Tuesday, January 23, 2018

DC MHANDO ALEZEA HATUA KWA HATUA MAENDELEO YA WILAYA YA TANGANYIKA

*Amshukuru Rais ,Dk. Magufuli kwa uamuzi wa kuanzisha wilaya hiyo

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

MKUU wa Wilaya ya Tanganyika Salehe Mhando amesema kwa kushirikiana na wananchi wameendelea kutatua changamoto zilizopo wilayani humo huku akielezea hatua kwa hatua miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayoendelea kufanywa.

ASHUKURU UAMUZI WA RAIS

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Michuz Blogu, leo kwa njia ya simu , Mhando amesema wanamshukuru Rais ,Dk.John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuanzisha Wilaya ya Tanganyika kwani imesaidia kusogeza mamlaka karibu, hali iliyochangia kutatuliwa kwa changamoto na kuboreshwa kwa miundombinu ya kimaendeleo.

"Tunamshukuru Rais uamuzi wake wa kuanzisha Wilaya ya Tanganyika iliyoanzishwa rasmi Julai Mosi mwaka 2016.Uwepo wa wilaya hii kumesaidia kwa sehemu kubwa kusogeza huduma kwa wananchi."Uwepo wa wilaya hii kumesaidia kuimarika kwa mindombonu hasa kwa kuzingatia ni wilaya ambayo ipo mpakani.Kwa sehemu kubwa tunampongeza Rais kwa uamuzi wake wa kuona haja ya kuwa na wilaya ya Tanganyika kwani inasukuma kwa kasi maendeleo ya wananchi,"amesema Mhando.

UMEME WILAYANI TANGANYIKA 

Kuhusu nishati ya umeme katika Wilaya hiyo, Mhando anasema kuwa kuna mikakati mingi inayoendelea ya kufanikisha nishati ya umeme inakuwepo katika maeneo yote na kufafanua tayari umeme umefika makao makuu ya wilaya."Wilaya ya Tanganyika ilianza kupata umeme mwaka 2017 baada ya kuanza kusambazwa kwa nguzo za umeme na sasa makao makuu ya wilaya tuna umeme, pia taasisi kadhaa pamoja na kaya 62 tayari nazo zimeanza kupata umeme.

"Malengo yetu ni kuendelea kuweka mikakati ambao utatusaidia kusogeza nishati ya umeme kwa wananchi wa Wilaya ya Tanganyika na hakika tunakwenda vizuri kwani Serikali Kuu nayo imekuwa ikituangalia kwa jicho la aina yeke."Imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kuendelea na miradi ya kimaendeleo na hasa inayohusu kutatua changamoto zilizopo ikiwamo hii ya umeme,"amesema Mhando.

MIUNDOMBINU YA BARABARA

Akizungumzia miundombinu ya barabara, Mhando anasema Wilaya ya Tanganyika imeendelea kufunguka, kwani wanaendelea kuboresha barabara zilizopo ndani ya wilaya hiyo na zile ambazo zinatoka nje ya wilaya yao."Tunaendelea na ujenzi wa miundombinu ya barabara , kwa kueleza tu tayari barabara za Mpanda hadi Kalema na ile ya Mpanda Uvinza zimekamilika.Pia kuna mradi wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 35 kutoka Vikonge hadi Mpanda.

"Tumedhamiria kuhakikisha tunakuwa na barabara za uhakika zitakazopitika wakati wa wote yaani masika na kiangazi na tumeanza kufanikiwa kwenye hili,"amesema Mhando.

WADHIBITI UHARIBIFU WA MAZINGIRA

Anafafanua pamoja na kuendelea kwa miradi ya kimaendeleo, Mhando anasema zipo baadhi ya changamoto wanaendelea kuzitafutia ufumbuzi wake na mojawapo ni ya uharibifu wa mazingira unaofanyika kwenye misitu na vyanzo vya maji.Amesema kuna watu wanaingiza mifugo kwenye misitu iliyopo hasa kwa kuzingatia Wilaya ya Tanganyika kuna eneo kubwa la misitu ambalo sasa linavamiwa .Hivyo Wilaya hiyo imekuwa ikipambana na wote wanaoingiza mifugo na kuharibu mazingira.

"Tumefanikiwa kudhibiti uharibifu wa rasilimali ya misitu na sasa hata Mto Katuma maji yapo tofauti na siku za nyuma.Ziwa Katavi pia maji yapo na hii imesaidia hata wanyama waliopo misitu ya Katavi kuwa salama.Tumedhamiria kulinda misitu yetu maana tunajua umuhimu wa misitu,"amesisitiza.

UPATIKANAJI WA MAJI SAFI

Akizungumzia miundombinu ya maji, Mhando amesema bado ni changamoto lakini tayari wameanza kutafuta ufumbuzi wake kwa kuhakikisha wananchi wa wilaya ya Tanganyika wanapata maji safi na salama.Amesema kuna mradi wa maji wa Majalila na Igagala ambayo imeanza kutoa maji ya bomba na hivyo kupunguza uhaba wa upatikanaji maji.Pia mradi wa maji wa visima 21 ambavyo navyo vinatoa maji .

Amefafanua Wilaya yao ina vijiji 55 ,hivyo wanakwenda vizuri kutoka na malengo ambayo wamejiwekea ."Tayari tumepata mkandarasi kwa ajili ya kufanikisha upatikanaji wa maji ikiwamo katika kata ya Kata Mwese."Tunao mradi wa maji Kamjela ambao nao karibu unaanza kutekelezwa pamoja na mradi wa maji wa Kalema.Hivyo kuna miradi kadhaa ya maji ambayo tunaendelea nayo,".

Amesema jambo la kushukuru Serikali imekuwa ikisaidia kutoa fedha kwa ajili ya kufanikisha miradi ya maendeleo na kutatua changamoto huku akieleza namna ambavyo wilaya inavyotumia fedha wanazokusanya kwa nidhamu na kuhakikisha zinatumika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

UHABA SHULE ZA MSINGI, SEKONDARI

Kuhusu shule za msingi na sekondari, Mhando anasema kwa kuwa wilaya hiyo bado mpya kuna tatizo la uhaba wa shule za sekondari kwani katika kata 16 zilizopo shule za sekondari ziko kwenye kata nane.Hivyo kinachoendelea sasa ni kuhakikisha kunakuwa na sekondari kwa kila kata na wameanza mchakato wa kuondoa changamoto hiyo.

Pia wameendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kushirikiana na wananchi na katika elimua msingi nako kuna changamoto zake lakini nazo zimeweka mikakati ambayo itafanikisha kuzitatua."Idadi ya wanafunzi wa sekondari ni wengi kuliko idadi ya shule zilizopo.Kwetu hii imetufanya tuweke mkakati madhubuti utakaowezesha kila kata kuwa na Serikali yetu imejikita kutatua kero zilizopo sekta ya elimu,"amesema Mhando.
 MKUU wa Wilaya ya Tanganyika Salehe Mhando akishirikiana na Wananchi katika kazi ya ujenzi wa wilaya mpya ya Tanganyika ,mkoani Katavi ."Tumeanzisha ujenzi wa Sekondari ktk Kata 5 kati ya 8 ambazo hazina kabisa Sekondari za Kata,Lengo ni kuhakikisha ifikapo Disemba 2018 kata zote 8 zinakuwa na Sekondari"alisema DC Mhando

MKUU wa Wilaya ya Tanganyika Salehe Mhando akishirikiana na Wananchi katika kazi ya ujenzi wa wilaya mpya ya Tanganyika ,mkoani Katavi ."Tumeanzisha ujenzi wa Sekondari ktk Kata 5 kati ya 8 ambazo hazina kabisa Sekondari za Kata,Lengo ni kuhakikisha ifikapo Disemba 2018 kata zote 8 zinakuwa na Sekondari"alisema DC Mhando

No comments: