Tuesday, January 23, 2018

OLE NASHA AAGIZA CHUO CHA UFUNDI ARUSHA KUFUNGWA VIFAA VYA KISASA NDANI YA WIKI NNE






Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,William Ole Nasha akitoa hotuba yake wakati wa mahafali ya tisa ya Chuo cha Ufundi Arusha(ATC) 
Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,William Ole Nasha(wa pili kuli) akiwapongeza wanafunzi wahitimu waliofanya vizuri zaidi katika kozi walizosomea 
Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,William Ole Nasha(katikati),Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha(ATC),Dk Masudi Senzia(wa pili kulia),Makamu Mkuu wa Chuo,Utawala,Fedha na Mipango,Dk Erick Mgaya pamoja na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wasichana. 


Arusha.Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,William Ole Nasha ameuagiza uongozi wa Chuo cha Ufundi Arusha(ATC) uwe umefunga vifaa vya kisasa vyenye thamani ya Sh 14 bilioni ndani ya wiki nne badala ya siku 67 ili vianze kutumika mara moja.

Ametoa agizo hilo kwenye mahafali ya tisa ya wahitimu 465 wa fani mbalimbali za ufundi jijini hapa kuwa ukarabati na upanuzi wa karakana ufanyike ndani ya muda alioutoa ili vifaa hivyo vitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

"Nilipotembelea Chuo hiki Desemba 2,mwaka jana nilitoa maagizo mharakishe ujenzi na ukarabati wa miundombinu itakayotumika kufunga vifaa hivyo kutoka Austria,nafarijika kusikia kuwa utaanza mara moja kwani Wizara ilishatoa kibali cha kutumia watalaam wenu wa ndani na fedha mnayo,"alisema Ole Nasha

Alisema sekta ya elimu ya ufundi kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2015 inatarajiwa kuleta maendeleo ya haraka ya rasilimali watu walioelimika na kupenda kujielimisha zaidi ili kulifanya taifa lipate maendeleo.Ole Nasha aliongeza kuwa elimu ya ufundi ina mchango mkubwa katika kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda na nchi zilizoendelea kama Japan na China zimefikia hapo zilipo kwa kutilia mkazo elimu ya ufundi.

"Katika Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo 2016/17 hadi 2020/21 tunalenga kuongeza idadi ya wahitimu wa Vyuo vya Ufundi Stadi(Veta) kutoka 150,000 hadi 700,000 na Vyuo vya Elimu ya Ufundi vinavyotoa elimu ya Kati kutoka 40,000 hadi 80,000,"alisema 

Kuhusu idadi ya wasichana wanaosoma elimu ya ufundi kuwa ndogo alivitaka vyuo vyote vya ufundi nchini kuweka mikakati ya kuongeza udahili ikiwa ni pamoja na kutoa kipaumbele maalum kwa kwa wanafunzi wa kike wanaomba kujiunga.

Pia aliagiza Mamlaka ya Elimu nchini(TEA)kuharakisha upatikanaji wa fedha kiasi cha Sh 1.7 bilioni kilichotengwa kwaajili ya ujenzi wa hosteli za wasichana katika Chuo hicho ili kupunguza pengo katika wavulana na wasichana.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha ATC,Dk Masudi Senzia alisema wahitimu 465 wamemaliza katika ngazi za Astashahada ya awali,Astashahada ,Stashahada na Shahada huku wahitimu wa kike ni 101 sawa na silimia 21 na wahitimu wa kiume ni 364 sawa na asilimia 78.

No comments: