Tuesday, January 23, 2018

MGALU ARIDHISHWA NA KASI YA MKANDARASI SENGEREMA

Na Mwamvua Mwinyi-Bagamoyo

NAIBU Waziri Wa Nishati Subira Mgalu, ameridhishwa na kasi na kazi anayoendelea nayo ,mkandarasi wa mradi wa umeme vijijini (REA) awamu ya III, Sengerema huko kijiji cha Kongo na kata ya Yombo wilaya ya Bagamoyo ,Mkoani Pwani.

Aidha amelitaka shirika la umeme (Tanesco) wilaya ya Bagamoyo, kukimbizana na wakati kwa kuwapa wananchi fomu za kujaza ili kupatiwa umeme wakati zoezi la kuweka nguzo likiendelea katika baadhi ya vijiji.

Aliyasema hayo wakati alipokwenda kutembelea kijiji cha Kongo ,kata ya Yombo na Visezi kata ya Vigwaza na kujiridhisha na kazi ya mradi huo inavyoendelea .Mgalu alisema mkandarasi huyo ameahidi kumaliza kazi hiyo mwanzoni mwa mwezi ujao na kwa uhakika anakwenda vizuri.

Alieleza kwasasa amekuta wanaendelea na kazi ya kusimamisha nguzo na maeneo mengine yanatarajiwa kutandaza nyaya ."Mkandarasi Sengerema yupo Mkoa wa Iringa na Pwani ,ameanza kazi vizuri na ndivyo tunavyohitaji ,tunaomba aendelee na kasi hii ili wananchi wapate huduma hii ya umeme haraka" alisisitiza Mgalu.

Naibu waziri huyo,alitoa tahadhali kwa wakandarasi wengine wa mradi wa REA kwenda na kasi inayotakiwa na serikali ya awamu ya tano,na atakaefanya kazi chini ya kiwango hatakuwa na masihala nae.

Pamoja na hayo ,alilitaka Shirika la Umeme (TANESCO) mkoani Pwani,kwenda kuhakiki nguzo 120 zilizotelekezwa chini miaka mitatu mfululizo,.kwenye vijiji hivyo ,ili kujua kama bado zinauwezo wa kutumiwa

Mgalu alisema, nguzo 60 zilizopo kijiji cha Visezi na nguzo nyingine 60 kijiji cha Kongo ,zilipelekwa na mkandarasi MBH kwa maelekezo ya umeme vijijini (REA)awamu ya II ,ambae alifanya uzembe .

Alieleza ,Tanesco ihakikishe inahakiki nguzo hizo bila kufanya ajizi kwani serikali ilishamlipa fedha mkandarasi huyo awamu iliyopita ,hivyo itakuwa ni hasara kubwa kuziacha nguzo hizo pasipo kuzifanyia kazi .Mgalu alisema mkandarasi huyo ,hatoshi na amechelewesha huduma ya umeme kwa wananchi na atachukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wakandarasi wababaishaji na wazembe.

”Ninaomba zikaangaliwe kama zinawezekana kufanyiwa kazi ,zitumike katika maeneo ambayo zitafaa kupelekwa ,kuliko kuendelea kukaa chini na kusababisha maswali ’alisema.

Mgalu aliwaeleza wakazi wa Visezi kuwa kijiji hicho kinatarajia kupata umeme kupitia mradi wa umeme unaotekelezwa katika mkoa wa Pwani na baadhi ya maeneo jijini Dar es salaam ikiwemo Kigamboni (PERI-URBAN).

Nae mbunge wa jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete ,alisema anaimani na wizara ya nishati na nia nzuri ya serikali kwa kupeleka umeme katika vitongoji vyote na hakuna kitongoji kitakachoachwa.

Alisema ,kijiji cha Visezi kimezungukwa na fursa za chama cha ushirika cha umwagiliaji,gesi,ukaribu wa bandari kavu ya Kwala ,hivyo kinapaswa kupatiwa huduma ya umeme ili kunufaika na kuinua uchumi wake.

Ridhiwani ,alieleza ni wajibu wa wakandrasi na Tanesco kufanya kazi inayotarajiwa na jamii ili kuwaletea maendeleo wanayoyategemea .Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kongo,waliipongeza serikali kwa kuwasogezea huduma ya umeme karibu na wanaamini maendeleo yataongezeka.

 Naibu Waziri Wa Nishati ,Subira Mgalu mwenye kitambaa chekundu kichwani ,akiwa ameambatana na mbunge wa jimbo la Bagamoyo.dk.Shukuru Kawambwa wa pili kushoto na wengine ni viongozi mbalimbali wa kijiji cha Kongo na kata ya Yombo wakati alipokwenda kutembelea maeneo yanayotekelezwa mradi wa umeme vijijini (REA )awamu ya III ,ambapo amejiridhisha na kasi anayoendelea nayo mkandarasi Sengerema.(picha na Mwamvua Mwinyi)
 Nguzo 60 za umeme zilizotelekezwa ndani ya miaka mitatu huko kijiji cha Visezi Kata ya Vigwaza pasipo kufanyiwa kazi ,jambo linaloelezwa ni uzembe uliofanywa na mkandarasi MBH aliyepewa kazi awamu ya pili ya mradi wa umeme vijijini (REA )ambapo ameitia hasara serikali na kuchelewesha huduma ya umeme kwa jamii(picha na Mwamvua Mwinyi)
Naibu Waziri Wa Nishati ,Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Visezi kata ya Vigwaza kuhusiana na masuala ya huduma ya umeme.
 Mbunge wa jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete akizungumza jambo kuhusiana na changamoto ya nishati ya umeme huko kijiji cha Visezi kata ya Vigwaza. 

No comments: