Tuesday, March 13, 2018

WANANCHI WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO MRADI WA UMEME VIJIJINI AWAMU YA TATU GEITA

Mkuu wa mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi Akizungumza na wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi wa REA baada ya kufika kwenye ofisi yake . 
Baadhi ya wajumbe wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Geita, 
Mwenyekiti wa REA Gedion Kaunda akimashukuru Mkuu wa Mkoa baada ya kutembelea miradi ya usambazaji wa umeme vijijini kwenye Wilaya za Bukombe pamoja na Chato. 
Meneja wa TANESCO Mkoani Geita Joachim Ruweta ,Akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi ya REA awamu ya Tatu kwenye baadhi ya maeneo. 
Wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi wa REA wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Geita,Mhandisi Robert Luhumbi.


Na, Joel Maduka,Geita

Mkoa wa Geita unatarajia kunufaika na mradi kabambe wa usambazaji umeme vijijini REA awamu ya Tatu kwa kuongeza shughuli za kiuchumi kwa wananchi kutokana na vitongoji 220, vijiji 372 na Kata 499 ambazo zinatarajia kunuifaika na Nishati ya Umeme.

Akizungumza mbele ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi REA meneja wa TANESCO Mkoani Geita Joachim Ruweta amesema Mradi huo kwa mzunguko wa kwanza utaunganisha wateja wapatao 12,944 na hivyo kukamilika kwa Mradi huo utafanya umeme kuongezeka kwa Asilimia 51 kwa wateja waliopo sasa.

“Mategemeo yetu ni kwamba mzunguko wa pili ambao unatarajia kuanza mwaka 2019 na kumalizika mwaka 2020 na 2021 utafanya vijiji vyote vya Mkoa wa Geita kupata umeme kwa asilimia mia moja” Alisema Ruweta.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Luhumbi amewataka wananchi kutoa ushirikiano na kujua kuwa hakuna fidia ambazo watalipwa kutokana na mradi huo.

“Wito kwa wananchi wa Mkoa wetu wa Geita watoe ushirikiano Katika vijiji vyote ambako wataalamu wetu watapitia wajue kuwa hakuna fidia kwasababu mradi huu utakuja kwaajili ya kutupatia maendeleo na unapowasha umeme itasaidia kukua kwa uchumi wa eneo husika na Mkoa wetu” Alisema Luhumbi. 

Aidha kwa upande wake Mwenyekiti wa REA Gedion Kaunda alisema hadi sasa hivi bado hawajaona tatizo lolote ambalo lipo kwenye mradi huo na kwamba wanaamini watafanikisha kwenye maeneo yote ambayo mradio huo umepangwa kufanyika.

Mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza Mkoani Geita unatekelezwa na mkandarasi aitwaye White city Guangdong JV ambaye ni ubia wa Kampuni ya Kitanzania na Kampuni ya nje na unatarajia kugharimu zaidi ya Shilingi za kitanzania Bilioni 61 na fedha za Kimarekani Dola milioni 7.8.

No comments: