Saturday, October 28, 2017

Kampuni ya Ujenzi ya CRJE yajitosa udhamini Rock City Marathon

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Ujenzi ya CRJE (East Africa Ltd), Bw Xie Zhixiang (kushoto) akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya sh milioni 10 kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio za Rock City Marathon Bw Zenno Ngowi (kulia) ikiwa ni udhamini wa mbio hizo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Wengine ni pamoja na Mahusiano na Utawala wa kampuni ya CRJE Bw Henry Kasapira (wa pili kushoto) na Mratibu wa mbio hizo kutoka kampuni ya Capital Plus International (CPI), Bw. Steven Otieno

ZIKIWA zimebaki siku chache tu kufanyika kwa mbio za Rock City Marathon, kampuni ya Ujenzi ya CRJE leo imekabidhi hundi yenye thamani Tsh milioni 10 kwa waandaaji wa mbio hizo ikiwa ni udhamini wa kampuni hiyo.

Mbio zinazotarajiwa kufanyika Octoba 29 mwaka huu, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Akikabidhi hundi hiyo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo Bw Zenno Ngowi, Ofisa Mahusiano na Utawala wa kampuni ya CRJE Bw Henry Kasapira alisema udhamini huo unalenga kuunga mkono juhudi za serikali kuhamasisha michezo na utalii wa ndani hapa nchini.

“Michezo huleta uimara wa afya na uimara wa afya ndio nguzo muhimu katika sekta ya ujenzi na ndio maana pamoja na kuinua utalii tunaunga mkono pia mpango huu unaolenga kuhamasisha uimara wa afya za wananchi.’’ Alisema.

Aliahidi kuwa kampuni yake itaendelea kushirikiana na waandaaji wa mbio hizo katika kuboresha zaidi mbio hizo kwa miaka ijayo huku akitoa wito kwa vijana wengi zaidi kutoka mikoa mbalimbali kujiandaa kwa ajili ya mbio hizo.

Akizungumza baada ya kupokea hundi hiyo, Ngowi alisema ushiriki wa kampuni hiyo ya kimataifa katika kufanisha Rock City Marathon utaongeza viwango vya ubora wa mbio hizo sambamba na kuwavutia zaidi washiri wa kamataifa ambao wamekuwa wakiiamini kampuni kutokana na utendaji wake wenye ufanisi.

Naye, Mratibu wa mbio hizo kutoka kampuni ya Capital Plus International (CPI), Bw. Steven Otieno amesema maandalizi ya mbio hizo tayari yamekamilika huku ushiriki wa viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza na wakuu wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenye mbio hizo ukiwa ni miongoni mwa vivutio vikubwa vinavyotarajiwa kupamba mbio hizo.

“Tunatarajia kwamba viongozi hawa wa kiserikali pamoja na wadhamini wetu wengine wakiwemo PUMA, Tiper, NSSF, RedBull, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), New Mwanza Hotel, EF Out door, CF Hospital, KK Security, na kampuni ya uchapishaji ya SDS watashiriki kikamilifu katika mbio za KM 5 sambamba na watu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino,’’ alitaja.

Alisema kamati ya maandalizi ya mbio hizo imejiandaa vilivyo na maandalizi yote yamekamilika, ikiwemo kupokea wakimbiaji kutoka nje ya nchi na washiriki wengine.

“Tunatarajia kuwa na washiriki zaidi ya 4000 wakiwemo wakimbiaji wa kimataifa, wakimbiaji kutoka mashirika mbalimbali, walemavu wa ngozi yaani Albino pamoja na wanafunzi.’’ Alitaja.

Akizungumzia usajili wa mbio hizo Bw. Otieno alisema kwa wakazi wa jiji la Mwanza na mikoa jirani wanaweza kujisajili kwa kuchukua fomu katika Ofisi za michezo wilaya zote za mkoa wa Mwanza, Ofisi za riadha mikoa ya Geita, Simiyu na Shinyanga.

Sehemu nyingine ni pamoja na Uwanja wa Nyamagana, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Mwanza, Kituo cha michezo Malya, Shule ya Kimataifa ya Isamilo, New Mwanza Hotel na Ofisi za EF Out door zilizopo jingo la Rock City Mall.

“Kwa upande wa Dar es Salaam Fomu za ushiriki pia zinapatikana jengo la SHAMO Tower, Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam’’ alitaja. Zaidi kuhusu usajili wa mbio hizo zinazoandaliwa kwa kushirikiana na Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza (MWAA), Bidan alisema unaweza kufanyika kupitia tovuti ya kampuni hiyo ambayo ni www.capitalplus.co.tz

No comments: