Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala” Mabodi” akitoa ufafanuzi wa mabadiliko ya Katiba ya CCM yaliyofanyika mwaka 2017, kwa washiriki wa mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo ili waweze kuzikabili changamoto za uchaguzi wa chama na jumuiya zake.
Mwasilishaji ambaye pia ni Afisa kutoka Makao Makuu ya CCM Dodoma, Nd.Alhaji Rajab Kundya akiwasilisha mada za Mabadiliko ya katiba ya CCM ya mwaka 2017, pamoja na maboresho ya kanuzi ya uchaguzi ya chama hicho.
Ni baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia kwa makini mada zinazowasilishwa wakiwemo makatibu, wenyeviti , wajumbe wa kamati za siasa za ngazi za matawi hadi majimbo kwa chama na jumuiya zake, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mkoa wa Mjini Amani Unguja.(PICHA NA AFISI KUU CCM ZANZIBAR).
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
WAFUASI wa CCM wameshauriwa kutowachagua baadhi ya wanachama wenye kashfa na tabia za usaliti kuwa viongozi wa ngazi mbali mbali zinazowaniwa ndani ya chama na jumuiya zake hicho kupitia uchaguzi unaoendelea hivi sasa.
Ushauri huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” katika mwendelezo wa mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo watendaji na viongozi wa majimbo ya Mkoa wa Magharibi Unguja, ili waelewe kwa kina Mabadiliko ya Katiba ya CCM na kanuni mbali mbali yaliyofanyika hivi karibuni mjini Dodoma.
Dkt. Mabodi alisema chama hicho ili kiendelee kuimarika ni lazima wanachama wake ambao ni waaminifu wafanye maamuzi magumu ya kuwaweka kando kwa njia ya Kidemokrasia baadhi ya wanachama wenye dalili na sifa za usaliti sambamba na kamati za maadili kuanzia ngazi za chini kuwafanyia vikao vya kikanuni kuwajadili na kuwapatia fursa za kujitetea endapo watakutwa na makosa wachukuliwe hatua kwa mujibu wa maelekezo ya Katiba na kanuzi za maadili.
Pia Dkt. Mabodi alieleza kwamba lengo la kuchukua maamuzi hayo sio kuwaonea watu hao bali ni kukisafisha chama ili kibaki na wanachama waadilifu watakaokilinda na kukipigania katika mazingira yoyote hasa wakati wa chaguzi za chama na dola pamoja na vipindi mbali mbali vya misukosuko ya kisiasa nchini.
“ Kama tunahitaji kufanya matengenezo ndani ya nyumba yetu ni lazima nyufa zilizomo zote tuzibomoe na kuanza kujenda upya awamu kwa awamu kwa nia ya kupata nyumba imara na ya kudumu, na uko ndiko tunakoelekea kwa sasa lazima tupate makada wa kweli wanaotamka dhana ya Mapinduzi daima pamoja na kuulinda muungano kwa vitendo na sio kauli pekee.”, alisema Dkt. Mabodi.
Akizungumzia mabadiliko ya Katiba ya CCM yaliyofanyika hivi karibuni, alisema yamelenga kuongeza ufanisi ndani ya chama hicho kwa kupunguza idadi za viongozi na vikao vilivyokuwa vikitumia fedha nyingi kwa uendeshaji wake na kubaki na mambo machache yatakayoongeza ufanisi kwa matumizi mazuri ya rasilimali za chama na kiutendaji.
Naibu Katibu Mkuu huyo aliwaagiza washiriki wa Mafunzo hayo kuwa mabalozi na walimu wa kuwaelekeza kwa ufasaha wanachama wa CCM ambao hawakupata fursa hiyo ili nao wajue lengo la mabadiliko.
Hata hivyo aliupongeza Mkoa huo kwa kazi nzuri walioyofanya katika Chaguzi za Dola za Octoba 2015 na Machi, 2016 kuwa zilizaa matunda ya kupatikana kwa Serikali ya Awamu ya Saba chini ya Uongozi wa Dkt. Shein pamoja na viongozi wengine wakiwemo Madiwani, Wawakilishi na Wabunge licha ya kuwepo kwa changamoto nyingi za kisiasa.
Aidha aliweka wazi kwamba suala la kuimarisha uchumi wa chama hicho kupitia miradi ya ndani ya chama kuanzia ngazi za matawi hadi taifac halina mbadala kwani linagusa moja kwa moja maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa.
Akijibu hoja za baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo mwasilishaji wa mada ya mabadiliko ya Katiba ya chama hicho, Alhaji Rajab Kundiya alieleza kwamba ndani ya maboresho ya kanuni ya uchaguzi haijamzui mfanyakazi wa umma kutowania nafasi yoyote ya uongozi ndani ya CCM, isipokuwa wafanyakazi wenyewe wana miongozo na taratibu zao za kiutumishi katika sehemu zao za kazi.
Sambamba na hayo alisema kupitia marekebisho ya kanuzi za uchaguzi na maadili zimeweka utaratibu mzuri utakaomaliza tabia za kupanga safu na rushwa ndani ya chama hivyo kutoa fursa kwa wapiga kura kumchangua kiongozi anayefaa na mwenye sifa zinazokubalika katika michakato ya kidemokrasia na kiuongozi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi, Nd. Yussuf Mohamed Yussuf alisema washiriki hao ni wadau wakubwa wa masuala ya chaguzi za chama na dola hivyo wanatakiwa kutumia mafunzo hayo kuongeza uzalendo, uaminifu na umakini zaidi katika uchaguzi huo
No comments:
Post a Comment