Friday, August 25, 2017

Waziri Profesa Mbarawa Akagua Ujenzi wa Reli ya Kati ya Kisasa

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika Hodhi la Reli (RAHCO) Bw. Masanja Kadogosa akielezea jambo mbele ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto) wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge) ambapo awamu ya yenye urefu wa Km 205 inajengwa kutoka Dar – Moro.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua ujenzi wa tuta kwa ajili ya njia ya reli alipotembelea eneo la Soga (Kibaha) wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Reli ya kiwango cha kimataifa (Standard Gauge) yenye urefu wa kilomita 205 kutoka Dar – Morogoro leo. Kutoka kulia ni Meneja Mradi wa SGR Mhandisi Maizo Mgedzi, Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Kampuni ya Yapi Merkezi Bw. Abdullah Kilic na Mhandisi Felix Nnalio.
Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Kampuni ya Yapi Merkezi Bw. Abdullah Kilic akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu ujenzi wa tuta la reli ya kisasa ya SGR alipotembele eneo la Soga (kibaha) leo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akifafanua jambo mbele ya Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Kampuni ya Yapi Merkezi Bw. Abdullah Kilic (katikati) alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Reli ya kiwango cha kimataifa (Standard Gauge) ambapo awamu ya kwanza inajengwa kutoka Dar – Moro yenye urefu wa 205km.
Muuonekano wa awali wa tuta la reli linaloendelea kujengwa kwa kuondolewa tabaka la udongo wa kilimo na kuwekewa udongo wa ujenzi katika eneo la Soga (Kibaha) ambapo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa unaendeleo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitazama kifaa cha kupima mgandamizo wa ardhi mara baada ya ardhi kushindiliwa alipokagua ujenzi wa tuta la reli katika eneo la Soga (Kibaha).
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiendelea na shughuli ya ujenzi wa karakana ya kutengeneza mataluma ya reli alipokagua ujenzi alipofanya ziara katika eneo la Soga (Kibaha).


………………………….


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi Yapi Merkezi na Motaengil Africa anayejenga Reli ya kati ya kisasa (Standard Gauge) sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro kilomita 205 kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ndani ya miezi thelathini iliyopangwa.

Akizungumza mara baada ya kukagua tuta litakapojengwa reli hiyo kutoka pugu, soga hadi ngerengere profesa mbarawa amepongeza kazi inayoendelea na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ili kazi ya kutandika reli ianze katika muda mfupi ujao.

“Hakikisheni kazi ya ujenzi wa tuta na kiwanda cha kutengeneza mataruma ya zege vinakamilika katika muda wa miezi mitatu kutoka sasa ili kwenda na ratiba ya ujenzi huo,” amesema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa amekagua kiwanda cha kutengeneza mataruma ya zege yatakayotumika katika ujenzi wa reli hiyo na kusisitiza umuhimu wa mkandarasi kutoa fursa za ajira kwa wananchi wanaozunguka reli hiyo.

“Wale mtakaopata ajira katika reli hii hakikisheni mnafanyakazi kwa bidii na uaminifu ili kuwezesha ukenzi kuwa katika ubora unaotakiwa na kukamilika kwa wakati”, amesisitiza profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli (TRL) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli RAHCO) Bwana Masanja Kadogosa kuanza mchakato wa kuagiza vichwa vipya vya treni vinavyowiana na Reli hiyo ili reli itakapokamilika kusiwe na hoja ya kusubiri vichwa hivyo.

Aidha amesisitiza umuhimu wa TRL na RAHCO kuandaa wataalam watakaotumika kuendesha Reli hiyo ya kisasa kwa kuwapatia mafunzo ya kiufundi na kibiashara ili kuhakikisha utendaji wa Reli hiyo unakuwa wenye tija.

Ujenzi wa Reli ya kisasa ya kati (Standard Gauge) awamu ya kwanza inayoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa Kilomita 205 unatarajiwa kukamilika 2019 na Serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha inapata fedha ya Ujenzi wa sehemu ya Morogoro-Dodoma.

Zaidi ya Kilomita 2600 za Reli ya Kisasa (Standard Gauge) ZINATARAJIWA kujengwa kutoka Dar es Salaam –Morogoro-Dodoma –Tabora-Isaka-Mwanza na Tabora –Kaliua-Kigoma ili kuiunganisha Tanzania nan chi jirani na hivyo kuboresha huduma za uchukuzi na biashara.

Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments: