Monday, June 19, 2017

TFDA YAZINDUA MKATABA WA HUDUMA KWA WATEJA

Frank Mvungi-Maelezo 

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imezindua mkataba wa huduma kwa wateja ikiwa ni nyenzo mojawapo inayowezesha kutolewa kwa huduma bora katika kiwango cha kimataifa na kutekelezwa kwa vitendo juhudi za Serikali katika kuwahudumia wananchi kwa weledi na uwajibikaji.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Tiba Dkt. Doroth Gwajima wakati akizindua mkataba wa huduma kwa wateja wa Mamlaka hiyo leo Jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.

Akizungumza kuhusu mkataba huo Dkt. Gwajima amesema kuwa ni jambo la faraja kuona kwamba uzinduzi wa mkataba huu unafanyika katika kipindi cha maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma mwaka 2017 ambayo msingi wake ni kutoa huduma bora zinazoridhisha wateja kwa kuzingatia mkataba shirikishi wa huduma kwa wateja.

“Nawapongeza TFDA kwani kwa kutekeleza mkataba huu,watumishi wataweza kuepuka uzembe,upendeleo, na rushwa mambo ambayo husababisha malalamiko kwa wananchi dhidi ya watumishi na Serikali yao” Alisisitiza Gwajima.

Akifafanua amesema mkataba huo utawezesha wateja kutambua haki zao, wajibu wao hali itakayosaidia TFDA kuweka mfumo dhabiti wa upimaji wa viwango vya huduma (service standards) kwa mujibu wa mkataba ili kubaini ufanisi wa mkataba huu na kuchukua hatua stahiki za uboreshaji wa huduma pale inapobidi.

Aidha, alipongeza TFDA kwa kuweka namba ya simu ambayo mteja anapiga bure wakati wa kazi, kuhusiana na huduma zinazotolewa na TFDA ambayo ni 0800110084 na kuitumia inavyostaili.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Hiiti Sillo amesema utaratibu wa kuwa na mkataba wa huduma kwa wateja umesaidia kuongeza tija ambapo kwa sasa huduma za usajili wa maneno ya biashara za bidhaa zinazodhibitiwa na TFDA awali zilitolewa ndani ya siku 45 mwaka 2006 na kufikia 2016 zinatolewa ndani ya siku 10 tu.

Utoaji wa vibali vya kuingiza na kusafirisha bidhaa nchini na nje ya nchi (Bidhaa zilizosajiliwa) mwaka 2006 zilitolewa ndani ya siku 5 na sasa ni siku  moja tu, wakati usajili wa dawa zinazozalishwa nchini awali ulikuwa unafanyika ndani ya siku 360 na sasa ni siku 120 tu.

Mkataba wa huduma kwa wateja uliozinduliwa unaonesha ahadi za TFDA katika kuhudumia wateja wake na pia wajibu wa wateja katika kuwezesha Mamlaka kuwahudumia kwa ufanisi bila kuathiri ubora,Usalama na ufanisi wa chakula,dawa,vipodozi,vifaa,tiba na vitendanishi.

Kwa mara ya kwanza,TFDA ilitayarisha mkataba wa huduma kwa wateja kwa kushirikiana na wadau wake mwaka 2006 na baadaye kurejewa mwaka 2012,marejeo ya mara kwa mara yanatokana na msukumo wa mabadiliko ya kijamii,maboresho ya mifumo ya utendaji,kuongezeka kwa rasilimali watu na ukuaji wa sayansi na teknolojia katika utoaji huduma. 
 Kaimu Mkurugenzi wa Tiba toka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto Dkt. Doroth Gwajima akisisitiza umuhimu wa Mamlaka ya Chakula na dawa (TFDA) kuendelea kusimamia utoaji wa huduma zake katika viwango vya Kimataifa wakati akizindua mkataba wa huduma kwa wateja wa Mamlaka hiyo leo Jijini  Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA ) Bw. Hiiti Sillo akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkataba wa huduma kwa wateja uliofanyika Leo Jijini Dar es Salaam.
 Kaimu Mkurugenzi wa Tiba toka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto Dkt. Doroth Gwajima (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi mkataba wa huduma kwa wateja wa Mamlaka hiyo leo Jijini  Dar es Salaam  kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
 Kaimu Mkurugenzi wa Tiba toka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto Dkt. Doroth Gwajima (katikati) akionesha mkataba wa huduma kwa wateja wa TFDA mara baada ya kuuzindua leo Jijini Dar es Salaam.kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA ) Bw. Hiiti Sillo na kushoto Mkurugenzi wa Idara ya Uchambuzi na Usahuri wa kazi toka Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Bw. Mick Kiliba. 
 . Kaimu Mkurugenzi wa Tiba toka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto Dkt. Doroth Gwajima akikata utepe kuzindua namba maalum itakayotumiwa na wananchi kuwasilina na Mamlaka hiyo ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa mkataba wa huduma kwa wateja.
 Kaimu Mkurugenzi wa Tiba toka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto Dkt. Doroth Gwajima (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa TFDA mara baada ya kuzindua mkataba wa huduma kwa wateja wa Mamlaka hiyo. 
Mkurugenzi wa Idara ya Uchambuzi na Usahuri wa kazi toka Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Bw. Mick Kiliba akipongeza TFDA kwa kuwa moja ya Taasi za Serikali inayotoa huduma zake kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu wakati wa uzinduzi wa mkataba wa huduma kwa wateja.

(Picha zote na Frank Mvungi –Maelezo).

No comments: