Monday, June 5, 2017

‘STACA’ MRADI WA WENYE MAFANIKIO LUKUKI MAHAKAMA MKOANI MTWARA

Na Nurdin Ndimbe

Kwa miaka ya hivi karibuni Mkoa wa Mtawara umekuwa na maendeleo makubwa ya Kichumi na ya Kisiasa. Kutokana na mabadiliko hayo maendeleo ya Mkoa wa Mtwara yameongeza ari na matumaini mapya ya maisha bora kwa wananchi wa Mkoa huo. 

Mtwara ya sasa ni yenye fursa lukuki kutokana na miradi mbalimbali ya maendeleo yaliyotokana na uchimbaji wa gesi asilia, maendeleo ya uboreshaji wa miundombinu na ongezeko na mapato katika zao la korosho.

Maendeleo haya yameikumba Sekta mbalimbali Mkoani humo ikiwemo ya Sekta ya Sheria hususani Mahakama. Mahakama ya Tanzania kanda ya Mtawara yenye watumishi 218 ilianza kutekeleza Mradi wa Mapambano dhidi Rushwa (Strengthening Tanzania Anti-Corruption Action ) kwa kifupi STACA Mwaka 2011/2012 chini ya ufadhili wa Uingereza kupitia Shirika lake la misaada la Kimataifa la DFID. 

Lengo kuu la mradi huu ilikuwa ni kuzuia na kupambana na rushwa mahala pa kazi, Katika Mkoa wa Mtwara mradi huu ulihusisha Wilaya zote tano za Tandahimba, Masasi, Newala, Mtwara na Nanyumbu. Mradi huu ulijikita katika ugawaji wa vitendea kazi kama kompyuta na ‘printer’ zake, mafaili ya kufungulia mashauri (case files), makabati ya kutunzia mafaili na kumbukumbu, pikipiki kwa watumishi wa Mahakama pamoja na baiskeli kwa ajili ya kusambazia ‘Summons.’

Hata hivyo, Mradi pia ulichapisha na kugawa vibonzo mbalimbali vyenye matangazo dhidi ya vitendo vya rushwa Mahakamani na ugawaji wa simu za mkononi kwa ajili ya kupokea malalamiko kwa wakuu wa Wilaya, Mikoa, Mahakama pamoja na wadau. “Tulifanya tathmini kimkoa na kuzumgumza na wahusika wenyewe yaani watumishi, imeonekana tumefanya vizuri sana’’ alisema Mtendaji wa Mahakama Mkoani Mtwara Bw. Selestine Onditi. 

Alieleza kuwa, kwa ripoti waliyonayo kwa upande wa rushwa hakuna malalamiko yaliyopokelewa yaliyohusu rushwa moja kwa moja. “Kwa maana hiyo, mradi wa STACA umefanya kazi kubwa” alisisitiza Mtendaji huyo wa Mahakama Mkoani Mtwara. Tathmini ya taarifa ya simu za mkononi zilizogawiwa kwa Watendaji mbalimbali Mkoani Mtwara na Mahakama kwa ujumla inaeleza kuwa hakuna lalamiko lolote lililohusu rushwa bali kulikuwa na malalamiko mengine kama ya ucheleweshwaji wa mashauri pamoja na nakala za hukumu. 

Alieleza kuwa, mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia mradi huu ni pamoja na mahakama za mwanzo kuwa ndio waliofaidika kwa kiasi kikubwa kutokana na mradi huu, kasi ya usikilizwaji wa mashauri katika Mahakama za Mwanzo uliongezeka kwa 90%, kasi ya utoaji wa nakala ya hukumu imeongezeka sana karibu 96%, huku hatuchelewi hukumu zinatolewa kwa muda ’’ alisisitiza Mtendaji huyo.

Makabati ya kutunzia mafaili ya kesi (case files) imesaidia katika utunzaji wa kumbukumbu, kabla ya hapo ilikuwa kupata faili lazima ukutane na mafaili yenye vumbi ndio lianze kushughulikiwa hii ilisababisha kuleta viashiria vya Rushwa kwa wateja waliokuwa wanapata huduma katika Mahakama zetu. Hali ilikuwa mbaya sana Mahakama nyingi hasa za mwanzo ndizo zilikuwa na matatizo ya utunzaji wa kumbukumbu.

Mafanikio mengine ya mradi huu ni pamoja na kuongeza ari na mazingira bora ya kufanyia kazi kwa watumishi wa mahakama. Baadhi ya watumishi wa Mahakama kupewa vifaa vya maofisini ,baiskeli na pikipiki. Hii imeongeza ari ya kufanya kazi zaidi kwa watumishi wa Mahakama. 

Baiskeli zinatumiwa kusambaza barua za wito wa kuhudhuria Mahakama (Summons), pikipiki zina tumiwa na Mahakamimu kwenda na kurudi kazini pamoja na kuhudhuria vikao vya na Mahakama zinazotembelewa. Hii imeleta ujasiri wa kazi,kujituma kwa watumiishi lakini kikubwa zaidi imeleta utandawazi (transparency) katika shughuli za Mahakama ambapo kwa sasa shughulizo zote za Mahakama hakuna siri tena. 

Mabango ya matangazo ya mapambano dhidi ya rushwa yamebandikwa katika ofisi mbalimbali za Serikali ikiwemo ofisi wa Mkuu wa Mkoa,Wakuu wa Wilaya, TAKUKURU ,Mahakama, pamoja na sehemu zenye mkusanyiko wa watu wengi. Kimsingi, sasa wananchi walio wengi wanaimini Mahakama kama mkombozi wa haki zao na ndio tegemeo pekee la kukimbilia wakiwa na shida. 

Kwa mantiki hiyo, hali ya wananchi kuikubali Mahakama imeongezeka kufikia 80% ukilinganisha 50% ilivyokuwa huku nyuma. “Haya ni mafanikio makubwa ambayo hayajawahi kutokea katika historia ya Mkoa wa Mtwara’’ Alieleza Bw. Onditi. Kwa mafanikio haya ya mradi wa STACA yametokana kwa pamoja na kutekeleza Mpango Makakati Mahakama wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania baada ya kufanya mafunzo katika ngazi mabalimbali katika mkoa wa Mtwara. 

Mafunzo yalisaidia kwa kila mtumishi wa Mahakama kutekeleza majukumu yake. Kwa shapa mtawara kila tunapokuwa na mikutano au mafunazo yoyote huwa taunaanza na dozi ya Mpango Mkakati kwanza. ‘’ Hii ndio siri ya mafanikio katika kutekeleza shughuli za Mahakama Mkoani Mtwara

Hata hivyo, pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Mradi wa kupambana na Rushwa Mkoani Mtwara pamoja na kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama wa miaka mitano kuna baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa mradi STACA kwa baadhi wa wadau kuomba mradi huu kuwa endelevu kwani kwa sasa mradi umemaliza muda wake, Mabango yamesaidia sana kupunguza masuala ya Rushwa, kwa tathmini ya Mkoa walipata mabango karibu 200 lakini hayakutosha kusambazwa katika taasisi zote Mkoani humo wakiwamo wadau wa Mahakama. Kuhusu matumizi ya simu kwa ajili ya kutuma taarifa (sms) kwa watumiaji wa kawaida, changamoto kubwa ilijitokeza ni kwa watu wengi kutopenda kutuma ujumbe mfupi na wengi wapependa simu zitumike kwa kupiga na kuzungumza moja kwa moja.Sababu nyingine ni kwa baadhi ya wananchi kutojua kusoma na kuandika, hivyo kutoweza kutumia namba za malalamiko kwa ajili ya kutuma malalamiko yao.

Changamoto nyingine ya ujumla kwa mkoa wa Mtwara ni uchakavu wa majengo hasa katika Mahakama za Mwanzo na hataka hata jengo la Mahakama Kuu kanda ya Mtwara ndio liko katika hatua ya mwisho ya kumalizia ukarabati.Hata hivyo hatua za awali kwa ajili ya kujenga jengo jipya la Mahakama Kuu kanda ya Mtwara inaendelea. 

Ni mategemeo ya watumishi wa Mahakama pamoja na wadau kuwa, Mahakama Tanzania itendeleza mradi wa STACA Chini ya ufadhili wa shirika la DFID la Uingereza ili uendane sambamba na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama unaotekelezwa kwa pamoja na Washirika wa maendeleo kama Benki ya Dunia.Pamoja na mambo hayo yote Mahakama ya kanda ya Mtwara inaendelea vizuri na kazi yake ya kutoa haki kwa wakati na kujenga imani imara kwa wananchi, kama chombo muhimu cha utoaji haki Mkoani humo. 

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa STACA-Mahakama ya Tanzania, Bi. Wanyenda Kutta anasema Mradi huo umefanikiwa kwa asilimia 100 akieleza kuwa kazi ambazo zilipangwa kutekelezwa chini ya mradi zilitekelezeka kwa asilimia 100 na kama kuna mapungufu ni kutokana na Jiografia ya Mkoa mmoja hadi mwingine.

Baadhi ya pikipiki zilizotolewa chini ya Mradi wa STACA, pikipiki hizi na baadhi ya vifaa vingine tajwa ni miongoni mwa vitendea kazi vilivyotolewa kurahisisha utoaji huduma ya haki.
Muonekano wa picha ya bango lenye ujumbe wa kuzuia na kupambana na Vitendo vya Rushwa ikiwa imebandikwa katika jengo la Mahakama Kuu-Kanda ya Mtwara. Bango hili ni kati ya Mabango mengi ambayo yamebandikwa katika majengo ya Mahakama nchini lengo likiwa ni kuzuia rushwa na vitendo vitendo vyenye ukosefu wa maadili.

No comments: