*Polisi yaendelea kuchunguza kifo cha Akwilina,waua majambazi Dar
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema linamshikilia mwanamke mmoja na mwanaume mmoja kwa tuhuma za kuhusishwa na mauaji ya kada wa Chadema Daniel John aliyekutwa amekufa maeneo ya Coco Beach jijini.
Akizungumza leo, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema kutokana na uchunguzi unaendelea kuhusu mauaji hayo huko maeneo ya Hananasifu Kinondoni wamefanikiwa kuwakamata watu wawili.
Amesema majina ya watu hao yamehifadhiwa kwa lengo la kutoharibu uchunguzi unaoendelea kuhusu tukio hilo la mauaji ya kada huyo wa Chadema.
UCHUNGUZI KIFO CHA AKWILINA WAENDELEA
Wakati huohuo, Kamanda Mambosasa amesema bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Usafirishaji Akwilina Akwiline aliyefariki dunia baada ya kupigwa risasi.
Mambosasa amesema bado wanaendelea kuchunguza tukio hilo ambalo limegusa hisia za watu wengi na baada ya kukamilisha uchunguzi wao watatoa taarifa kwa umma ili ujue.
WAKAMATA SILAHA TANO, RISASI 35
Pia Mambosasa amesema Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa takriban wiki mbili sasa wamekuwa wakifanya operesheni ya kukamata wahalifu wanaojihusisha na matukio ya ujambazi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali jijini.
Amesema maeneo ya Pugu alikamatwa mtu mmoja aitwaye Peter Kwema a.k.a Babu na alipohojiwa alikiri kujihusisha na matukio ya ujambazi katika mikoa ya Dar es Salaam,Morogoro,Arusha,Tanga na Kilimanjaro.Pia ametaja baadhi ya wenzake ambao amekuwa akishirikiana nao.
"Baada ya kumhoji alikubali kwenda kutuonesha ambako wenzake wapo lakini baadae aliamua kupiga kelele kuwashutua kwa lengo la polisi washambuliwe ili yeye atoroke.
"Majambazi hao walianza kurushia risasi askari na ndipo yakaanza majibizano na hatimaye Polisi kufanikiwa kuua majambazi wawili.Pia tumekamata silaha mbili ambazo ni SMG moja iliyokuwa na risasi saba na bastola mbili aina ya Saurus mmoja iliyokuwa na risasi tatu,"amesema Mambosasa.
Amesema jambazi Kweka yeye alipigwa risasi ambazo zilimjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake wakati akijaribu kutoroka chini ya ulinzi wa Polisi na hatimaye akafariki dunia.
Pia Februari 16 mwaka huu,Polisi walipata taarifa za kiitelejensia huko maeneo ya Chanika kuna kundi la wahalifu limepanga kufanya tukio la unyang'anyi wa kutumia silaha. Jeshi la Polisi lilianza ufuatiliaji.
Amesema saa tano usiku wakiwa njiani kuelekea maeneo ya Chanika Homboza kuelekea eneo la kufuatilia wahalifu hao walikutana na kundi la watu sita na waliposimamishwa walikaidi amri na kuanza kufyatua risasi kwa askari.
Amesema askari walijibu mashambulizi na hatimaye kuwazidi nguvu na kusababisha majeraha kwa majambazi huku wengine wakikimbia.
Majambazi hao walipopekuliwa mmoja alikutwa na SMG iliyofutwa namba ikiwa na risasi 28 ndani ya magazini na mwingine akiwa na Bastola aina ya Browning yenye namba Tz Car 103143 ikiwa na risasi 9 ndani ya magazini.
No comments:
Post a Comment