Thursday, June 1, 2017

WAZIRI SIMBACHAWENE AAGIZA WAHITIMU CHUO CHA SERIKALI ZA MITAA HOMBOLO WAPEWE KIPAUMBELE


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene 


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imeziagiza Halmashauri,Miji na Majiji nchini kutoa kipaumbele cha ajira kwa wahitimu wa chuo Kiongozi cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa(LGTI) ambao mafunzo wanayopata yanalenga kuongeza na kuleta ufanisi katika serikali za mitaa nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene amesema hivi karibuni kuwa Chuo Kiongozi cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa (Hombolo) kipo mahusiusi kwa ajiri ya kutoa mafunzo kwa ajili ya wafanyakazi wanaoajiliwa kwenye serikali za mitaaa nchini.

“Naagiza kunapokuwa na nafasi za kazi kwenye halmashauri, miji na hata majiji ni vyema wahitimu wa chuo hiki wakapewa kipaumbele. Ni vizuri wakapata nafasi ya kushindanishwa na wengine kwani hawa ni walengwa,” alisema Waziri Simbachawene wakati alipokutana na viongozi na wawakilishi wa chuo hicho mjini Dodoma.

Bila kumung’unya maneno, Waziri Simbachawene alisema wahitimu kutoka chuo Kiongozi cha Serikali za Mitaa ndiyo wabobezi kwenye taaluma za serikali za mitaa na hivyo kuwa kwenye nafasi nzuri ya kuleta ufanisi zaidi.

“Ni vizuri tukakumbuka kuwa chuo hiki kilianzishwa na serikali kwa lengo la kuwaandaa wafanyakazi wa kada zote katika serikali za mitaaa,” alisema na kuongeza kuwa serikali itaendelea kukijengea uwezo chuo hicho ili kiweze kutoa wahitimu bora.

Waziri Simbachawene aliuagiza uongozi wa chuo hicho kutosita kutoa taarifa yeyeto endapo chuo kinapokuwa na upungufu wa watumishi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Martin Madale alimshukuru Waziri Simbachawene kwa kuwa karibu na chuo na pia kufuatilia maendeleo na ustawi.

“Kwa niaba ya Bodi, Menejimenti, Wafanyakazi na wanachuo wote wana imani kubwa na uongozi wako kwani umekuwa karibu sana nasi na pia umekuwa msaada mkubwa katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazokikabili chuo,” alisema Dkt. Madale.

Alimwomba waziri kukisaidia chuo kupata kompyuta zaidi, viti na vifaa mbalimbali ilikukabiliana na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaoomba kujiunga na chuo hicho kwa sasa.

Naye Rais wa Serikali ya wanachuo, Bw. Kelvin Mbuta alimwomba waziri kusaidia kufikisha ombi la wanachuo serikalini kuhusu mikopo kama wanachuo wa vyuo vingine wanavyopata.

“Nipo hapa kwa niaba ya wanachuo ambao wameniagiza kilio chao kuhusu mikopo. Tunakuomba Mheshimiwa waziri utusaidie tupate mikopo kwaajili ya kujikimu kwani kuna wachuo wengi wanetoka kwenye familia maskini sana,” alisema.

Chuo Kiongozi cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa maarufu kama Chuo cha Hombolo kina wanachuo zaidi ya 3,000 ambao wapo katika Kampasi Kuu ya Hombolo ambayo ipo pembeni kidogo mwa Mji wa Dodoma na ile Kampasi ya Mjini.

Chuo kinatoa programu sita za Stashahada (Diplomas) na program sita za Cheti(Certificates) katika Usimamizi wa Raslimali Watu (Human Resource Management), Serikali za Mitaa na Utawala(Local Government and Administration)Uhasibu na Usimamizi wa Fedha Serikali za Mitaa(Local Government Accounting and Finance),Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka(Records and Archive Management),Manunuzi (Procurement)na Maendeleo ya Jamii (Community Development).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. George Simbachawene akisalimiana na Rais wa Serikali ya Wanachuo Chuo Kiongozi cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa (Hombolo), Bw. Kelvin Mbuta hivi karibuni mjini Dodoma. Pembeni ni Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Martin Madale. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. George Simbachawene akizungumza na Uongoza na Wawakilishi wa Serikali ya Wanachuo ya Chuo Kiongozi cha Mafunzo ya Serikali za Mitaa (Hombolo)mjini Dodoma hivi karibuni.

No comments: