Tuesday, March 13, 2018

MAKAMU WA RAIS AZUNGUMZA NA BALOZI WA UFARANSA NA MKURUGENZI MKAZI WFP





Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amekutana na kuzungumza na Balozi mpya wa Ufaransa nchini Mhe. Frederic Clavier ambaye aliongozana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) Bw. Emmanuel Baudran.

Katika mazungumzo hayo ambayo yamefanyika Ofisini kwa Makamu wa Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Balozi Clavier amewasilisha salaam za Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na kusema “Rais wa Ufaransa ana uhakika na Tanzania ijayo na anaunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na Rais Magufuli”

Balozi huyo mpya wa Ufaransa nchini ambaye amekutana na kuzungumza na Mheshimiwa Makamu wa Rais aliipongeza Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika masuala mbali mbali ya Kimataifa na kusema “Tanzania ni nchi yenye utulivu na Amani kitu ambacho kinaipa taswira nzuri Umoja wa Mataifa”.

Mhe. Balozi amemjulisha Makamu wa Rais kwamba Ufaransa imekusudia kuimarisha uhusiano zaidi na Tanzania wa Uchumi na Siasa na kuanzisha majadiliano mbali mbali katika masuala ya Mazingira,Mabadiliko ya Tabia Nchi.

Balozi Clavier amemjulisha Makamu wa Rais kuwa mwezi ujao kutakuwa na ugeni wa wafanya biashara kati ya 30 au 40 kutoka nchi ya Ufaransa ambao watakuja kujionea fursa mbali mbali za kibiashara na uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania.

Mhe. Balozi amemuelezea Makamu wa Rais azma ya Ufaransa kushirikiana na Vyuo Vikuu vya Tanzania katika kuanzisha na kuendesha kozi mbali mbali kwa manufaa ya pande zote mbili.Mwisho aliipongeza Serikali kwa mapambano dhidi ya rushwa na urasimu jambo litakalo wavutia wawekezaji wengi nchini.

Aidha, Bw. Emmanuel Baudran Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa alisema Shirika lao linakusudia kuanzisha kiwanda cha vifaa vya umeme wa jua (solar) mkoani Shinyanga pia shirika hilo limeshafanya miradi ya uboreshaji maji taka katika manispaa ya Temeke na wanaendelea na mikakati ya uanzishwaji wa miradi mingine.Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alimshukuru na kumpongeza Balozi wa Ufaransa kwa kazi nzuri wanazofanya hapa nchini.

Alimhakikishia kwamba Serikali ya Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano kwa mambo yote muhimu yenye maslahi kwa wananchi.Wakati huohuo Makamu wa Rais alikutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Mhe. Michael Danford.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Frédéric CLAVIER aliyemtembelea Makamu wa Rais ofisini kwake ,Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Frédéric CLAVIER ofisini kwa Makamu wa Rais Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimia na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani(WFP) hapa nchini Bw. Michael Dunford ambaye alifika ofisni kwa Makamu wa Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani(WFP) hapa nchini Bw. Michael Dunford ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais

No comments: