Wednesday, May 24, 2017

Waziri Mahiga Aongoza Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa SADC nchini Lesotho

Dr. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrioka Mashariki na Mkuu wa Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa SADC akizungumza na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Lesotho, Mhe. Jaji Mstaafu Lesao Lehohla (wa pili kutoka kulia) alipotembelea tume hiyo mjini Maseru Lesotho kabla ya kuzindua rasmi Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya SADC. 
Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na Mkuu wa Umoja wa Makanisa wa Lesotho Archbishopp Gerald Tlali Lerotholi na ujumbe wake alipotembelea ujumbe huo kusikiliza maoni yao kuhusu uchaguzi mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika tarehe 3 Juni 2017. 
Dkt. Mahiga na ujumbe wake wakikamilisha majumuisho ya mikutano mbalimbali waliyoifanyana na wadau . 
 Dkt Mahiga akiagana na wenyeji wake nje ya Tume Huru ya Uchaguzi. 



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, amezihimiza taasisi za Serikali na za dini nchini Lesotho kudumisha amani na usalama kwenye kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi mkuu nchini hapa ili kuwezesha Serikali itakayoingia madarakani kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa ajili ya wananchi wa Lesotho. 

Uchaguzi huo mkuu wa wabunge ambao ni wa tatu kufanyika ndani ya kipindi cha miaka mitano, unatarajiwa kufanyika tarehe 3 Juni 2017 ambapo vyama 26 kati ya 30 vilivyojiandikisha, vitashiriki kwenye kinyang’anyiro hicho cha kuchagua wawakilishi Bungeni. 

Kwa mujibu wa Katiba ya Falme ya Lesotho, kiongozi wa chama kitakachoshinda viti vingi zaidi vya ubunge kwenye uchaguzi huo ndiye atakayeapishwa kuwa Waziri Mkuu na Kiongozi wa Serikali, ambapo mkuu wa nchi na mtawala mkuu anaendelea kuwa Mfalme Letsie III. 

“Wakati umefika sasa kwa Jumuiya yetu ya SADC kushiriki kwenye uangalizi wa uchaguzi huu tukiwa na habari njema ya kurejesha matumaini kwa wananchi kuhusu mustakabali wa uongozi. Lakini pia tuwe na ujumbe mzito kwa Serikali ijayo ili iweze kufanya mageuzi ya kweli kwenye nyanja mbalimbali kwa manufaa ya wananchi” Mhe. Mahiga amehimiza kwa wajumbe wa timu ya waangalizi wa uchaguzi.

Tangu alipowasili nchini hapa tarehe 22 Mei 2017, Dkt. Mahiga na ujumbe wake wamekutana na wadau mbalimbali wakiwemo Tume Huru ya Uchaguzi ya Lesotho na Umoja ya Makanisa wa Lesotho kwa lengo la kupata maoni ya kina kabla ya kuzindua Timu ya Uangalizi ya SADC (SADC Elections Observersion Mission - SEOM) tarehe 25 Mei 2017. 

Mhe. Dkt. Mahiga anaongoza timu hii ya waangalizi wa uchaguzi ya SADC kwasababu kwa sasa Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC Organ).

Akiongoza mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa Lesotho Mhe. Mampono Khaketla, Mhe. Mahiga alipongeza jitihada za Serikali kuhakikisha kuwa usalama wa raia na amani vinatawala nchini humo wakati wa uchaguzi. Hata hivyo aliongeza kuwa yeye na ujumbe mzima wa asasi hiyo muhimu ya maamuzi ya SADC ipo Lesotho kwa mara ya tatu, kama waangalizi wa uchaguzi ambapo mara ya kwanza na ya pili ilikuwa uchaguzi wa mwaka 2012 na 2015. 

Alisema ni matarajio yake na ujumbe mzima kuwa uchaguzi wa mwaka huu utazaa matunda yatakayoleta matumaini kwa wananchi ya kuwa na Serikali imara itakoyoongoza na kusimamia mageuzi ya kweli. “Haya ni matumaini ya wananchi wa nchi hii, na mimi kama kiongozi wa SEOM nimekuja kuwahakikishia ndugu zangu, tutasimama pamoja nanyi, tutawasindikiza kwenye uchaguzi huu, kama misingi ya Jumuiya yetu inavyoelekeza lakini pia wananchi wanatarajia hayo”

Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi ya SADC imewasili nchini Lesotho tarehe 18 Mei, 2017 na inaundwa na nchi tisa ambazo ni wananchama wa Jumuiya hiyo. Wajumbe wapatao 41 watasambaa kwenye majimbo yote ya uchaguzi kama waangalizi na kutoa taarifa ya kina siku chache baada ya uchaguzi huo, kuhusu mwelekeo na mwenendo wa uchaguzi huo.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 

Maseru, Lesotho 23 Mei, 2017

No comments: