Tuesday, February 6, 2018

RC NDIKILO AIAGIZA CBT KUMLIPA MALIPO MKANDARASI GHALA LA KUHIFADHIA KOROSHO MKURANGA

MKUU wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo,(kulia)akielekeza jambo baada ya kuonyeshwa ramani ya ghala la korosho ambapo linatarajia kujengwa huko Mkuranga, wakati alipokwenda kutembelea ujenzi wa ghala hilo .(Picha na Mwamvua Mwinyi) Na Mwamvua Mwinyi,Mkuranga

MKUU wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ameiagiza bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kuhakikisha inamlipa ,malipo ya awali kiasi cha sh.bilioni 1.6, mkandarasi wa ghala la kuhifadhia korosho wilayani Mkuranga.

Alitoa agizo hilo ,wilayani Mkuranga alipotembelea ujenzi wa ghala hilo linalojengwa na kampuni ya BQ Contractors Ltd .Alieleza kabla ya ujenzi waliingia mkataba wa kulipa asilimia 30 ya malipo ya awali ya ujenzi wa ghala hilo la kisasa ambalo litagharimu kiasi cha shilingi bilioni 5.5 hadi kukamilika kwake.

Aidha Ndikilo alisema, kampuni hiyo ilitoa malalamiko kuwa zimepita siku 52 wakiwa hawajapewa hata shilingi moja kwa ajili ya ujenzi huo hali ambayo inasababisha ujenzi huo kuwa mashakani kukamilika kwa wakati.

“CBT ihakikishe inatoa fedha hizo ndani ya wiki hii, bodi ya korosho ambao ndiyo wamiliki wa ghala hilo na endapo watashindwa kufanya hivyo atawapeleka kwa Waziri Mkuu kwa ajili ya hatua zaidi";

"Mkurugenzi wa bodi hiyo itabidi wakutane Dodoma kwa ajili ya kueleza ni sababu gani inawafanya washindwe kumlipa mkandarasi huyo,” alisema Ndikilo.Alisema serikali kwa kushirikiana na bodi ya korosho walikubaliana kujenga ghala hilo ili kuwe na ghala moja kwa kila wilaya tatu za Mkuranga, Kibaha na Rufiji ambako ndiko zinalimwa korosho nyingi.

Ndikilo alieleza lengo la kuwa na ghala la uhakika ni kufanikisha mfumo wa stakabadhi ghalani.“Kuanzia msimu ujao korosho zote zitauzwa kwenye ghala moja kubwa badala ya kutumia maghala ya watu binafsi ama ya vyama vya msingi vya ushirika ambao wanaonekana kufanya hujuma kwa kuweka korosho ambazo hazina viwango ,:;ambapo kwa msimu huu tatizo lilikuwa kubwa sana,” alifafanua Ndikilo.

Hata hivyo ,alieleza kutotolewa fedha hizo kutasababisha ujenzi huo kutokamilika kwa wakati kutokana na hali ya mvua za masika unaokuja ambazo zitasababisha ujenzi huo kushindwa kufanyika katika kipindi lengwa.Nae mwakilishi wa bodi ya korosho Japhari Matata alikiri kucheleweshwa kwa fedha hizo .Alisema kwasasa taratibu za kuzipata fedha hizo zinaendelea ili kumpatia mkandarasi huyo.

Matata alisema atalifikisha suala hilo kwa wahusika kwa ajili ya kuhakikisha linafanikiwa ili ujenzi huo ukamilike mwezi wa nane kipindi ambacho ndicho ilipangwa ukamilike.Awali akitoa taarifa kuhusu ujenzi huo, meneja wa maendeleo ya biashara wa kampuni hiyo Hilu Bura, alisema changamoto kubwa ni ukosefu wa fedha kwa ajili ya ujenzi huo ambao ulianza Oktoba mwaka jana.

Alitaja changamoto nyingine ni eneo hilo kuwa na maji kwa wingi hivyo endapo fedha zitachelewa kutasababisha kujenga kipindi cha mvua za masika ambacho kinakaribia kuanza.Bura alimuomba mkuu wa mkoa huyo wa Pwani kuwasaidia ili waweze kupatiwa fedha za awali.

No comments: