Monday, February 26, 2018

DK. KIGWANGALLA ATOA MIEZI TISA KWA WANANCHI KULIPWA FIDIA WAPISHE HIFADHI YA TAIFA TARANGIRE NA PORI LA AKIBA MKUNGUNERO


Na Hamza Temba-WMU-Manyara
........................................................................

Serikali italipa fidia na vifuta jasho kwa vitongoji ambavyo vipo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Pori la Akiba Mkungunero ili viweze kupisha maeneo hayo yaendelee kuhifadhiwa kwa mujibu wa sheria.

Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Kimotorok katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara ambao ulihudhuriwa pia na Wakuu wa Wilaya za Simanjiro, Kiteto na Kondoa.

Alisema fidia hiyo italipwa kwa vitongoji viwili vya kijiji cha Irkishbo vya Maasasi na Lumbenek  vilivyopo katika Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara ambavyo vilikutwa ndani ya Pori la Akiba Mkungunero wakati pori hilo linaanzishwa mwaka 1996 kwa Tangazo la Serikali Na. 307.

"Tutafanya tathmini, tutawaomba wananchi mshirikiane na Serikali ili muweze kulipwa fidia mpelekwe maeneo mengine, jukumu letu sisi ni kugharamia zoezi la tathmini na kulipwa fidia ili muweze kuondoka katika maeneo haya ya hifadhi," alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema kwa upande wa baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kimotorok ambao wameanzisha makazi kimakosa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Pori la Akiba Mkungunero hawatalipwa fidia na badala yake watafanyiwa tathmini na kulipwa kifuta jasho na kupelekwa maeneo mengine.

"Kimsingi ukimkuta mtu yupo katika eneo lako hupaswi kulipa fidia, hapa tumekuwa waungwana na kutumia roho ya kibinadamu, vinginevyo tungeweza kusema leo hapa tusione mtu na tungevunja kwa sababu ni eneo halali la hifadhi na hairuhusiwi kwa mujibu wa sheria mtu kuishi ndani ya hifadhi.

"Kwa sasa hatutatumia nguvu, lakini tukikamilisha zoezi la tathmini tukalipa watu fidia yao, tutatoa muda maalum wa watu kuondoka na watu watapaswa kuondoka, ilimradi tutajiridhisha kwamba tulimtendea haki kila mwananchi anayeishi katika eneo hili," alisema Dk. Kigwangalla.

Akizungumzia moja ya zahanati iliyojengwa ndani ya kitongoji hicho cha Kimotorok ambayo nayo itabomolewa baada ya zoezi la kulipa vifuta jasho, aliiagiza TANAPA kujenga zahanati nyingine katika eneo jipya litakalopangwa Halmashauri husika kwa ajili ya wananchi hao kuhamia.

Alisema zoezi la tathmini pamoja na wananchi kulipwa fidia na vifuta jasho linatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi tisa ijayo kuanzia mwezi Machi, 2018. 

Akizungumzia hatma ya makazi mapya kwa wananchi watakaondolewa kwenye maeneo hayo ya hifadhi, Dk. Kigwangalla ameziagiza Halmashauri husika za Kiteto, Kondoa na Simanjiro kupanga maeneo mengine mbadala ya kuwahamishia wananchi hao punde baada ya kulipwa fidia zao.

Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa linalosimamia Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori inayosimamia Pori la Akiba Mkungunero kusaidia jamii jirani na maeneo hayo ya hifadhi kwa kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi, kuendeleza eneo la malisho na kuchimba mabwawa ya maji ya kunywesha mifugo ili kujenga misingi ya urafiki na ujirani mwema.

Katika hatua nyingine, Dk. Kigwangalla amefuta mipaka ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Makame ambayo imeingia kimakosa ndani ya Pori la Akiba Mkungunero na kumuagiza Meneja wa Pori hilo, Emmanuel Bilaso kuweka ulinzi mkali katika eneo hilo.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula alisema watasimamia utekelezaji wa maagizo hayo ya Serikali ili kuhakikisha mgogoro huo wa muda mrefu unapatiwa ufumbuzi. 

Katika ziara hiyo ya siku moja Mkoani Manyara, Waziri Kigwangalla alitembelea na kukagua eneo la Ranchi ya Manyara ambayo pia ni sehemu ya mapito ya wanyamapori,  eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge, Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Pori la Akiba Mkungunero ambapo alitoa maelekezo mbalimbali ya kuboresha maeneo hayo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Herman Batiho kukakua maeneo hifadhi hiyo jana wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani Manyara. 

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akionyeshwa mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na viongozi wa hifadhi hiyo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani Manyara jana.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiongozwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Herman Batiho kukakua maeneo ya mapito ya wanayamapori na mipaka ya hifadhi hiyo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi mkoani Manyara jana. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisalimiana Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Sezaria Makuta wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua changamoto za uhifadhi katika Kijiji cha Kimotorok mkoani Manyara jana. Wanaoshuhudia kushoto Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magesa.

No comments: