Wednesday, November 22, 2017

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, MHE. JAPHET HASUNGA AAGIZA KUUNDWA KWA CHOMBO CHA KUDHIBITI UBORA WA MAZAO YA MISITU NCHINI



Na Hamza Temba – WMU
..........................................................
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kubuni utaratibu mpya ikiwemo kuanzishwa kwa chombo kitakachosimamia upangaji wa madaraja ya ubora wa mbao zinazozalishwa hapa nchini ziweze kukidhi viwango vya mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Ametoa agizo hilo jana kwenye kikao cha majumuisho na watumishi wa Shamba la Miti la Serikali la Kiwira ambalo linasimamiwa na wakala huyo wakati anahitimisha ziara yake ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.

“Kuna changamoto kubwa kwenye soko la mbao, kwa kiwango kikubwa mbao zetu nyingi tunaziuza hapa nchini, Lazima tufike mahali hizi mbao tuwe tunaziexport (uza nje) kwa kiwango kikubwa. Lakini ili tufikie malengo hayo mbao zetu lazima ziwe kwenye kiwango kinachokubaliwa.

“Mbao zinazokuwepo kwenye soko letu la ndani huwezi kuzitenganisha kwamba hizi ni za TFS au za mwananchi wa kawaida, nyingine zina ubora nyingine hazina, agizo langu kwenu kaeni chini kama watendaji tuje na utaratibu utakaotuwezesha kuzipanga kwenye madaraja, daraja la kwanza, la pili, la tatu au la nne ili mnunuzi ajue ananunua mbao ya ubora wa aina gani,” alisema Hasunga.

Alisema amepata taarifa kuwa baadhi ya wananchi wanavuna miti ambayo haijakomaa jambo ambalo linaathiri ubora wa mbao kwenye soko kwa kutokidhi mahitaji ya wateja, hivyo akaagiza Wakala huyo kubuni mbinu mpya za kuwalinda wateja ikiwemo kuanzishwa kwa chombo maalum cha udhibiti wa ubora wake.

"Kwa maeneo mengine tuna TBS, kwenye chakuka tuna TFDA, kwenye mbao je? Nani anaregulate?(dhibiti), ni lazima tufike mahali tuwe na mdhibiti atakayetusaidia kuhakikisha kwamba ubora unakuwepo,” alisema Hasunga.

Aidha alitoa wito kwa taasisi hiyo kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuvuna miti ikiwa imeshakomaa ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa miche ya miti na kuhamasisha wananchi wapande miti zaidi kwa faida yao na taifa kwa ujumla.

Akizungumzia nidhamu kwenye Utumishi wa Umma, Naibu Waziri Hasunga alisema Serikali ya awamu ya tano haitomvumilia mtumishi yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa, uzembe au uvivu kwenye kutekeleza majukumu ya Serikali kwa kua sifa hizo ni chanzo kimojawapo kikubwa cha umasikini nchini.

Kwa upande wa kampeni ya upandaji miti kitaifa, alisema Serikali itafuatilia nchi nzima kuona utekelezaji wa agizo hilo ambalo linaitaka kila Wilaya kupanda miti milioni moja na laki tano kwa mwaka ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha miti mingi zaidi inapandwa kwa kuwashirikisha zaidi wananchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Zawadi Mbwambo alisema taasisi hiyo imewahi kupokea malalamiko juu ya ubora hafifu wa baadhi ya mbao zinazopatikana kwenye soko ambazo baadhi ya wananchi hutumia jina la Shamba la Miti Sao Hill kuziuza na hivyo kuharibu sifa ya shamba hilo.

Alisema maagizo yote aliyoyatoa Naibu Waziri Hasunga yatafanyiwa kazi kupitia vikao halali vya kiutendaji vya taasisi hiyo ikiwemo vile vya kuandaa mikakati ya utekelezaji wa majukumu yake ya uhifadhi.

Awali Meneja wa Shamba la Miti Kiwira, William Dafa akiwasilisha taarifa yake kwa Naibu Waziri Hasunga, alisema shamba hilo ambalo lilianzishwa mwaka 1964 likiwa na hekta 2,713 limekuwa na maendeleo mazuri ambapo mwaka 2016/2017 lilivuka malengo ya makusanyo ya mapato ya Serikali kutoka bilioni 1.3 hadi bilioni 1.7.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) akizungumza na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja (wa pili kushoto) alipofika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo akiongozana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Juliana Shonza (wa pili kulia) kwa ajili ya kujitambulisha wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi mkoani humo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akimsikiliza Meneja wa Shamba la Miti Kiwira, William Dafa wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi katika shamba hilo jana katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akimsikiliza Meneja wa Shamba la Miti Kiwira, William Dafa wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi katika shamba hilo jana katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya. 
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Zawadi Mbwambo (kushoto) wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi kwenye Shamba la Miti Kiwira lililopo Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya jana.

Mti huu wa kumbukumbu ulipandwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1965 katika shamba la miti la Serikali  la Kiwira katika Wilaya ya Rugwe Mkoani Mbeya.
 Mti alipanda Mwalimu Nyerere mwaka 1965 katika shamba la miti Kiwira.
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga akizungumza na watumishi wa Shamba la Miti Kiwira  wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi kwenye Shamba hilo katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya jana.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Zawadi Mbwambo akizungumza katika kikao hicho.
Baadhi ya watumishi wa shamba la miti Kiwira.

No comments: