojengwa katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Tano ni zaidi ya 3,600. Kwa upande wa sekta binafsi, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi na kuzinduliwa kwa viwanda vifuatavyo: (i) Saruji: Kilimanjaro Cement na upanuzi wa viwanda vya Tanga Cement na Mbeya Cement ambapo vimeongeza uzalishaji kufikia tani milioni 11.28 na kutoa ajira 8000; (ii) Marumaru: Goodwill Ceramic Ltd cha Mkuranga kilichozalisha ajira 4,500; (iii) Chuma: Kilua Steel-Mlandizi chenye uwezo wa kuzalisha tani 500,000 kwa mwaka na ajira 800; (iv) Kusindika Matunda: Elven Agri Co. Ltd chenye uwezo wa kukausha matunda tani 2,500, kusindika nyanya tani 1,000 kwa mwaka na ajira 300; na (v) Kiwanda cha Sigara cha Phillip Morris – Morogoro na Kiwanda cha kuzalisha Mita za Umeme (LUKU) cha INHEMETER – Dar es Salaam. Aidha, kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti cha Mount Meru – Singida, Kahama Oil Mills, viwanda vya plastiki, chuma, mabati na mabomba vilivyopo Kahama vimezinduliwa na vinafanya kazi.  
Vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2018/19
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango unaowasilishwa ni watatu katika hatua za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17-2020/21 wenye dhima ya “Kujenga Uchumi wa Viwanda ili kuchochea Mageuzi ya Uchumi na Maendeleo ya Watu”. Hivyo, vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2018/19 vitazingatia maeneo mbalimbali ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Aidha, sehemu kubwa ya miradi itakayotekelezwa katika maeneo hayo ya vipaumbele ni ile inayoendelea kama ifuatavyo:
  • Miradi ya Kielelezo na Itakayopewa Msukumo wa Kipekee
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Miradi itakayotekelezwa ni pamoja na: kituo cha kuzalisha umeme wa maji katika Mto Rufiji (MW 2100); ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge, hususan, vipande vya Dar es Salaam hadi Morogoro (km 300) na Morogoro hadi Makutupora (km 336); kuboresha Shirika la Ndege Tanzania; ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Tanga; uzalishaji wa makaa ya mawe na umeme – Mchuchuma na chuma – Liganga; uendelezaji wa shamba la miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari Mkulazi; Kituo cha Biashara na Huduma Kurasini; uendelezaji wa kanda maalum za kiuchumi hususan, Bagamoyo na Kigamboni; uanzishwaji wa kiwanda cha kusindika gesi asilia kuwa kimiminika – Lindi na kuongeza idadi ya wataalam katika fani adimu.
  • Miradi Mingine ya Kukuza Uchumi wa Viwanda
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Miradi ya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda inalenga kuendelea kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini, hususan za kilimo, madini na gesi asilia. Katika eneo hili, miradi itakayopewa kipaumbele ni pamoja na: kuimarisha shughuli za Shirika la Viwanda Vidogo – SIDO; Kiwanda cha Ngozi na Bidhaa za Ngozi-Karanga; Mradi wa Magadi Soda – Bonde la Engaruka; Kituo cha zana za Kilimo na Ufundi Vijijini-CARMATEC; na viwanda vya Nyumbu na Mzinga.
  • Miradi ya Kufungamanisha Maendeleo ya Viwanda na Maendeleo ya Watu
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili linalenga kuendeleza mafanikio ya upatikanaji wa huduma msingi kwa ustawi wa maisha ya Watanzania. Miradi katika eneo hili ni pamoja na: ujenzi na ukarabati wa maktaba za mikoa; ujenzi na uboreshaji wa maabara katika shule na taasisi; kuendeleza ujenzi na kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji, kupanua huduma za elimu ya afya na usafi wa mazingira shuleni, mijini na vijijini; kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma kwa ngazi zote ikiwemo zahanati, vituo vya afya, hospitali za mikoa, kanda na kitaifa, huduma za matibabu ya kibingwa, kupunguza vifo vya akina mama wajawazito, kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, sambamba na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya; kukamilisha ujenzi na ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi vya wilaya na mikoa; utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu; na kuimarisha programu ya kukuza ujuzi.
  • Miradi ya Ujenzi wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili Serikali imejielekeza katika kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu, ikijumuisha miundombinu ya nishati, usafirishaji (reli, barabara, madaraja, viwanja vya ndege na bandari) na ununuzi na ukarabati wa meli na vivuko. Baadhi ya miradi iliyozingatiwa katika eneo hili ni: kuendelea na ukarabati wa reli ya kati na TAZARA ikiwemo ununuzi wa injini na mabehewa; kuendelea na ujenzi wa barabara zinazounganisha makao makuu ya mikoa, zinazounganisha masoko ya kikanda na barabara za kupunguza msongamano mijini; na miradi ya kuzalisha na kusambaza umeme. Aidha, ujenzi wa mazingira wezeshi utahusu pia uimarishaji wa ulinzi na usalama, upatikanaji wa haki, utawala wa sheria na utawala bora.
  • Kuimarisha Usimamizi na Utekelezaji wa Mpango
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na: kuimarisha mifumo ya kitaasisi kwa lengo la kuimarisha ufuatiliaji na tathmini kwa kuzingatia Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma; kujenga uwezo wa wataalam katika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi ya maendeleo; na kuimarisha mifumo ya uhifadhi na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi kulingana na thamani ya fedha (value for money).
  • Mikakati ya Kuchochea Ukuaji wa Sekta za Kilimo
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kuchochea ukuaji wa sekta za kilimo itaendelea: kuboresha miundombinu ya umwagiliaji; kuongeza upatikanaji wa zana na pembejeo za kilimo; kuongeza huduma za ugani; kuboresha upatikanaji wa miundombinu ya hifadhi ya mazao na masoko; na kutatua vikwazo mbalimbali vinavyosababisha viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi zitokanazo na kilimo kushindwa kushindana na bidhaa husika kutoka nje.
Mikakati ya Kuchochea Ushiriki wa Sekta Binafsi
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango unasisitiza ujenzi wa mazingira yatakayochochea na kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Pamoja na hatua za kuondoa vikwazo katika uwekezaji na ufanyaji biashara, Mpango umezingatia utekelezaji wa mapendekezo ya marekebisho ya sheria, kanuni na taratibu kwa miradi ya ubia (PPP) na kuhakikisha upatikanaji rahisi wa maeneo ya uwekezaji. Hatua nyingine zitakazochukuliwa ni pamoja na: kuandaa Sera ya Maendeleo ya Sekta Binafsi; kuimarisha mfumo rekebu na miundo – taasisi; kuimarisha mfumo wa majadiliano kati ya Serikali na sekta binafsi; kuweka vivutio na sera za kibajeti kuwezesha sekta binafsi kuwekeza katika maeneo ya kipaumbele na kushindana katika soko la ndani na kimataifa; na kusimamia ubora wa bidhaa na kuhamasisha wananchi kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/19, Serikali inategemea kufanya upembuzi yakinifu kuainisha uwezekano wa kutekeleza miradi ifuatayo kwa utaratibu wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP): miradi ya bandari ya Mwambani, reli ya Mtwara-Mchuchuma/Liganga kwa kiwango cha standard gauge, reli ya Tanga-Arusha-Musoma kwa kiwango cha standard gauge, ujenzi wa miundombinu ya reli na uendeshaji wa treni ya abiria katika jiji la DSM, usambazaji wa gesi asilia nchini na mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) awamu ya II hadi IV.
SEHEMU YA TATU
MFUMO NA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2018/19
Mwenendo wa Mapato na Matumizi Hadi Februari 2018
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika mwaka 2017/18, Serikali ilipanga kukusanya na kutumia jumla ya shilingi bilioni 31,712.0. Hadi kufikia mwezi Januari 2018, jumla ya mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia shilingi bilioni 17,401.9 sawa na asilimia 85.0 ya lengo la kipindi hicho, ambapo:
  1. Mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 10,036.3 sawa na asilimia 88.3 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 11,360.8;
  2. Mapato yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 1,456.1 sawa na asilimia 98.2 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 1,483.4;
  3. Mapato yaliyokusanywa na Halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 345.9 sawa na asilimia 74.1 ya makadirio ya shilingi bilioni 466.9;
  4. Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilifikia shilingi bilioni 1,408.5, sawa na asilimia 66 ya lengo la shilingi bilioni 2,145.1;
  5. Mikopo ya ndani ilifikia shilingi bilioni 3,931.0 ikiwa ni asilimia 95.6 ya kiasi kilichopangwa kukopwa, ikijumuisha shilingi bilioni 3,246.0 zilizokopwa kulipia amana za Serikali zilizoiva (rollover) na mikopo mipya ya shilingi bilioni 685.0; na
  6. Mikopo ya nje ya kibiashara ilifikia shilingi bilioni 224.1.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika kipindi hicho, Serikali iliweza kutoa mgao wa shilingi bilioni 17,401.9 kwa mafungu mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti, sawa na asilimia 85.0 ya makadirio ya bajeti hadi Januari 2018. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 13,349.9 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 4,052.0 kwa matumizi ya maendeleo, zikijumuisha shilingi bilioni 3,447.3 za ndani na shilingi bilioni 604.5 za nje.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mgao wa bajeti ni pamoja na: kulipa deni la Serikali na mishahara ya watumishi wa umma; kugharamia ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege; kulipia malimbikizo ya madai ya wazabuni, wakandarasi na watumishi wa umma; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya uzalishaji na usambazaji wa umeme na kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; kugharamia elimu-msingi bila ada; utekelezaji wa miradi ya maji; na kununua dawa na vifaa tiba.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/18 katika kipindi cha Julai 2017 hadi Februari 2018 ni pamoja na:
  1. Kuimarisha na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ambapo jumla ya shilingi bilioni 59.0 zimetolewa kwa Halmashauri za Wilaya 110 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya, shilingi bilioni 24.1 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali za mikoa 24. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 125.7 zimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi;
  2. Katika kutekeleza lengo la kuwapatia wananchi mijini na vijijini huduma ya maji safi na salama kiasi cha shilingi bilioni 149.3 kimetolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji;
  3. Katika jitihada za kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme ili kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma hii muhimu, kiasi cha shilingi bilioni 300.9 kimetolewa kwa ajili miradi ya nishati vijijini, umeme wa jotoardhi, uzalishaji wa umeme katika vyanzo mbalimbali na usambazaji wa gesi asilia;
  4. Katika kutekeleza azma ya kutoa elimu msingi bila ada na kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Serikali imetoa shilingi bilioni 543.5;
  5. Serikali imeendelea kutekeleza ujenzi wa miundombinu ili kupanua fursa za uchumi, kilimo, biashara na viwanda ikiwemo barabara zinazounganisha mikoa na nchi jirani, barabara zinazopunguza msongamano katika majiji, barabara za vijijini, reli, viwanja vya ndege, na bandari. Katika eneo hili kiasi cha shilingi bilioni 1,451.5 kimetolewa;
  6. Serikali imeendelea kulipa malimbikizo ya madai ya watumishi umma, wazabuni, wakandarasi na watoa huduma ambapo kiasi cha shilingi bilioni 939.5 kimelipwa; na
  7. Serikali imeendelea kusimamia matumizi bora ya fedha za umma kwa kufanya ufuatiliaji na uhakiki wa madai mbalimbali ikijumuisha uhakiki wa madai ya fidia kwa wananchi wanaopisha miradi ya maendeleo na malimbikizo ya madai ya  watumishi wa umma. Kati ya madai yaliyowasilishwa ya shilingi bilioni 312.6, shilingi bilioni 156.8 zilikubaliwa baada ya kukidhi vigezo na hivyo Serikali imeokoa shilingi bilioni 155.8.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya mafanikio yaliyopatikana kulikuwa na changamoto za utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2017/18, hususan kutokana na kutofikiwa kwa malengo ya makusanyo ya mapato kulikosababishwa na:
  1. Mwamko mdogo wa kulipa kodi na hususan kuzingatia matumizi ya mashine za kielektroniki;
  2. Masharti magumu ya upatikanaji wa mikopo ya kibiashara kutoka nje; na
  3. Mabadiliko ya sera za misaada katika nchi zilizokuwa zikitupatia misaada ya kibajeti.
Aidha, utekelezaji wa Mpango na Bajeti uliathiriwa pia na uwepo wa malimbikizo ya madai; ugumu wa upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji; matayarisho hafifu ya miradi; na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yalisababisha uharibifu wa miundombinu ya usafiri kutokana na mvua kubwa katika baadhi ya maeneo.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na:
  1. Kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu na faida za kulipa kodi kwa kutumia mitandao ya kielektroniki. Aidha, Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala za Serikali zilihimizwa kutumia mabenki katika kukusanya maduhuli;
  2. Kuwezesha mifumo ya kodi kutambua malipo kwa kutumia huduma za simu za mkononi kukusanyia kodi mbalimbali. Kwa kufanya  hivyo itatoa fursa kwa walipa kodi kulipa kodi kwa urahisi na kuwezesha kodi nyingi kukusanywa;
  3. Kuanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Stempu za Kodi (Electronic Tax Stamps) kwenye viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa na zile zinazoingizwa nchini. Mfumo huu utasaidia kupata taarifa kamili za uzalishaji viwandani pale tu kiwanda kinapofanya uzalishaji na kupunguza uvujaji wa mapato ya Serikali;
  4. Kuboresha na kuimarisha mfumo wa kielektroniki wa kutolea risiti za kodi (EFDMS) ili kuwezesha ufuatiliaji wa karibu wa mauzo na utoaji wa risiti kwa kila manunuzi badala ya kutumia risiti za makundi (batch). Hii itasaidia kupata taarifa za uhakika za walipa kodi zitakazotumika katika kukokotoa kodi kwa usahihi na kuweza kutoa makadirio stahiki ya kodi;
  5. Kutekeleza mradi wa dirisha moja la Forodha (Tanzania Electronic Single Window System) ili kuwaweka pamoja wadau wote wa kuondosha mizigo bandarini na mipakani. Lengo ni kusogeza huduma karibu na waagizaji bidhaa na hivyo kuongeza kasi ya uingizaji bidhaa nchini (Turn around);
  6. Kutekeleza Mwongozo wa Ushirikiano baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo (Development Cooperation Framework – DCF) ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa fedha kutokana na ahadi zao;
  7. Kuendelea kusisitiza nidhamu katika utekelezaji wa bajeti kama ilivyoidhinishwa na Bunge kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015;
  8. Kuendelea kuwianisha mapato na matumizi kwa kuhakikisha kuwa mgao wa fedha unaendana na upatikanaji wa mapato na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima;
  9. Kuzuia ongezeko la malimbikizo mapya ya madai na kulipa madai yaliyohakikiwa ikiwa ni pamoja na kusaidia kuongeza ukwasi na kuchochea shughuli za kiuchumi; na
  10. Kuanza utekelezaji wa mkakati wa kufanya maboresho ya mazingira ya biashara nchini (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment).
Sera za Mapato na Matumizi  kwa Mwaka 2018/19
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera za mapato kwa mwaka 2018/19 kwa ujumla wake zitalenga kuongeza mapato ya ndani kwa kurahisisha ulipaji wa kodi kwa kutumia mifumo ya kielektroniki; kuendelea na zoezi la kurasimisha sekta isiyo rasmi ikiwa ni pamoja na kupima na kutoa hati miliki za makazi/viwanja, mashamba  na kuthaminisha majengo; kuimarisha mazingira ya kuvutia uwekezaji na biashara ili kufikia azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda, hii ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama, utawala wa sheria na utawala bora; kutekeleza mkakati wa kufanya maboresho ya mazingira ya biashara nchini; na kusimamia mfumo wa Serikali wa ukusanyaji wa maduhuli kwa njia ya kieletroniki (GePG). Aidha, kwa upande wa misaada na mikopo nafuu, Serikali itaendelea kuimarisha mahusiano na Washirika wa Maendeleo kwa kutumia Mwongozo wa Ushirikiano baina ya Serikali na Washirika wa Maendeleo. Uboreshaji huu unatarajiwa kuongeza uwekezaji, uzalishaji, ajira na miamala ya biashara na hivyo kupanua wigo wa mapato.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/19, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015. Lengo kuu ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma, kudhibiti malimbikizo ya madai mapya na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi ya kielelezo. Serikali itachukua hatua mbalimbali ili kutimiza azma hii kama ifuatavyo:
  1. Kuwianisha matumizi na mapato halisi yatakayopatikana kwa kila mwezi;
  2. Kuhakikisha kuwa ununuzi wa umma unazingatia thamani ya fedha;
  3. Kusimamia kikamilifu na kuzuia matumizi na miadi ya matumizi nje ya mfumo wa “IFMS”;
  4. Kuendelea kufanya uhakiki wa madai mbalimbali na kulipa madai yaliyohakikiwa;
  5. Kuimarisha maandalizi na uchambuzi wa miradi; na
  6. Kuimarisha ufuatiliaji wa matumizi ya Serikali ili kupata thamani ya fedha.
Kiwango na Ukomo wa Bajeti kwa Mwaka 2018/19
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia shabaha, na sera za bajeti kwa mwaka 2018/19, Sura ya Bajeti inaonesha kuwa jumla ya Shilingi bilioni 32,476.0 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho. Mfumo na ukomo wa bajeti ya mwaka 2018/19 umezingatia hali halisi ya upatikanaji wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri yanatarajiwa kuwa Shilingi bilioni 20,894.6 sawa na asilimia 64 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Shilingi bilioni 18,000.2 sawa na asilimia 13.6 ya Pato la Taifa. Mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia shilingi bilioni 2,158.8 na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri ni Shilingi bilioni 735.6.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, vyanzo vingine vya mapato ni pamoja na misaada na mikopo yenye masharti nafuu ya Shilingi bilioni 2,676.6 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo, ikiwa ni asilimia 8 ya bajeti yote. Serikali pia inatarajia kukopa Shilingi bilioni 5,793.7 kutoka soko la ndani, ambapo shilingi  bilioni 4,600.0 kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na Shilingi bilioni 1,193.7 ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Kiasi cha Shilingi bilioni 1,193.7 ambazo ni mikopo mipya ni sawa na asilimia 0.9 ya Pato la Taifa. Ili kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi muhimu ya miundombinu, Serikali inatarajia kukopa shilingi bilioni 3,111.1 kutoka soko la nje.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa matumizi, katika mwaka 2018/19 Serikali inapanga kutumia jumla ya Shilingi bilioni 32,476.0. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 20,468.7 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya bajeti. Matumizi ya kawaida yanajumuisha Shilingi bilioni 10,004.5 kulipia deni la Serikali, shilingi bilioni 7,369.7 mishahara, shilingi bilioni 3,094.5 matumizi mengineyo (OC) na shilingi bilioni 389.9 matumizi yatokanayo na vyanzo vya ndani vya Halmashauri.
Kwa upande wa matumizi ya maendeleo, Serikali itatumia shilingi bilioni 12,007.3 sawa na asilimia 37 ya bajeti. Kiasi hiki kinajumuisha Shilingi bilioni 9,876.4 sawa na asilimia 82.3 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 2,130.9 sawa na asilimia 17.7 ni fedha za nje. Hata hivyo, kiasi hiki hakihusishi uwekezaji wa moja kwa moja wa sekta binafsi, mashirika ya Umma na ubia kati ya sekta ya umma na binafsi. Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kuwezesha mashirika ya Umma na sekta binafsi kutekeleza miradi ya maendeleo.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo, kiwango na ukomo wa bajeti kwa mwaka 2018/19 ni kama inavyooneshwa katika Jedwali Na. 1.
Jedwali Na. 1: Mfumo wa Bajeti ya Mwaka 2018/19
Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango
HITIMISHO
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/19 vinalenga hasa katika kuendelea kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya  Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha ustawi wa jamii. Aidha, Serikali itaendelea kujizatiti katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuendelea kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi.
  • Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa matumizi, serikali itaendelea kuweka mkazo katika usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma ili zitumike zaidi kugharamia miradi ya kipaumbele na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

  • Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

No comments: