Friday, July 7, 2017

Shilingi bilioni 39.7 za Bodi ya Mikopo ya Elimu hazijarejeshwa na wakopaji

    Na Haji Nassor (OUT), Pemba
Kiasi cha  shilingi bilioni 39.7 kati ya shilingi bilioni 42 zilizotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu Zanzibar ‘BMEJZ’ kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi waliosoma elimu ya juu, ziko mikononi mwa wadaiwa hao, kuanzia mwaka 2006 hadi mwezi Juni mwaka huu.
Wakati fedha hizo zikiwa mikononi mwa wadaiwa, tayari shilingi bilioni 2.3 ndizo pekee, zilizokwisharejeshwa na wakopaji, ambapo kati ya hizo shilingi bilioni 42, shilingi bilioni 7.7 Bodi hiyo ilizirithi kutoka kwa uliokuwa mfuko wa elimu ya juu Zanzibar, ambao ulikoma kufanya kazi zake mwaka 2011.
Bodi hiyo ya mikopo ya elimu ya juu, kila mwezi hukusanya wastani wa shilingi milioni 100, kutoka kwa wakopaji ambao ni wanafunzi kila mwezi hadi mwezi Juni mwaka huu wa 2017.
Aidha taarifa ya Bodi hiyo inaeleza kuwa, tokea kuanza kwake mwaka 2011, wanafunzi zaidi ya 18,994 waliomba kupatiwa mikopo, ingawa baada ya kupitia vigezo husika, ni wanafunzi 5, 293 ndio walioteuliwa kwa kipindi hicho, hadi mwaka huu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini Chakechake, Mratibu wa Bodi hiyo, kisiwani Pemba Ahmada Omar Juma kwa niaba ya Mkurugenzi wake, Idd Khamis Haji, alisema urejeshaji umekuwa wa kusuasua.
Mkurugenzi Iddi alisema, fedha ambazo ziko mikononi shilingi bilioni 39.7 kwa wanafunzi ambao wameshahitimu bado ni nyingi, hivyo ni lazima kwa waajiri iwe wa serikali au taasisi binafsi, kufanya uhakiki na wakiwagundua waliosomeshwa na Bodi hiyo, wasisite kutoa taarifa kwao.
Alieleza kuwa, zipo sheria za Bodi hiyo, ambazo bado hazijatumika ipasavyo juu ya wanafunzi waliomaliza na kutotoa taarifa za makato, lakini kama wataendelea kuwa wasugu, zitatumika ikiwa ni pamoja na kuanza na wadhamini wao.
“Kuna adhabu mpaka shilingi millioni 5,000,000 au kifungo kwa madhamini, lakini hata kwa mkopaji kutakiwa kulipa deni kwa mkupuo au kuligawa, endapo kutakuwa na hali ya kukimbia ulipaji wa deni lake”,alifafanua.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo alisema, changamoto kubwa hasa inayowakabili, ni pamoja na wale wanaoajiriwa kwenye mashirika binafsi na kisha waajiri kushindwa kutoa ushirikiano wa dhati na bodi.
Aidha amesema wengine hata kwa mashirika ya umma, wamekuwa wazito kutoa taarifa za waajiriwa wapya, na wale wanaoondoka nchini kufuata ajira nje ya nchi.
“Suala la kurejesha mikopo halimuhusu mkopaji pekee, bali hata muajiri na mdhamini ni lao, maana fedha hizo zinahitajika kuzngurushwa, ili na wengine wapate kuziomba”,alisema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Hassan Khamis Hassan wa Konde, alisema yeye alishawahi kumpelekea ripoti mwanafunzi aliemdhamini, ambae kwa sasa anaendelea kukatwa.
“Nilimuuliza kuwa, umeshaanza mikato, akanionyesha dharau, lakini baadae nilipomfahamisha alikubali kwenda kujipelekea ripoti na sasa anaendelea kukatwa”,alisema.
Hata hivyo mwanafunzi Asha Mohamed Ali, alisema lazima fedha za kujikimu ziongezwe, maana maisha hasa ya chuoni yamekuwa magumu kutokana na kupanda kwa bei ya vyakula.
Wakati huo huo Mratibu wa Bodi ya mikopo ya elimu ya juu, kisiwani Pemba Ahmada Omar Juma, amempongeza rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Mhe: Dk Ali Mohamed Shein, kwa kutimiza ahadi yake ya kuwaongoeza bajeti kwenye bodi yao.
Alisema ongezeko hilo ni kutoka shilingi bilioni 6.8 kwa mwaka uliomalizika wa fedha 2016/2017 hadi kufikia shilingi bilioni 10.2 kwa mwaka 2017/2018, jambo ambalo limewapa kufanya kazi zao kwa ufanisi.
“Lazima tumpongeza rais wetu pamoja na waziri na hata baraza la wawakilishi, kwa kukubali kutuongezea na kupitisha ongezeko la bajeti kwenye bodi yetu”,alifafanua Mratibu huyo.
Idadi ya wanafunzi wanaopatiwa mikopo na Bodi hiyo, imekuwa ikiongeza kila mwaka, ambapo mwaka 2011/2012 walikuwa wanafunzi 209, mwaka 2012/2013 887, kisha wanafunzi 1,417, wanafunzi 1,611, baadae wanafunzi 575 na mwaka 2016/2017 ni 594 huku malengo ya bodi kwa mwaka 2017/2018 ni kufikia wanafunzi 1,600.
                  

   

No comments: