Barabara ya lami ya Kia-Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ambayo imeshakabidhiwa kwa Serikali, inaendelea kuwa kwenye kipindi cha matazamio kwa muda wa mwaka mmoja.
Mradi huo wa barabara uliokabidhiwa serikali Mei 31 mwaka huu, mkandarasi wake anaendelea na kazi ndogo ndogo za ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua, vivuko na vituo vya basi hasa eneo la Kairo.
Meneja wa wakala wa barabara nchini (Tanroads) mkoa wa Manyara, mhandisi Bashiri Rwesingisa aliyasema hayo wakati akisoma taarifa ya mradi huo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi) mhandisi Joseph Nyamhanga alipotembelea eneo hilo.
Mhandisi Rwesingisa alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 27 iliyojengwa na kampuni ya China Henan International Cooperation Group (Chico) kwa gharama ya sh32.2 milioni, chini ya usimamizi wa ujenzi mhandisi mshauri M/s LEA International Ltd ya India kwa ushirikiano na kampuni ya DOCH Tanzania Ltd.
Alisema kazi zilizotekelezwa ni ujenzi wa kiwango cha lami urefu wa kilometa 27 ikijumuisha Kia hadi Mirerani, Mirerani hadi eneo la uwekezaji la (EPZ), barabara ielekeayo Arusha inayopitia Mbuguni, barabara ya kuingia na kutoka kituo cha mabasi Mirerani na mzunguko kiwanda cha TanzaniteOne.
"Ujenzi wa barabara hii umehusisha pia kujenga mifereji ya pembezoni mwa barabara kwenye maeneo ya mji, sehemu za kuvuka mifugo na sehemu za kuvushia huduma muhimu kama waya za simu na umeme," alisema mhandisi Rwesingisa.
Alisema mradi huo umekuwa na changamoto za migomo ya wafanyakazi, wananchi kugoma kuondoa mali zao ndani ya hifadhi ya barabara.
Alisema mipango ya baadaye ni kujenga kilometa 114 barabara kwa kiwango cha lami itakayounganisha eneo la EPZ na mji mdogo wa Orkesumet, makao makuu ya wilaya ya Simanjiro, kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia ujenzi, mhandisi Joseph Nyamhanga alipongeza jitihada zilizofanyika kwa pande zote hadi barabara hiyo ikamalizika.
Mhandisi Nyamhanga alisema wakati wanasubiri barabara hiyo kuzinduliwa wakati inaendelea kutumika, watumiaji wanapaswa kufuata masharti ya matumizi ya barabara hiyo ili waitunze.
Aliitaka jamii ya eneo hilo ambao kwa muda mrefu walikuwa wanalilia utengenezwaji wa barabara na ndiyo wanufaika wa mradi huo, kuutunza vizuri kwani ni kwa ajili ya faida yao na vizazi vijavyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi) mhandisi Joseph Nyamhanga (katikati) akizungumza na viongozi wa wakala wa barabara nchini (Tanroads) Mkoa wa Manyara, alipotembelea eneo la mji mdogo wa Mirerani, (kushoto) ni meneja wa Tanroads Mkoani Manyara, mhandisi Bashiri Rwesingisa
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Manyara, mhandisi Bashiri Rwesingisa (aliyevaa shati la maua) akimwelezea Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi) Joseph Nyamhanga (kushoto kwake) juu ya barabara ya lami ya Kia - Mirerani, ambayo imemalizika inasubiri kufunguliwa.
No comments:
Post a Comment