Friday, May 26, 2017

TASAF YANG’ARISHA WALENGWA WA MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASIKINI KISIWANI UNGUJA.



NA ESTOM SANGA-ZANZIBAR.

Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF – unaendelea kuboresha maisha ya walengwa wake Kisiwani Unguja ambao wameanza kujiimarisha kiuchumi kwa kuanzisha miradi midogo midogo ya uzalishaji mali kwa kutumia fedha za zitolewazo na Mpango huo.

Mmoja ya walengwa wa Mpango huo kutoka shehia ya kijini ,kisiwani Zanzibar Bi. Hafsa Seleman Abdallah mama wa watoto WANANE amewaambia wadau wa maendeleo na viongozi nwa TASAF waliotembelea kijijini hapo kuonana na walengwa wa Mpango huo kuwa kwa kutumia fedha za ruzuku kutoka TASAF ameweza kuanzisha shamba la migomba ambalo limeanza kumwingizia kipato kutokana na mauzo ya ndizi kutoka shambani humo.

“Ninaishukuru sana serikali na watu wa TASAF kwa kunitoa kwenye dimbwi la umaskini hadi sasa namiliki shamba hili la migomba kupitia fedha walizonipatia” amesema mama huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40 hivi.

Amesema mikungu ya ndizi iliyoko shambani mwake imekwishanunuliwa hata kabla ya kuvunwa kutokana na mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo hasa wakati huu wa kuelekea mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan unaotarajiwa kuanza hivi karibuni ambapo mkungu mmoja huuzwa kwa shilingi 20,000.

Katika hatua nyingine walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya masikini katika eneo la Kijini huko Makunduchi kisiwani Unguja wameanzisha vitalu vya miche ya matunda na kupanda mboga mboga kupitia utaratibu wa Ajira ya Muda .Kwa mujibu wa maelezo ya sheha , eneo hilo hapo awali halikuwa likizalisha mboga mboga kutokana na aina ya ardhi iliyochanganyika na mawe.

Hata hivyo chini ya utaratibu wa ajira za muda walengwa wa Mpango wa Kunusuru kaya masikini wameweza kuboresha ardhi hiyo kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo na wameweza kulima mboga za majani , pilipili hoho na hata vitunguu mazao ambayo huyauza na kujiongezea kipato.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bwana Ladislaus Mwamanga aliyeshika kitabu akiwa na mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika kijiji cha Kijini kisiwani Unguja Bi. Hafsa Seleman Abdallah wakiwa katika shamba la migomba alilolianzisha mlengwa huyo kwa kutumia fedha za ruzuku kutoka TASAF ikiwa ni njia ya kujiongezea kipato.
Mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika eneo la Kijini ,Makunduchi –Unguja Bi. Hafsa Seleman Abdallah akiwa ndani ya shamba lake la migomba alilolianzisha kwa kutumia fedha za ruzuku kutoka TASAF.
Baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wa kijiji cha Kijini ,Makunduchi kisiwani Unguja wakisikiliza nasaha kutoka kwa wadau wa maendeleo (hawapo pichani ) waliotembelea eneo hilo kuona na mna walengwa hao wanavyonufaika na fedha za Mpango huo.
Wadau wa Maendeleo na viongozi wa TASAF wakiangalia Kamba za kungia mifugo zilizosukwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika eneo la Kijini,Makunduchi –Unguja kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato. Uanzishwaji wa miradi midogo midogo ya kiuchumi kwa walengwa ni sehemu muhimu ya Mpango wa Kunusuru Kaya masikini.
Picha ya juu na chini ni baadhi ya wadau wa maendeleo na viongozi wa TASAF wakiwa katika bustani ya mboga iliyoanzishwa na walengwa wa Kijini ,Makunduchi kisiwani Zanzibar chini ya utaratibu wa Ajira ya Muda ambayo hutekelezwa kwa siku 15 kila mwezi kwa kipindi cha miezi minne wakati wa hari na kisha hulipwa ujira ili kuwaongezea kipato.
Moja ya nyumba iliyoezekwa kwa mabati yaliyonunuliwa na Mlengwa wa Mpango wa kunusuru Kaya Masikini katika eneo la Kijini –Makunduchi kisiwani Zanzibar.
Kiongozi wa shughuli za TASAF katika benki ya Dunia,TTL, Bwana Muderis Mohamed akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini (hawapo pichani ) baada ya kutembelea kaya za walengwa katika eneo la Kijini, Makunduchi kisiwani Zanzibar ikiwa sehemu ya ziara ya wadau wa maendeleo kuona mafanikio na changamoto cha Mpango. 
Bi. Hafsa Seleman Abdallah (aliyeshika kikapo) mkazi wa kijiji cha kijini Makunduchi kisiwani Unguja akiwa katika picha na baadhi ya wadau wa maendeleo waliotembelea shamba la migomba alilolianzisha kwa kutumia fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini. Aliyevaa suti nyeusi ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Ladislaus Mwamanga na kulia kwake ni Msimamizi wa shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia Bwana Muderis Mohamed.

No comments: