Monday, June 5, 2017

SERIKALI YAIPATIA TADB RUZUKU YA SHILINGI BILIONI 209.5 KUENDELEZA SEKTA YA KILIMO NA MIFUGO



td1
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu akisaini mkataba wa kuipatia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) fedha za kuiongezea mtaji kiasi cha shilingi bilioni 209.5. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bw. Francis Assenga, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam
td2
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sheria kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Eligius Mwankenja (kushoto), na Mchumi kutoka Wizara hiyo  Bw. Said Nyenge (kulia) wakiwaelekeza Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Bw. Francis Assenga, maeneo maalumu ya kutiwa saini kwenye Mkataba wenye thamani ya Sh. 209.5 bilioni utakaoiwezesha Benki hiyo kutoa mikopo ya muda wa kati na mrefu kwa riba nafuu kwa wakulima wadogo wadogo, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam
td3
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto) akibadilishana mkataba na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania-TADB, Bw. Francis Assenga mara baana ya kusainiwa mkataba wa kuiongezea mtaji Benki hiyo wenye thamani ya Sh. Bilioni 209.5 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2021, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
td4
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu wakionesha mkataba waliokwisha usaini kwa waandishi wa habari (hawamo pichani) na kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam
td5
Wajumbe waliohudhuria hafla ya utiaji saini mkataba wa kuiongezea mtaji Benki ya Kilimo wenye lengo la kuunganisha maboresho ya sekta ya kilimo na mpango wa mageuzi ya viwanda wenye thamani ya Sh. 209.5 bilioni, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
td6
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (kushoto) akitoa ufafanuzi wa maswali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawamo pichani) na kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania-TADB, Bw. Francis Assenga, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam
td7
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania-TADB, Bw. Francis Assenga (kulia) akiongea na waandishi wa habari pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo (hawamo pichani).
td8
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania-TADB, Bw. Francis Assenga (kulia) akiongea na waandishi wa habari pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo (hawamo pichani).
td9
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania-TADB, Bw. Francis Assenga (kulia) akiongea na waandishi wa habari pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo (hawamo pichani).
td10
Wajumbe wa Bodi wakifuatilia kwa makini zoezi la utiaji saini mkataba wa Serikali kuipatia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) shilingi bilioni 209.5. kwa ajili ya kuiongezea mtaji. Kutoka kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya TADB Bw. William Mhoja, Mkurugenzi wa Fedha na TEHAMA – TADB Bw. Severin Ndaskoi, Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji Fedha Bw. Albert Ngusaru, Mkuu wa Idara ya Utimilifu-TADB, Bw. Adam Kamanda, Mkaguzi wa Ndani Mkuu Bi, Joyce Maduhu, na Mkurugenzi wa Mikopo wa TSDB, Bw. Augustino Matutu.
…………………………………………………………………………
Benny Mwaipaja, WFM- Dar es Salaam
SERIKALI imeipatia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), shilingi 209.5 bilioni kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Kilimo na Mifugo hapa nchini, leo, Jijini Dar es salaam.
Akiongea kwa niaba ya Serikali wakati wa tukio la utiaji saini mkataba wa makabidhiano ya fedha hizo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, alisema kuwa kiasi hicho cha fedha ambacho ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ni sehemu ya shilingi 800 bilioni ambazo Serikali inatarajia kuipatia Benki hiyo ili iweze kukuza mtaji wake.
“Ninaishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB kwa kuipatia Serikali mkopo wa Dola za Marekani 93.5 milioni ambazo ni sawa na kiasi hicho cha fedha cha Sh. 209.5 bilioni kwa ajili ya kuiongezea mtaji TADB ili iweze kuwafikia wakulima wengi zaidi kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu” alisema Dkt. Kazungu.
Alisema kuwa fedha hizo zitasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya sekta ya kilimo na mifugo ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo ili sekta hiyo iweze kuchangia zaidi katika ukuaji wa pato la Taifa kuliko ilivyo sasa.
“Mwaka jana kilimo ambacho kinategemewa na idadi kubwa ya Watanzania kilichangia wastani wa asilimia 29.1 ya Pato la Taifa lakini tunataka kupitia Benki hiyo Sekta ya kilimo iiwezeshe nchi kukua kiuchumi kwa zaidi ya asilimia 7 hadi 10 katika kipindi kifupi kijacho” aliongeza Dkt. Kazungu.
Akiongea baada ya kutia saini makubaliano ya kupokea fedha hizo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB), Bw. Francis Assenga, ameishukuru Serikali kwa kuiongezea Benki yake mtaji utakaotumika kuendeleza Sekta ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ufugaji nyuki.
Alisema kuwa kiasi hicho cha fedha kitaiwezesha Benki hiyo ambayo imekwisha wafikia wakulima zaidi ya 3,700 hapa nchini, kuanza kutoa mikopo ya muda mrefu kwa wakulima wadogo na wa kati ili kuinua Sekta hiyo kwa kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yatokanayo na kilimo na mifugo.
Ameihakikishia Serikali kwamba Benki yake itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa matunda ya fedha hizo yanaonekana na kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Ras Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwakwamua wananchi wake katika lindi la umasikini.
“Riba za Mikopo ya Benki yetu ziko chini ikilinganishwa na Benki nyingine ambapo sisi tunatoza asilimia 8 hadi 12 kwa wakulima wadogo na asilimia 15 kwa wakulima wa kati wenye viwanda wakati viwango vya riba katika soko ni asilimia 18 na wakati mwingine vinafika hadi asilimia 40.” alisema Bw. Assenga wakati akijibu maswali ya wanahabari.

No comments: