Friday, September 22, 2017

WAFANYAKAZI WASHAURIWA KUPIMA AFYA MARA BAADA YA KUSTAAFU.

Na: Lilian Lundo – MAELEZO Dodoma.

Wafanyakazi nchini wameshauriwa kupima afya zao mara tu wanapostaafu ili kujihakikishia ikiwa hawajaathirika na kazi ambazo wamekuwa wakizifanya.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Eric Shitindi alipokuwa akifungua semina ya viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi juu ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, leo Mjini Dodoma.

“Kumekuwa na mazoea kwa wafanyakazi kupima Afya pale tu wanapoajiriwa na kutotilia maanani upimaji afya zao mara wanapostaafu ili kujua ikiwa kazi wanazozifanya zimewaathiri kwa kiasi gani,” amesema Shitindi.

Ameendelea kwa kusema kuwa, upimaji wa afya mara baada ya kustaafu utasaidia watumishi kujua afya zao na ikiwa watakuwa wameathirika upitia kazi walizokuwa wakizifanya basi mwajiri atawajibika mkulipa fidia mtumishi huyo.

Aidha amesema kuwa licha ya juhudi za Serikali katika kusimamia Usalama na Afya maeneo mengi ya kazi sio ya kuridhisha kutokana na waajiri wengi kutokuzingatia sheria na kanuni mbalimbaliza Usalama na Afya.

Hivyo basi kutokana na waajiri hao kutofuata sheria na kanuni hizo kumesababisha maeneo mengi ya kazi kulalamikiwa kutokana na ukiukwaji wa sheria hizo.

Vile vile amesema kuwa baadhi ya waajiri na wafanyakazi wana uelewa mdogo  kuhusu kuzingatia maelekezo ya Usalama na Afya Mahali pa kazi ikiwemo matumizi sahihi ya vifaa kinga.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Khadija Mwenda amesema kuwa, wameamua kuandaa semina hiyo kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi hapa nchini ili na wao wakatoe elimu hiyo kwa wafanyakazi wote nchini kutokana na wafanyakazi hao kutokuwa na uelewa mzuri juu ya masuala ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.
 Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) Bi. Khadija Mwenda akiongea na Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania(TUCTA) na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wakati wa Ufunguzi wa Semina kuhusu masuala ya usalama na afya mahala pa kazi Leo Mjini Dodoma.Kulia ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw.Qambos Sule
 Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Bw. Eric Shitindi akiongea na Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania(TUCTA) na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wakati wa Ufunguzi wa Semina kuhusu masuala ya usalama na afya mahala pa kazi ambapo aliwashauri wafanyakazi nchini kupima afya mara wanapostaafu ili kujihakikishia kama hawajaathirika na kazi walizokuwa wanafanya.Katikati ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw.Qambos Sule na Kushoto ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) Bi. Khadija Mwenda 
 Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw.Qambos Sule akiongea naViongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania(TUCTA) na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wakati wa Ufunguzi wa Semina kuhusu masuala ya usalama na afya mahala pa kazi, kulia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Bw. Eric Shitindi na kushoto ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) Bi. Khadija Mwenda
 Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw.Qambos Sule (KUSHOTO) na Katibu Mkuu Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw. Jones Majura(KULIA) wakiteta jambo na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Bw. Eric Shitindi baada ya ufunguzi wa Semina kuhusu masuala ya usalama na afya mahala pa kazi leo Mjini Dodoma
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Bw. Eric Shitindi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Semina kuhusu masuala ya usalama na afya mahala pa kazi Leo Mjini Dodoma. PICHA NA IDARA YA HABARI-MAELEZO,DODOMA

No comments: