Tuesday, January 23, 2018

WATANZANIA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA COMORO

Balozi wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mhe, Sylvester Mabumba (wa pili kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji wa Comoro, Bw. Said Mohamed Omar (wa pili kutoka kushoto), Mkurugenzi wa vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group pamoja na wajumbe waliofuatana nao katika ziara maalum ya kufungua na kuzitangaza fursa zilizopo Tanzania na Comoro.
Balozi wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya comoro pamoja na Wajumbe kutoka clouds Media Group wakiwa katika mazungumzo ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Comoro, Bw. Mouzamildine Youssouf.


BALOZI wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya Comoro,  Sylvester Mabumba ameupokea ujumbe wa Clouds Media Group uliowasili visiwani humo Januari 20 mwaka 2018.

Upo kwenye ziara maalumu ya siku tatu ikiwa na lengo la kushirikiana na ubalozi kuzitangaza fursa mbalimbali zinazopatikana visiwani humo kwa Watanzania. Ujumbe huo wa Clouds Media Group ukiongozwa na Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji, Ruge Mutahaba uliwasili Comoro kutokana na mualiko wa Ubalozi wa Tanzania hapa Comoro

Ambapo lengo lake lilikuwa ni kuja kufanya tathamini ya kuzindua Jukwa la Fursa (FURSA EXPO) Visiwani Comoro kama sehemu ya kuendeleza kampeni za kuwapatia vijana wa kitanzania taarifa muhimu kuhusu fursa za uwekezaji na biashara.

Ubalozi wa Tanzania Visiwani Comoro kwa kushirikiana na Ujumbe wa Clouds Media Group umelenga ifikapo Aprili mwaka 2018 kupanua mianya ya uwekezaji nchini Comoro na kuhakikisha masoko ya uhakika yanapatikana kwa ajili ya bidhaa za Tanzania hasa katika kipindi hiki ambapo Uchumi wa Tanzania unaelekea kuwa ni uchumi wa Viwanda. 

Aidha, Balozi akiwa ameambatana na ujumbe wa Clouds Media Group amepata fursa ya kuonana na kufanya mazungumzo na wadau kutoka sekta mbalimbali za Serikali ya Comoro, Mashirika ya Umma na Sekta Binafsi. “Serikali ya Tanzania itaendelea kufungua maeneo mapya ya ushirikiano sambamba na kuhakikisha vijana wananufaika na ushirikiano baina ya nchi na nchi ulioanzishwa na mataifa yao” mesema Balozi

Aidha, Mhe. Balozi alielezea anataraji ziara hiyo italeta matokeo chanya na kwamba kuzinduliwa kwa jukwaa la FURSA EXPO ni sehemu mojawapo ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ambayo inalenga kwenye Diplomasia ya Uchumi na kwamba kupitia jukwaa hilo bidhaa za Tanzania zinauhakika wa kuingia kwenye Soko la Comoro kwani nchi ya Comoro inaitegemea Tanzania kwa kiasi kikubwa katika mahitaji yake mbalimbali. 

Pia ujumbe wa Clouds Media Group ulitumia nafasi hiyo kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji Visiwani Comoro, Ndg. Said Mohamed Omar, Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Kitaifa ya Utalii, Ndg. Mouzamildine Youssouf pamoja na Mkurugenzi wa Uhamasishaji wa Vijana. Katika mazungumzo hayo, wajumbe walionesha nia ya kutaka kushirikiana kwa pamoja katika kuendesha kampeni itakayoibua maeneo muhimu ya kimkakati ambayo Vijana wa Kitanzania na wale wa KiComoro wanaweza kushirikiana.


Naye Bw. Ruge Mutahaba kwa upande wake alieleza kufurahishwa na fursa mbalimbali zinazopatikana Comoro na kuahidi kuendelea kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania Visiwani hapa kuhakikisha kwamba FURSA EXPO Comoro inafanikiwa na kuleta matokeo chanya kwa lengo la kuinua uchumi wa vijana wa Kitanzania na wa KiComoro.

No comments: