Thursday, August 17, 2017

WATUMISHI WA UMMA WANATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA SHERIA

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Dkt. Steven J. Bwana (pichani) amewataka watumishi wa umma kuhakikisha wanafanya kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwenye utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza katika mahojiano maalum hivi karibuni, Dkt. Bwana amesema Tume katika kutekeleza majukumu yake ya msingi ya ukaguzi wa rasilimali watu na kushughulikia rufaa na malalamiko, imebaini kuwepo kwa ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu miongoni mwa Watumishi wa umma, Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu.

Amesema kuwa baadhi ya Watendaji Wakuu wanashindwa kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria, watumishi wenye utendaji usioridhisha na wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma walio chini yao. Tatizo hili lipo zaidi kwa baadhi ya Halmashauri zetu na Taasisi za Umma.

“Kumekuwa na udhaifu mkubwa kwa baadhi ya Watendaji Wakuu ambao wameshindwa kuchukua hatua za nidhamu mapema dhidi ya watumishi walio chini yao. Utakuta mtumishi anatoweka tu kazini bila kutoa taarifa wala kuomba ruhusa! Mtumishi kutokuwepo kazini kwa siku tano bila ruhusa wala sababu za msingi adhabu yake ni kufukuzwa kazi. Inashangaza kuona mtumishi wa umma hayupo katika kituo chake cha kazi kwa zaidi ya siku tano, siku 115 na Mwajiri wake hajui, wala hachukui hatua.” Amesema.

Hata hivyo, Dkt. Bwana ameonyesha kutoridhishwa na hali ya utendaji kazi katika baadhi ya Halmashauri. Alisema, “Rufani nyingi tunazopata zinatoka huko, kuna haja ya kurekebisha mambo mengi sana hasa kwenye Halmashauri zetu, hakuko sawa kwa upande wa usimamizi wa Rasilimali watu. Kuna wizi kule, kuna matumizi mabaya ya fedha za umma na mali za Halmashauri.

Japokuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali “CAG” anafanya kazi nzuri ya ukaguzi wake na kutoa ripoti, sehemu fulani watu wanachukuliwa hatua za kisheria, lakini hayo maeneo yanahitaji kusimamiwa kikamilifu zaidi. Bado kuna mapungufu mengi sana” alisisitiza.

Dkt. Bwana amesema kuna haja ya Watendaji Wakuu kupatiwa mafunzo yatakayowawezesha kujielimisha, ili waweze kuzielewa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo na kuzizingatia wakati wote wa kutekeleza majukumu yao. “Tatizo kubwa tunaloliona kwenye Halmashauri kule kuna mambo mengine yanafanyika kana kwamba Viongozi hawajui Sheria ama wanazijua ila wanazipuuza, Pawe na utaratibu wa kuwapatia mafunzo ya aina fulani ya mara kwa mara Viongozi na Watendaji Wakuu, yatakayowawezesha kufanya kazi bila kuvunja Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Vyuo vya Mzumbe, Chuo cha Serikali za Mitaa-Hombolo na Chuo vya Utumishi wa Umma vitumike, kwani vikitumika kikamilifu vitasaidia sana kupunguza matatizo ya utumishi tunayoyaona”. Alisema Dkt. Bwana.

Kwa upande wa Watumishi wa Umma alisema, kumekuwepo kwa tabia na mienendo isiyofaa kwa baadhi ya watumishi wa umma, ambayo imesababisha kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria au za kinidhamu. Miongoni mwa makosa yanayofanywa na Watumishi mara kwa mara na kusababisha kuwachukulia hatua ni kufanya vitendo vinavyodhalilisha utumishi wa umma, wengine kushindwa kutekeleza majukumu yao, uzembe uliokithiri na kusababisha hasara kwa mwajiri, utoro kazini, wizi na kukiuka maadili.

“Kuna tatizo sugu la Watumishi wa Umma, hasa vijana wanaotaka kujiendeleza kwenda masomoni kutokufuata taratibu. Rufani nyingi zinazokuja kwetu unakuta watumishi wamefukuzwa kazi kwa kosa la utoro, wanapokata Rufaa wanajitetea kuwa walikwenda masomoni. Hili ni tatizo sugu, vijana wana haki ya kujiendeleza lakini pia kuna haki ya kufanya kazi mwajiri hawezi kuruhusu watumishi wote wakaondoka kwenda masomoni bila kufuata utaratibu wa mafunzo, wafuate utaratibu” alisema.

Akizungumzia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa Watumishi wa Umma, mfano kwa upande wa watumishi wa umma waliopatikana na vyeti vya kughushi alisema, “Kughushi ni kosa, kosa la jinai, Sheria iko wazi, mtu yeyote akituhumiwa kuwa na cheti cha kughushi akipelekwa Mahakamani anahukumiwa na kupewa adhabu stahiki. Naipongeza Serikali kwenye hili. Mfano mdogo umejitokeza kwenye usaili wa nafasi za kazi katika Afrika ya Mashariki, mara nyingi vyeti vyetu Watanzania haviaminiki, wanachukuliwa wa kutoka Kenya, Uganda na sisi kubaki kulalamika, wakati tunashindwa kushindana kwenye soko la ajira.

Sawa, unakuta mtu anaweza kuongea Kiingereza lakini cheti kinakuwa na mashaka, ni asilia kweli hiki?. Ni vizuri mtu akapata mafanikio kutokana na juhudi yako, siyo hizi njia za mkato mkato. Hapana, ni zoezi ambalo nafikiri liendelee” alisema. “Serikali ya Awamu ya Tano inafanya vizuri, tunaelekea kuzuri, inapambana kurudisha nidhamu na kudumisha Maadili Serikalini. Udokozi umepungua na Nidhamu ya kazi inarudi” alisisitiza.

Alitaja miongoni mwa changamoto zinazoikabili Tume ya Utumishi wa Umma kuwa ni uwezo mdogo wa kuzifikia Taasisi zote za umma kupitia jukumu la ukaguzi wa Rasilimali watu ambao utasaidia kurekebisha kasoro nyingi zitakazobainika na pia utoaji wa huduma. Hata hivyo, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuiwezesha Tume ili iweze kutekeleza majukumu yake. Dkt. Bwana alihitimisha kwa kuwakumbusha watumishi wa umma kuwa wanapaswa kuzingatia Maadili ya Utumishi wa Umma na ya Taaluma zao wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.

Imeandaliwa na:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
TUME YA UTUMISHI WA UMMA
17 AGOSTI, 2017

No comments: