Thursday, July 20, 2017

ELIMU SAHIHI ITUMIKE KWANZA KABLA YA MATUMIZI YA SHERIA KWA WAKEKETAJI

Elimu sahihi juu ya madhara ya ukeketaji ya muda mfupi na mrefu inatakiwa itolewe kwa jamii kabla ya kuwachukulia hatua baadhi yao wanaoendelea kufanya vitendo vya ukeketaji licha ya uwepo wa sheria kali.

Rai hiyo imetolewa mapema leo na Mratibu wa Mradi wa Kupinga Ukeketaji (WOWAP) Nasra Suleiman katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida, kwa ushirikiano wa Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida na mradi huo kwa ufadhili wa shirika la WAAF-Japan.

Mratibu huyo amesema nguvu ya sheria itasaidia kuondoa ukeketaji endapo wananchi wengi watakuwa na uelewa wa kutosha juu ya madhara ya ukeketaji na kuamua kwa hiyari kuachana na mila hiyo.

“Sheria isiwe nguvu pekee ya kupambana na ukeketaji, tukifanya hivyo itafikia kipindi tutakwama kwa kiasi kikubwa kwa kuwa watu wataendelea kukeketa kwa kificho ili wasikamatwe, lakini kila mwana jamii akiwa na elimu ya kutosha ya madhara hayo, nguvu ya sheria itatumika tu kwa wachache watao kaidi”, amesisitiza Nasra.

Ameongeza kuwa Watendaji wa kata na vijiji wana uwezo mkubwa wa kubadilisha mtazamo na mila ya ukeketaji kwa kuelimisha wananchi wao hasa baada ya semina zinazoandaliwa na miradi au mashirika Fulani kwakuwa zinawajengea uwezo ili waweze kutoa elimu sahihi na mbinu za kuelimisha.

Nasra amesisitiza kuwa jukumu la elimu lisiachwe kwa sekta binafsi kama mradi wake wa WOWAP pekee bali liwe jukumu la jamii nzima huku akifafanua kuwa elimu inayotakiwa kutolewa ni ile inayoelezea madhara ya ukeketaji na sio kuwakataza kwa kigezo cha kutii sheria pekee.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Msange Magni Oisso amesema katika kata hiyo ukeketaji umekufanyika kwa siri sana kwa kuogopa mkono wa sheria huku wahanga wakiwa watoto wachanga na wale waliomaliza kliniki.

Oisso amesema kumekuwa na usiri mkubwa huku wakeketaji wakibadili mbinu namna za kujificha wasigundulike kwa jamii ambayo elimu imeanza kuwafikia baadhi yao.

Aidha amependekeza kuwa ili kukomesha ukeketaji moja ya njia ni kutoa elimu katika vituo vya kutolea huduma za uzazi na mtoto ili mtoto aweze kunusurika pia elimu itolewe shuleni kwa ngazi zote kuanzia darasa la awali hadi la saba.

Akichangia mada katika semina hiyo mzee maarufu na mwenyeji wa Msange Bi Greta Musa Nyonyi amesema elimu ni bora zaidi kuliko kuwaogopesha wanajamii kwa kutumia sheria kwakuwa watatafuta namna ya kutekeleza azma yao kwa usiri ili kukwepa mkono wa sheria na sio kuacha.

Greta ameongeza kuwa kwa sasa kutokana na kuwa wakeketaji wamebainika kuwa wanakeketa watoto wachanga na hugundulika wakienda kliniki baadhi yao wanabadili mbinu na kusubiri mtoto amalize kliniki ndipo anakeketwa.

Naye Mzee wa Kimila Hosea Mnyambi amesema yeye amekulia katika familia ya wakeketaji na wamekuwa wakirithishwa mbinu za ukeketaji kizazi hadi kizazi ila kutokana na kuwepo kwa sheria, dini kuhubiri madhara ya ukeketaji, mila hiyo wameiacha.

Amesema wachache wanaoendelea kufanya vitendo hivy o ha wanawake wamekuwa wakifanya kwa usiri mkubwa huku akina baba wakiwa hawana taarifa ya kinachoendelea na endapo mtoto anafariki hudanganywa ugonjwa uliopelekea kifo cha mtoto.

Mzee Mnyambi amesema elimu iendelee kutolewa hasa kwa kutumia vyombo vinavyoaminika mfano vyama vya siasa, dini na vikundi vya kuweka na kukopa pamoja na kuiweka agenda ya ukeketaji kwa vikao vya Kata na vijiji.

Semina ya kupinga ukeketaji Kata ya Msange imefanywa na mradi wa WOWAP kwa ushirikiano wa maafisa ustawi wa jamii mkoa wa Singia kwa watendaji wa kata na vijiji, watoa huduma za afya, polisi, waalimu, wawakilishi wa viongozi wa dini, maafisa ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii, wazee maarufu na wa kimila ili wawe mabalozi wa kusambaza elimu hiyo kwa jamii inayo wazunguka.
 Mzee maarufu na mwenyeji wa Msange Bi Greta Musa Nyonyi akichangia hoja katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
 Mratibu wa Mradi wa Kupinga Ukeketaji (WOWAP) Nasra Suleiman akizungumza na washiriki wa semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
 Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Msange Magni Oisso akichangia hoja katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.
 Washiriki wa semina ya kupinga ukeketaji iliyoandaliwa na Mradi wa WOWAP wakifuatilia kwa umakini filamu fupi ya Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.

Mzee wa Kimila Hosea Mnyambi akichangia hoja katika semina ya kupinga Ukeketaji iliyofanyika katika Kata ya Msange Wilayani Singida.

No comments: