Wednesday, February 7, 2018

ZAIDI YA BILIONI 2.1 KUKARABATI BIHAWANA NA DODOMA SEKONDARI

 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Graceana Shirima (wa pili kushoto) akikagua shughuli ya ukarabati katika Shule ya Sekondari ya Dodoma baada ya kuzindua rasmi kazi hiyo. TEA imetoa zaidi ya Shilingi milioni 900 kwa ajili ya ukarabati huo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi na kulia ni Mhandisi Lupakisyo Mwalwiba ambaye ni Meneja Miradi kutoka Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST)  ambaye ndiyo Mtaalamu Mshauri. 
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TEA Graceana Shirima (kushoto) akikagua maeneo mbalimbali yanayofanyiwa ukarabati katika Shule ya Sekondari ya Bihawana iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma jana mara baada ya kufanya uzinduzi rasmi wa kazi hiyo. TEA imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 1.2 kwa ajili ya kuikarabati Shule hiyo.
 Ukarabati ukiendelea katika Shule ya Sekondari ya Dodoma

Na Ramadhani Juma, Ofisi ya Mkurugenzi 
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 2.1 kwa ajili ya kukarabati Shule za Sekondari za Bihawana na Dodoma zilizopo Manispaa ya Dodoma ikiwa ni sehemu ya utekezaji wa mpango wa Serikali wa kuzifanyia ukarabati mkubwa Shule kongwe Nchini.

Kati ya Fedha hizo, zaidi ya Shilingi Bilioni 1.2 zitatumika kukarabati Shule ya Sekondari ya Bihawana pekee na zaidi ya Shilingi Milioni 900 zitatumika katika Shule ya Sekondari ya Dodoma.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kazi ya ukarabati katika shule hizo jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TEA Graceana Shirima alisema kuwa, shughuli ya ukarabati ilitanguliwa na upembuzi yakinifu wa hali halisi ya mahitaji ya ukarabati uliofanywa na mtaalamu mshauri ambaye ni Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

“Baada ya upembuzi yakinifu, maeneo ya kipaumbele katika ukarabati kwa awamu hii itahusisha Madarasa, maabara, bwalo na jiko,  vyoo, na mifumo ya umeme, mifumo ya TEHAMA na mifumo na maji safi na maji taka” alisema Shirima.

Alisema  awamu hii ya ukarabati inatarajiwa  kukamilika ndani ya kipindi cha  miezi minne, na awamu nyingine za ukarabati zitatekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi aliishukuru Mamlaka ya Elimu kwa kuzipatia Shule za Manispaa hiyo Fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati huku akitolea mfano wa Shule ya Wasichana ya Msalato ambayo ilishafanyiwa ukarabati mkubwa mwaka uliopita.

Kunambi aliahidi kuwa, Manispaa ya Dodoma  ambaye ndiye mmiliki wa Shule hizo itasimamia kwa karibu kila hatua ya kazi hiyo.

Baadhi ya Wanafunzi wa Shule zinazofanyiwa ukarabati wamepongeza hatua ya Serikali ya kutekeleza mpango huo na kwamba itawaboresha mazingira ya kujifunzia ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa miundombinu muhimu kama umeme, maji, na mabweni.



Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza Mpango kabambe wa ukarabati wa Shule kongwe 89 za Sekondari Nchini ambao unafanyika kwa awamu.

No comments: