Naibu Kamishna wa forodha na Maboresho ya Vihatarishi Hatari wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. James Mbunda (Kushoto) na akizungumza na Mwakilishi Mkazi wa Ubalozi wa China anayeshughulikia Uchumi na Biashara, Bw. Lin Zhiyong, wakati wa kufungua mafunzo kuhusu Takwimu na kudhibiti Vihatarishi hatari vya Forodha, yanayotolewa na Chuo cha Forodha cha Shanghai-China, Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali watu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Grace Sheshui akiwakaribisha watoa mafunzo ya Takwimu na Udhibiti Vihatarishi hatari vya Forodha, yanayotolewa na Chuo cha Forodha cha Shanghai-China, Jijini Dar es Salaam.
Naibu Kamishna wa Forodha na Maboresho ya Vihatarishi Hatari wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. James Mbunda, akizungumza na na watoa mafunzo ya Takwimu na Udhibiti Vihatarishi hatari vya Forodha, yanayotolewa na Chuo cha Forodha cha Shanghai-China, Jijini Dar es Salaam, kushoto kwake ni Mwakilishi Mkazi wa Ubalozi wa China anayeshughulikia Uchumi na Biashara, Bw. Lin Zhiyong.
Baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wakisikiliza kwa makini maelezo ya awali ya mafunzo ya kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Ubalozi wa China anayeshughulikia Uchumi na Biashara, Bw. Lin Zhiyong, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
Maafisa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na wengine (kulia) na wakufunzi wa Takwimu na Udhibiti Vihatarishi hatari vya Forodha wakisikiliza maelezo ya awali wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Mkufunzi Mkuu wa masuala ya forodha kutoka Chuo cha Forodha cha Shanghai, China, Profesa Sun Hao (kulia) akizungumza jambo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya siku 14 ya maafisa wa Forodha kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dae Salaam.
Naibu Kamishna wa Forodha na Maboresho ya Vihatarishi Hatari wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. James Mbunda (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wakufunzi, pamoja na maafisa wa forodha kutoka TRA, baada ya ufunguzi wa mafunzo ya siku 14 kuhusu masuala ya forodha, katika ukumbi wa Wizara ya fedha na Mipango, Jijini, Dar es Salaam.
Mwakilishi Mkazi wa Ubalozi wa China anayeshughulikia Uchumi na Biashara, Bw. Lin Zhiyong (Kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali watu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Grace Sheshui (kulia) wakipeana mkono baada ya ufunguzi wa mafunzo ya masuala ya forodha yanayotolewa na Chuo cha Forodha cha Shanghai, China, mafunzo yanayofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM).
Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Kiwango cha biashara kati ya Tanzania na China kimefikia Dola bilioni 4.7 katika kipindi cha mwaka 2015 na kwamba kiwango hicho kinatarajiwa kuongezeka zaidi.
Mwakilishi Mkuu Mkazi wa Masuala ya Uchumi na Biashara, kutoka Ubalozi wa China hapa nchini, Bw. LIN Zhiyong, amesema hayo Jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya forodha kuhusu Maboresho na Vihatarishi hatari vya kiforodha, yanayotolewa kwa maafisa wa forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na wataalamu kutoka Chuo cha Forodha cha Shanghai-China.
Bw. Zhiyong amesema kuwa uhusiano wa Tanzania na China ni wa kihistoria na kwamba hivi karibuni nchi yake iliipatia Tanzania seti 3 za makontena ya vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, vyenye uwezo mkubwa wa kugundua pembe za ndovu, dawa za kulevya na silaha zinazosafirishwa kimagendo kutoka ndani na nje ya nchi.
Alisema pia kuwa hivi sasa nchi yake ni kama imeondoa kabisa kodi kwa bidhaa za Tanzania zinazosafirishwa kwenda China hadi kufikia asilimia 97, na kwamba anatarajia kuona wafanyabishara wa Tanzania wakichangamkia fursa hiyo na kuongeza kiwango cha bidhaa za Tanzania zenye ubora zinazosafirishwa kwenda nchini mwake.
Bw. Zhiyong, amezishauri Idara za Forodha za Tanzania na China kuimarisha ushirikiano na kukuza biashara na uwekezaji kwa faida ya pande zote mbili.
Akizungumzia kuhusu sekta ya elimu, Mtaalamu huyo wa masuala ya Uchumi na Biashara amesema kuwa hadi mwishoni mwa mwaka uliopita, Watanzania 5,000 wako nchini China wakipatiwa mafunzo mbalimbali kupitia Wizara ya Biashara ya nchi hiyo kwenye vyuo mbalimbali.
Alisema kuwa wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma nchini China wameiletea sifa kubwa Tanzania kutokana na umahili wao mkubwa katika masomo pamoja na nidhamu ya hali ya juu jambo linalowafanya wawe mabalozi wazuri wa nchi yao ndani na nje ya nchi kwa ujumla.
Akifungua mafunzo hayo ya majuma mawili, Naibu Kamishna wa Maboresho ya vihatarishi hatari, kutoka Idara ya Forodha ya Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. James Mbunda, amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wafanyakazi wa idara hiyo wa kukabiliana na vihatarishi vyote vya masuala ya forodha kwa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini kwenda nje ya nchi.
Amesema kuwa mafunzo hayo yameratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya Utumishi ikiwa ni hatua ya Serikali ya kuboresha utendaji kazi wa idara hiyo kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Ameyataja baadhi ya masuala watakayopewa utaalamu na wakufunzi watano kutoka Chuo hicho cha Forodha cha Shangai wakiongozwa na Profesa wa masuala ya forodha Bi. Sun Hao, ni pamoja na kupitia sheria mbalimbali za forodha, misamaha ya kodi, udhibiti wa biashara, namna ya kukabiliana na watu wasio tii sheria na vigezo vya utoaji leseni.
No comments:
Post a Comment