Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeridhia ombi la upande wa mashtaka la kutaka ushahidi utakaotolewa na askari polisi kutoka Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kitengo cha kupambana na Ujangili,D 7847 Sajenti Beatus usikilizwe kwa usiri.
Ushahidi huo ni katika kesi ya uhujumu uchumi kwa kujihusisha na Meno ya Tembo ya bilioni 13 inayomkabili raia wa China anayedaiwa kuwa Malkia wa Pembe za Ndovu, Yang Feng Glan (66)na watanzania wawili.
Mapema wakili wa Serikali Paul Kadushi, aliiomba Mahakama hiyo ushahidi wa askari huyo ambaye awali alikwishaanza kutoa ushahidi wake kwa uwazi, usikilizwe kwa usiri kwa sababu unahusisha masuala ya amani ndani ya nchi.
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alikubaliana na ombi hilo la upande wa mashtaka kusikilizwa kwa usiri.
Hata hivyo, mmoja wa mawakili wa utetezi, wa Masumbuko Lamwai alilipinga hilo na kudai kuwa hakuna mahusiano juu ya Pembe za Ndovu na amani ya nchi.
Alidai kuwa, upande wa mashtaka hawakueleza ni kwa namna gani ushahidi wa Pembe za Ndovu utaingiliana na amani na utulivu katika nchi hii.
Aliongeza kuwa, mtu yoyote anayetuhumiwa kutenda kosa ni haki yake kikatiba,kesi isikilizwe hadharani ili kuhakikisha Haki ionekane imetendeka na umma ujue.
Aliongeza kuwa kufanya hivyo kunaleta uwezekano wa mtu kuleta ushahidi wa kubambika.
Alibainisha kuwa upande wa mashtaka haujaweza kutoa sababu kwa nini ushahidi wa shahidi huyo uendelee kusikilizwa kwa usiri wakati ndugu wana Haki ya kujua hii kesi inaendeleaje.
" Kesi imekuwa kijamii mno, halafu isikilizwe kwa usiri kama mahakama ya kijeshi siyo Haki, mteja wangu amepewa Umalkia wa Pembe za Ndovu huo umalkia uthibitishwe hadharani siyo kisiri siri tunaomba hilo ombi likataliwe." Aliomba Lamwai.
Kadushi akijibu hoja za Lamwai alidai kuhusiana na hoja ya upande wa mashtaka kutoeleza sababu ni rai yetu kama Jamuhuri itakuwa haina maana tukisema sababu.
Akitoa uamuzi wake baada ua kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Shaidi amesema upande wa mashtaka haulazimishwi kueleza kile ambacho wanafikiria, sababu Mawakili wa washtakiwa wapo,Lamwai na Nehemiah Nkoko tutajua kwa mini usikilizwaji wa usiri ufanyike, isikilizwe kwa usiri.
Baada ya uamuzi huo, watu wote walitolewa nje na kubakia Mawakili wa Serikali, washtakiwa na Mawakili wao.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kwa usiri Juni 9, 2017.
Manase, raia wa China anayedaiwa kuwa Malkia wa Pembe za Ndovu, Yang Feng Glan (66) na Salvius Matembo wanakabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na biashara ya nyara za serikali kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22,2014 zenye thamani ya Sh 13 bilioni .
wanadaiwa kufanya biashara ya vipande 706 vya meno ya Tembo vyenye uzito wa kilogramu 1889 zenye thamani ya Sh 5.4 bilioni bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na Mkurugenzi wa Wanyama Pori.
Kwa upande wa Salvius na Manase wanadaiwa kuongoza makosa ya uhujumu uchumi kwa kusaidia biashara ya nyara za serikali kwa kukusanya, Kusafirisha na Kuuza Meno ya Tembo kwa nia ya kujipatia faida.
Ilidai kuwa Mei 21, 2014 katika eneo la Sinza Palestina wilaya ya Kinondoni mshtakiwa Manase alitoroka chini ya ulinzi halali wa askari wa Jeshi la Polisi D 7847 Koplo Beatus ambaye alikuwa akimshikilia kwa makosa ya kujihusisha na biashara za nyara za serikali.
No comments:
Post a Comment