Saturday, November 11, 2017

RC MAHENGE ATOA NENO KWA WATUMISHI DODOMA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge akikagua kitalu cha miche ya Mikorosho ambayo itaanza kugaiwa bure kwa wananchi kwa lengo la kuipanda na kukuza kilimo cha zao la korosho wilayani Mpwapwa
Sehemu ya Kitalu cha Miche ya Mikorosho kilichopo eneo la Magereza Mpwapwa, jumla ya tani sita (6) za mbegu bora za mikorosho zimeoteshwa kwa lengo la kugawa bure miche ya mikorosho kwa wananchi kuipanda na kukuza kilimo cha zao hilo Wilayani Mpwapwa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge namna miti ya mikorosho ilivyozaa korosho kwenye shamba darasa la Magereza Mpwapwa.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge akikagua maendeleo ya ujenzi wa Kiwanda cha kukamua mbegu za alizeti na usindikaji mafuta ya alizeti cha mjasiriamali Ndg. Sangito Akyoo. 



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge amewataka watumishi wa Umma na Taasisi mbalimbali kwenye Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuwahudumia Wananchi kikamilifu na kwa uadilifu wakitambua kuwa sasa Mkoa wa Dodoma ndio Makao Makuu ya Nchi.


Aidha amesema yapo baadhi ya maeneo Mkoa bado haufanyi vizuri hususani katika sekta ya elimu ambapo hali ya ufaulu hairidhishi.

Akiwa wilayani Mpwapwa katika ziara yake ya kutembelea wilaya za Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kujitambulisha Dkt. Mahenge amesema eneo la Elimu ya Msingi na Sekondari hali ya ufaulu hairidhishi ambapo Mkoa umeshika nafasi ya 24 kati ya Mikoa 26 kwenye matokeo ya Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2017, Wakati kwa upande wa Matokeo ya Mtihani wa kumaliza elimu ya Sekondari kidato cha nne mwaka 2016 Mkoa ulikuwa wa 19 kati ya Mikoa 26.

Amesema viongozi hao wanayodhamana kubwa kwa Wanadodoma kwenye masuala yote ya maendeleo kama vile Elimu, Afya, Kilimo, Uwekezaji, Viwanda na Biashara na kutumia fursa ya kuwa jirani na Serikali katika kusukuma mbele masuala ya Maendeleo kwenye Mkoa.

Amewataka Viongozi na Watendaji wote kwenye Wilaya za Mkoa wa Dodoma kutambua wana jukumu kubwa la kusimamia elimu kwenye Wilaya zao na ameagiza kila Wilaya ikae na kufanya tathimini ya sababu ya kufanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani ya msingi na sekondari na kutafuta majibu ya changamoto hizo na pia kubuni mikakati itakayo ukwamua Mkoa kielimu na baadae mipango hiyo ya Wilaya ijadiliwe pamoja ili kutoka na mkakati mmoja wa Mkoa wa kupandisha hali ya Elimu na Ufaulu kwenye Mkoa wa Dodoma.

Dkt. Mahenge amezitaka Wilaya za Mkoa wa Dodoma kujipanga vizuri kwenye Sekta ya kilimo akiainisha kuwa Viongozi na Watendaji kwenye Mkoa wana jukumu la kuhakikisha tatizo la upungufu wa chakula linakuwa historia kwenye Mkoa wa Dodoma kwa kuhimiza Wananchi wetu kulima mazao yenye kustawi hata katika mazingira ya maji kidogo na hali ya hewa ya Mkoa wa Dodoma kama Mtama, Uwele, Muhogo na Alizeti.

Aidha, Katika kukuza mapato na uchumi wa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma, Dkt. Mahenge amezitaka Halmashauri hizo kwa sasa kuanza uwekezaji kwenye kilimo cha Korosho ambacho kimewasaidia wakulima wengi kuinua hali ya uchumi kwenye maeneo wanayolima zao hilo.

Amesema tayari wataalamu wa kilimo wamebainisha kuwa zao hilo linauwezo wa kustawi vizuri na kuwa na mavuno ya kuridhisha kwenye Mkoa wa Dodoma na kiuchumi soko la Korosho lipo na bei ya zao hilo kwenye soko ni nzuri. Ameipongeza Wilaya ya mpwapwa kwa jitihada walizoanza za kuwekeza kwenye kilimo cha Korosho na amezitaka Wilaya nyingine Mkoani Dodoma kuona namna nazo zinavyoweza kuanza utekelezaji wa mpango huo wa kilimo cha Korosho.

Dkt. Mahenge amezitaka Wilaya za Mkoa wa Dodoma kuweka mkakati wa utekelezaji wa Kampeni ya Serikali ya Uanzishaji wa Viwanda kwa kila Mkoa uliozinduliwa hivi karibuni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Seleman Jafo kwa kuzishirikisha hadi ngazi za chini kwenye wilaya zetu na kutaka mkakati huo ulenge kuanzisha viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotokana na malighafi ya mazao yanayolimwa kwenye Mkoa wa Dodoma.

Aidha, ametaka Mkakati huo wa uanzishaji Viwanda kwa kila Wilaya uwajumuishe Vijana na Wanawake, kwa kuwaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya Mkoani Dodoma kuhakikisha wanatenga asilimia kumi (10%) kwenye bajeti zao za Halmashauri kwa ajili ya miradi ya uzalishaji mali na uchumi kwa vijana na wanawake, na fedha hizo zipelekwe kwenye kuanzisha viwanda vidogovidogo kwa ajili ya makundi hayo.

Dkt. Mahenge amebainisha kuwa tayari amekutana na kuzungumza na makundi mbalimbali kwenye Mkoa yakiwemo ya Wazee, Viongozi wa Madhehebu ya Dini, Wafanyabiashara na Wakuu wa Vyuo Vikuu na Elimu ya Juu ambapo amekutana na Malalamiko ya baadhi ya watumishi kutokuwa waadilifu na kutotekeleza wajibu wao ipasavyo wa kuwahudumia wananchi.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Jabir Shekimweri amemwelezea Dkt. Mahenge kuwa bado Makusanyo ya Wilaya hiyo hayaridhishi kwani kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Wilaya ya Mpwapwa ililenga kukusanya zaidi ya shilingi 2,800,000,000 lakini mapato halisi yalikuwa Shilingi takribani Bilioni moja, akibainisha kuwa hali hiyo inatokana na uchache wa vyanzo vya mapato hivyo ili kukuza mapato na hali ya uchumi tayari Wilaya ya Mpwapwa imeanza utekelezaji wa Mkakati wa kukuza kilimo cha Korosho.

“Kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho tayari Wilaya ya Mpwapwa tumepokea jumla ya tani sita (6) za mbegu bora na za muda mfupi za Korosho na pia tumefikia makubaliano na Bodi ya Korosho ya kujenga kiwanda cha kubangua Korosho hapa Mpwapwa jambo ambalo litakuza sana kilimo cha korosho na kuingizia Wananchi na Wilaya kwa ujumla pato kubwa na kukuza uchumi” amebainisha Mheshimiwa Shekimweri.

Mheshimiwa Shekimweri amesema tayari Wilaya ya Mpwapwa imeanza kuitikia Maelekezo ya Serikali ya kuanzisha Viwanda na tayari Wilaya imetenga eneo la hekta 3.7 kwa ajili ya uanzishaji wa viwanda ambapo baada ya upimaji wa eneo hilo jumla ya viwanja 40 vilipatikana kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.

Pamoja na kuzungumza na watumishi wa Serikali Wilayani humo, Mkuu wa Mkoa Dkt. Mahenge alitembelea kitalu cha miche ya Korosho kwenye Gereza la Mpwapwa,alitembelea kituo cha utafiti wa Mifugo Mpwapwa, Mradi wa kiwanda cha kukamua alizeti na kujibu kero za wananchi kwenye mkutano wa hadhara kijiji cha Chitemo.

No comments: