Mhandisi Mkuu kutoka Shirika la Reli (TRL), Mhandisi Nelson Ntejo akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia) kuhusu maendeleo ya kazi ya ukarabati wa eneo lililoathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha mwanzoni mwa mwaka, katika eneo la Kilosa mkoani Morogoro, wakati Waziri huyo alipokagua reli hiyo Mkoani humo, hivi karibuni.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mkuu kutoka Shirika la Reli (TRL), Mhandisi Nelson Ntejo, alipokagua ukarabati wa njia ya reli ya kati ya eneo la Kilosa mkoani Morogoro iliyoharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha mwanzoni mwa mwaka huu. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akikagua kazi zinazoendelea katika eneo la Kilosa, ambapo ukarabati umekamilika na treni za mizigo zimeanza kupita.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akishiriki katika kazi za kujaza mchanga kwenye viroba vinavyotumika kama kingo za kudhibiti maji ya mto Mkondoa yasifike kwenye miundombinu ya reli katika eneo la kilosa, mkoani Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Stephen Kebwe, akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Reli (TRL), na wakazi wa Kilosa, wakati alipokagua ukarabati wa njia ya reli ya kati eneo la Kilosa karibu na mto Mkondoa, mkoani humo.
Muonekano wa sehemu ya njia ya reli ya kati eneo la Kilosa iliyokarabatiwa baada ya kuharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha, mkoani Morogoro mwanzoni mwa mwaka huu.
Muonekano wa treni ya mizigo ikianza safari zake katika stesheni ya Kilosa, mkoani Morogoro kuelekea mkoani Mwanza mara baada ya njia hiyo kukarabatiwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Stephen Kebwe na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Bw. Adamu Mgoyi, alipokutana nao katika ukaguzi wa ukarabati wa njia ya reli ya kati kutoka eneo la Kilosa.
…………………………………………………………………………………
Shirika la Reli Tanzania (TRL) limepata hasara ya takribani shilingi bilioni tano katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya njia ya reli ya kati kusombwa na mafuriko katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro na Gulwe mkoani Dodoma.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya reli hiyo na kusema kuwa Serikali imejipanga kupata suluhisho la kudumu la uharibifu katika maeneo hayo ambapo mara kadhaa yamekuwa yakiathiriwa na mvua kutokana na mabwawa yaliyopo kujaa mchanga na hivyo kusababisha uharibifu huo.
“Serikali kwa sasa inayafanyia kazi mapendekezo matatu yaliyowasilishwa na RAHCO ikiwemo kuihamisha reli kwenye milima jirani, kuihamishia eneo ambapo inajengwa reli ya kisasa ya SGR ama kujenga tuta kubwa, huku tukizingatia gharama halisi za kazi hiyo kabla ya kufanya maamuzi”, amesema Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa mbali na Serikali kuja na suluhu ya muda mfupi ya kurejesha safari za treni pia amewatoa hofu wafanya biashara kwa kuwahakikishia kuwa mizigo yao iko salama na itasafirishwa kwa wakati.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Steven Kebwe, amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Mkoa umejipanga kuhakikisha unatoa elimu kwa wananchi kwenye utunzaji wa mazingira ili kunusuru uharibifu unaotokea kutokana na shughuli za kibinadamu.
“Kama Mkoa tumejipanga kuwa kuanzia sasa Sheria zilizopo zinazokataza kulima kandokando ya mito na kando ya reli sasa zitafuatwa na tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili miudombinu hiyo isiathirike kwa sababu ya shughuli za kibinadamu zinazofanywa kupitia kilimo”, amesisitiza Dkt. Steven Kebwe.
Ameongeza kuwa kuanzia mwakani mkoa umejipanga kutenga fedha kwa ajili ya kutumia njia za asili kulinda miundombinu hiyo kwa kupanda miti na kuotesha matete ili kulinda miundombinu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Massanja Kadogosa, amesema kazi ya ukarabati imekamilika kwa sehemu kubwa kwani tayari treni tano za mizigo zimepita salama na kuongeza kuwa kazi zinazomaliziwa kwa sasa ni kujaza mchanga kwenye matuta ya reli hiyo na kumalizia kingo ili kuilinda reli.
No comments:
Post a Comment