Friday, August 25, 2017

WAZIRI AWAPONGEZA WASHIRIKI WA MKUTANO WA GHACOF KWA KUWEZESHA SAYANSI YA HALI YA HEWA KUTUMIKA KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO YA JAMII.

Picha ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (MB) katika picha ya pamoja na washiriki mbalimbali wa Mkutano wa 47 wa maandalizi ya mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa msimu wa mvua za vuli (Oktoba-Disemba 2017) kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (Greater Horn of Africa Climate Outlook Forum-GHACOF-47), Zanzibar Beach Resort, tarehe 21-22 Agosti 2017
-------------------------------------------------------
 “Napenda kuwapongeza GHACOF kwa kuwezesha sayansi ya hali ya hewa kutumika katika shughuli za maendeleo ya jamii, nikiangalia kwa upande wa nchi yetu ya Tanzania kumekuwa na ongezeko la mahitaji na matumizi ya huduma za hali ya hewa kwa kiasi kikubwa sambamba na wigo mpana wa uelewa wa matumizi ya taarifa hizo, ambapo inasaidia sana wananchi kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa,” haya aliyasema Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (MB) wakati akifungua rasmi Mkutano wa 47 wa maandalizi ya utabiri na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (Forty Seventh Greater Horn of Africa Climate Outlook Forum (GHACOF-47) kwa msimu wa mvua za vuli wa mwezi Oktoka hadi Desemba 2017.
Katika mahojiano yaliyofanyika na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi alielezea dhumuni la kukutana kwa wataalamu wa mkutano huo kuwa ni kujadili, kukubaliana kwa pamoja na kutoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa msimu wa mvua za vuli kuanzia mwezi wa Oktoba hadi Desemba 2017 kwa Kanda ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika. Aidha aliongezea kuwa baada ya taarifa hiyo kutolewa kila nchi shiriki ikiwemo Tanzania itakaa na kuandaa taarifa yake ambapo  kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) taarifa rasmi itatolewa kwa vyombo vya habari mwishoni mwa mwezi Agosti 2017.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Kituo cha Ufuatiliaji wa Hali ya Hewa cha Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika (ICPAC) Dkt. Guleid Artan akizungumza katika ufunguzi huo alisema, ICPAC kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wanatekeleza programu ya utoaji wa tahadhari na kwa wakati (Integrated Regional Early Warning System (IREWS)) ukiwa na lengo la kuhakikisha nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika wananufaika kwa kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zitolewazo zinafika kwa jamii kwa wakati na zinatumika katika kupunguza madhara ya yatokanayo na hali mbaya ya hewa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A, Zanzibar Mhe. Mwinyi Ussi Abdallah Hassan akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi aliwataka wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa kwa karibu kwa kutumia njia za kisasa zilizopo.
GHACOF ni Mkutano unaowakutanisha wataalamu wa hali ya hewa kama watoa huduma pamoja na wataalamu kutoka katika sekta mbalimbali kama watumiaji kutoka nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika kwa lengo la kujadili, kuandaa na kutoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa msimu husika katika ukanda huu.

IMETOLEWA NA: MONICA MUTONI, AFISA HABARI, 
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

No comments: