Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (wa pili kutoka kulia), akijibu maswali mbalimbali kutoka kwa wachimbaji wadogo wa madini wa eneo la Mererani, wakati wa mafunzo maalum kuhusu usalama migodini yaliyofanyika hivi karibuni. Wengine pichani (kutoka kulia) ni Mkaguzi Mkuu wa Migodi Tanzania, Mhandisi Ally Samaje, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma na Fundi Sanifu Migodi kutoka Ofisi ya Madini Dar es Salaam, Stanslaus Basheka.
Mkaguzi Mkuu wa Migodi Tanzania, Mhandisi Ally Samaje, akiwasilisha mada kuhusu Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira katika Migodi ya Wachimbaji Wadogo wa Madini, wakati wa mafunzo maalum kwa wachimbaji wadogo wa eneo la Mererani yaliyozinduliwa rasmi hivi karibuni.
Fundi Sanifu Migodi kutoka Ofisi ya Madini Dar es Salaam, Stanslaus Basheka, akiwasilisha mada kuhusu Matumizi salama na utunzaji wa baruti migodini, wakati wa mafunzo maalum kwa wachimbaji wadogo wa madini wa eneo la Mererani hivi karibuni.
Ofisa wa Sheria kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Hadija Ramadhan, akiwasilisha mada kuhusu Ufafanuzi wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009, Ufafanuzi wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Kanuni zake za Mwaka 2010, wakati wa mafunzo maalum kwa wachimbaji wadogo wa madini wa eneo la Mererani hivi karibuni.
Sehemu ya umati wa wachimbaji wadogo wa madini wa eneo la Mererani, wilayani Simanjiro, wakifuatilia mafunzo maalum kuhusu usalama migodini yaliyotolewa hivi karibuni wilayani humo.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini, eneo la Mererani, wilayani Manyara, wakiuliza maswali kwa watoa mada (hawapo pichani), wakati wa mafunzo maalum kuhusu usalama migodini, yaliyozinduliwa rasmi kitaifa wilayani humo hivi karibuni.
Na Veronica Simba
Serikali imesema itaifungia migodi yote ya madini ambayo itapata ajali kutokana na uzembe na haitafunguliwa hadi hapo Mkaguzi Mkuu wa Migodi atakapojiridhisha kuwa hali ya usalama imeboreshwa na hatua stahiki za kisheria zimechukuliwa kwa Meneja wa Mgodi au Msimamizi aliyehusika na uzembe huo.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka wakati akifungua mafunzo maalum kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini, kwa lengo la kuwakumbusha kuzingatia kanuni zote za usalama mahali pa kazi ili kuepusha ajali za mara kwa mara zinazotokea na kusababisha vifo.
Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini, kupitia Idara yake ya Madini, yalifunguliwa rasmi Mererani, wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara, ambapo Kamishna Mchwampaka aliwaambia wachimbaji wadogo wa madini wa eneo hilo kuwa, kwa sasa uchimbaji mdogo wa madini nchini umegubikwa na ajali nyingi ambazo zinaweza kuepukika endapo tahadhari za kiusalama zitachukuliwa.
“Ajali zinazotokea katika Migodi mingi ya wachimbaji wadogo hapa nchini, zimesababisha vifo, vilema vya maisha na pia gharama kubwa wakati wa shughuli za uokoaji.”
Kamishna Mchwampaka alisema kuwa, Serikali imelazimika kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha kuwa uchimbaji madini nchini, unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Madini kwa kuzingatia usalama na pia utunzaji wa mazingira.
Akizungumzia kuhusu takwimu za ajali migodini, Mhandisi Mchwampaka alifafanua kuwa, taarifa zinaonesha kwamba kuanzia mwaka 2008 hadi mwezi Mei mwaka 2017, ajali zilizotokea katika Migodi yenye leseni ya wachimbaji wadogo wa madini, nchini ni 125 na wachimbaji waliopoteza maisha kutokana na ajali hizo ni 213.
Aidha, aliongeza kuwa, ajali zilizotokea katika maeneo ya wachimbaji wadogo wasiokuwa na leseni hususan maeneo ya mifumuko ya uchimbaji madini, katika kipindi hicho, ni 56 na kusababisha vifo vya wachimbaji 140.
“Kwa mwaka huu pekee, hadi kufikia tarehe 19 Mei, jumla ya ajali zilizotokea ni 11 na jumla ya wachimbaji waliofariki ni 26.”
Kamishna Mchwampaka alisema kuwa, kutokana na takwimu hizo za ajali na vifo, Serikali imeazimia kuhakikisha hali hiyo inadhibitiwa na usalama unaimarishwa katika migodi yote ya wachimbaji wadogo nchini. Alifafanua kuwa, Wizara imepanga kutoa mafunzo husika nchi nzima kupitia Kanda zote 10 za Madini na kwamba mafunzo hayo yatasimamiwa na Maafisa Madini wa Kanda husika.
Akielezea zaidi kuhusu mazingira ya ajali zinazotokea, alisema kuwa uchambuzi wa takwimu unaonesha kuwa vyanzo vikubwa vya ajali hizo ni kuangukiwa na vifusi kutokana na kukatika kwa ngema, kulipukiwa na baruti, kukosa hewa na kuteleza na kuangukia mashimoni. “Hivyo, ni dhahiri kuwa ajali nyingi zingeweza kuepukika kama tahadhari za kiusalama zingechukuliwa.”
Kamishna Mchwampaka alitumia fursa hiyo kutoa maagizo kwa wamiliki wote wa migodi nchini, kuhakikisha wanateua mameneja wa migodi kama Sheria ya Madini ya mwaka 2010 inavyoelekeza ambao alieleza kuwa mojawapo ya majukumu yao ya msingi ni kusimamia usalama, afya za wachimbaji na uhifadhi wa mazingira migodini.
Alielekeza kuwa, Meneja anapokuwa hayupo, lazima kuwe na msimamizi atakayewajibika na kusimamia masuala husika na kwamba, ajali itakapotokea, Meneja au Msimamizi atakuwa wa kwanza kuwajibika.
Aliwataka Maafisa Madini wa Kanda nchi nzima, kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo ambapo Msimamizi Mkuu wa suala hilo ni Mkaguzi Mkuu wa Migodi Tanzania.
Aidha, Kamishna Mchwampaka alieleza kuwa, tayari amemwelekeza Mkaguzi Mkuu wa Migodi, Mhandisi Ally Samaje, ambaye kwa upande wake ametoa maelekezo maalum kwa wakaguzi wote wa Migodi nchini, kuhakikisha kuwa Migodi yote nchini inakaguliwa ipasavyo na ile itakayobainika kuwa haina usalama, itafungwa mara moja hadi pale marekebisho stahiki yatakapofanyika.
Kwa upande wake, Mhandisi Samaje, akitoa mada inayohusu usalama migodini kwa wachimbaji hao wa Mererani, alibainisha kuwa, inawezekana kuweka Migodi salama iwapo kila mmoja kwenye Mgodi, kuanzia Meneja hadi mfanyakazi wa chini, atajenga utamaduni wa kuheshimu sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa.
Mada nyingine zilizotolewa katika mafunzo hayo ni pamoja na Ufafanuzi wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009, Ufafanuzi wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Kanuni zake za Mwaka 2010, Kanuni za Afya na Usalama Migodini, Matumizi salama na utunzaji wa baruti pamoja na utunzaji wa mazingira kwa wachimbaji wadogo na wa kati.
No comments:
Post a Comment