Thursday, June 1, 2017

HATI YA MASHTAKA KESI YA WEMA SEPETU NA MWENZAKE YABADILISHWA.

Na Karama Kinyuko.

⁠⁠⁠⁠⁠UPANDE wa mashtaka katika kesi ya dawa za kulevya inayomkabili msanii wa filamu Wema Sepetu na mwenzake umebadilisha hati ya mashtaka dhidi ya washtakiwa.

Hatua hiyo imekuja leo baada ya wakili wa Serikali Constatine Kakolaki kuomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuomba kufanya mabadiliko hati ya mashtaka kabla ya kuwasomea maelezo ya awali.

Mapema Mwezi uliopita mahakama hiyo iliambiwa kuwa upelelezi wa kesi umekamilika na Leo ilikuwa inakuja kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali (PH).

Wema na wafanyakazi wake Angelina Msigwa na Matrida Abas wamesomewa mashtaka mapya mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambaye alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka.

Katika mashtaka hayo mapya, washtakiwa wanakabiliwa na mashitaka mawili la kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa za kulevya.

Akiwasomea mashyaka hayo amedai, February 4, mwaka huu katika makazi yao Kunduchi Ununio, washtakiwa walitenda kowa.Imedaiwa kuw siku hiyo washtakiwa wote walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.

Aidha katika shtaka la pili linalomkabili Wema peke yake imedaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na 3, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, Wema alitumia dawa za kulevya aina ya bangi.

Washitakiwa hao wanaotetewa na Wakili Peter Kibatala wamekana mashitaka, ambapo walisomewa maelezo ya akimu awali.

Akisoma maelezo hayo, Kakula amedai Wema alikuwa miongoni mwa watu waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, wakituhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.

Amedai kuwa Februari 3, mwaka huu, alijipeleka kituo cha polisi cha kati ambako alikamatwa na Februari 4, ukaguzi ukafanyika nyumbani kwake ambapo kulipatikana vitu vinavyodhaniwa dawa za kulevya.

Kakula ameongeza kudai ukaguzi huo ulifanyika mbele ya Wema, polisi na shahidi huru na Februari 6,vitu hivyo vilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na Februari 8 mkemia alitoa taarifa ya uthibitisho juu ya vielelezo hivyo kuwa ni bangi yenye uzito wa gramu 1.08.

Ameongeza kuwa, Februari 8, Wema alipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupimwa mkojo, ambapo uchunguzi ulieleza mkojo wa msanii huyo ulikuwa na bangi.

Baada ya kusomewa maelezo hayo ya awali, Wema alikubali majina yake, mahali anapoishi na kwamba alikuwa miongoni mwa waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kujihusisha na dawa za kulevya.

Alikubali pia kujipeleka polisi huku akikana maelezo mengine. Washitakiwa wengine walikubali majina yao na kuwa wafanyakazi wa Wema tu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 14, Mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

No comments: