Sunday, June 18, 2017

OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAHIMIZA USHIRIKIANO NA WADAU


Katika kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma,  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa  Serikali  leo  ( Juni 16) imekutana   na wadau mbalimbali  mkoani Tabora kwa  madhumuni ya  kujadiliana na kubadilishana mawazo yenye lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali za kiutendaji.   
Akitoa maelezo ya awali mbele ya wadau hao kutoka taasisi za serikali   zinazofanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Mdemu  pamoja na mambo mengine amesisitiza haja na umuhimu kwa wadau hao  pamoja na Ofisi yake kufanya kazi  kwa ushirikiano wa karibu ili kuiwezesha serikali  kutekeleza majukumu yake kwa  ukamilifu.
“ Nyinyi ni  wadau wetu muhimu sana sana,  ni kwa sababu hiyo, katika wiki hii ya maadhimisho ya  Utumishi wa Umma  tukaamua kuja Mkoani Tabora ili tukutane nanyi. Ni tumie basi, kikao hiki cha kazi kusisitiza kwenu,  haja na umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano na ukaribu ili kwa pamoja tuisaidie na kuiwezesha  Serikali itekeleze  majukumu yake kwa ukamilifu”. Akasema Naibu Mwanasheria Mkuu.
Akaongeza kwamba, ni kwa kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu licha ya kwamba kutaisaidia serikali lakini  kubwa zaidi kutapuguza lawama na kunyosheana vidole.
“ Ni vema tutambue kuwa hakuna Taasisi ambayo inaweza kutekeleza majukumu yake  pasipo kushirikiana na  Taasisi nyingine. Lakini  hili halilengi  au haina maana ya  kuingilia majukumu ya  Taasisi au Mihimili mingine  bali ni katika kutekeleza  misingi na maadili ya utumishi wa umma” akabainisha  Bw. Mdemu.
Wadau waliohudhuria majadiliano hayo  ni kutoka Jeshi la Polisi, Mahakama, Magereza,  Takukuru,  Halmashauri, Wakala wa Barabara,  na Idara ya Misitu na  jamii.
Akifafanua  ziaidi hoja hiyo ya ushirikiano.  Naibu Mwanasheria Mkuu ambaye ameambata na Wakurugenzi kutoka Divisheni zinazounda Ofisi ya Mwanasheria Mkuu. Pia amewataka wadau hao kuelezea kwa   uwazi  ni ushauri wa aina gani na katika eneo  gani ambao wanauomba kutoka Ofisi ya Mwanasheria mkuu.
“Pale mnapoleta mikataba yenu  katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa ushauri au maoni, ni muhimu sana mkaweka wazi  katika barua zenu ni maeneo gani  gani ya mkataba mnayotaka ushauri au maoni, na kwa sababu gani.  Badala ya kuleta  maelezo ya mstari mmoja  kwamba mnataka ushauri”.
Kasisitiza “ Jukumu letu  kuu na la msingi na ambalo limeainishwa katika Katiba ni    kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali na  wadau wengine. Lakini  ili ushauri huo uweze kutolewa kwa ukamili,utaalamu na kwa mujibu wa sheria  inayosimamia  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu .  Hivyo ni lazima basi wadau wetu  wawe tayari kutoa ushirikiano kwa kuweka wazi  maeneo wanayotaka kushauriwa. Tukifanya hivi tutakuwa tunaisaidia sana   Serikali”.
Wakati  huo huo Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewashukuru wadau hao  kwa kutenga muda wao na kuitikia wito wa  kukutana  na kubadilishana na mawazo ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu.
Kwa upande wao wadau hao  wameishukuru  Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kwa  kuamua safari hii kukutana na wadau wa Mkoa wa Tabora na kwamba   mikutano  ya aina hiyo ni muhimu sana katika uboreshaji wa uhusiano, ushirikiano na utetekelezaji wa majukumu ya kila taasisi.
Wadau hao pamoja na kutoka maoni yao na michango yao pia wameipongeza Ofisi ya Mwanasheria  Mkuu wa Serikali  kwa namna ambavyo imekuwa ikitekeleza majukumu yake ya utoaji wa ushauri  kwa wakati.

Katika maadhimisho ya mwaka jana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  ilikutana na  wadau wa Mkoa wa Dar Es Salaam. 

No comments: