Wednesday, February 7, 2018

TANZANIA KINARA UTAWALA BORA AFRIKA MASHARIKI

Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa ahadi mbalimbali za Serikali mapema hii leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi (kulia) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa ahadi mbalimbali za Serikali mapema hii leo jijini Dar es Salaam.Picha na Eliphace Marwa – MaelezoNa. Immaculate Makilika- MAELEZO

Orodha ya Hali ya Demokrasia Duniani (2017 Democracy Index) iliyozinduliwa Februari 2, mwaka huu na kuchapishwa na jarida kongwe na mashuhuri duniani la The Economist imeitaja Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika maswala ya Utawala Bora kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi alisema kuwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwenye masuala ya Utawala bora imeweza kusaidia ukuaji wa Uchumi wake.

“Utawala Bora ni kigezo muhimu cha ukuaji wa uchumi na hata ustawi wa jamii, kama ambavyo Orodha ya Hali ya Demokrasia Duniani iliyotolewa na jarida kongwe na mashuhuri duniani la The Economist imeitaja Tanzania ni ya kwanza katika ukanda wa EAC, ikifuatiwa na nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC. 

Pia, ripoti ya Foresight Afrika na taarifa ya Uchumi ya Benki ya Dunia vyote vimeitaja Tanzania kuwa katika nchi tano Bora za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi katika mwaka 2018, nchi hizo ni Ghana, Ethiopia, Kodivaa , Senegali na Tanzania”.

Aidha, Dkt. Abbasi alisema kuwa ukuaji huo wa uchumi ni dhamira isiyoyumba ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uchumi mkuu unaendelea kujiakisi katika maisha ya watanzania kupitia utoaji wa huduma kwa wananchi na kuboresha sekta mbalimbali.

Katika sekta ya Afya, Dkt. Abbasi alisema kuwa pamoja na ujenzi wa vituo vya afya unaoendelea nchi nzima na uboreshaji wa hospitali, Serikali imetenga bajeti ya dawa na vifaa tiba kutoka Bilioni 31 mwaka 2015 hadi Bilioni 269. Aidha, bajeti ya sasa imewezesha Serikali kuboresha usambazaji wa dawa hadi kufikia asilimia 86 ya uhakika wa kupatikana dawa muhimu.

Bajeti hiyo imewezesha ukarabati wa wodi 5 za ICU na kuongezwa vitanda kutoka 21 mpaka 75, kununua mashine mpya za CT-Scan yenye uwezo mkubwa imenunuliwa katika hospitali ya Muhimbili na Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya fahamu (MOI) zenye uwezo mkubwa ambapo wastani wa wagonjwa wanaopimwa imepanda kutoka 20 hadi 50 kwa siku.

Vifaa vingine vilivyonunuliwa ni pamoja na mashine 14 za upasuaji (diathermy machines) na mashine za kuchuja damu kwa ajili ya wagonjwa wa figo zipatazo 25 na kuongeza uwezo wa kuhudumia wagonjwa kutoka 68 kwa siku hadi 126. 

Uboreshaji huo wa sekta ya afya umeifanya Muhimbili kuwa hospitali ya kwanza ya umma katika ukanda wa Afrika Mashariki kutoa huduma za juu za kibingwa hasa oparesheni ya kuweka vifaa vya kusaidia kusikia ambapo watoto 5 waliokuwa awali hawasikii kabisa walifanyiwa oparesheni mwaka jana na kusikia kwa mara ya kwanza katika maisha yao. Wengine 6 wamefanyiwa wiki iliyopita. 

Katika sekta ya Sekta, Msemaji huyo wa Serikali alisema kuwa lengo la Serikali ni kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 85 vijijini ifikapo mwaka 2020 kutoka asilimia 67.7 mwaka 2015, makao makuu ya mikoa asilimia 95, Dar es Salaam asilimia 95 na miji mikuu ya wilaya asilimia 90 ifikapo 2020. 

Ambapo hadi sasa kwa ujumla kuna takribani miradi 1,423 imekamilika na kuna vituo vya maji 117,190 vyenye uwezo wa kuhudumia watu milioni 29 sawa na asilimia 79. Katika miaka hii miwili pekee zaidi ya miradi 388 ilikamilishwa.

Dkt. Abbasi, anafafanua kuwa katika usambazaji wa umeme mijini na vijijini kazi imeendelea kwa kasi kubwa. Katika kutekeleza Mradi wa REA III, kiasi cha shilingi bilioni 985.9 zitatumika kuwafikishia wananchi umeme katika programu maalum iliyoanza kutekelezwa.

Alisititiza kuwa, “Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, imedhamiria kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi si tu kwa maneno bali kwa vitendo, mfano namna ambavyo Serikali imeongeza wigo wa barabara vijijini na mijini, pamoja na kuundwa kwa wakala maalum (TARURA) ambao utajikita zaidi katika kuharakisha ujenzi wa barabara za vijijini”

Aliongeza kuwa mwaka huu Serikali inakusudia kutekeleza upanuzi wa njia za mwendokasi jijini Dar es Salaam kwenda njia za barabara ya Kilwa kwenda Mbagala yenye urefu wa kilomita 19 na barabara ya Uhuru kwenda Gongolamboto yenye urefu wa kilomita 23.9.

Aidha, Dkt Abbasi amewakumbusha watanzania kuwa wazalendo, kuunga mkono jitihada za Serikali kufanya kazi kwa bidii, kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano inasisitiza wananchi kufanyakazi ili kuijenga Tanzania uitakayo.

No comments: