Friday, May 26, 2017

DC MTATURU AKABIDHI NYUMBA 12 ZA WALIMU WA SEKONDARI



Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akizindua rasmi nyumba zilizojengwa kwa ajili ya walimu wa shule za sekondari za Minyughe na Wembere baadhi ya aliofuatana nao ni mwenyekiti wa CCM wilaya Hassan Tati mwenye shati la kijani na Diwani wa kata ya Minyughe Saddack. Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akikagua nyumba 12 za walimu baada ya kuzizindua.

Mkuu wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa wilaya,kata na walimu waliokabidhiwa nyumba kwenye shule ya sekondari ya Minyughe.

…………………………………………………

MKUU wa wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu amekabidhi nyumba 12 za walimu wa shule ya Sekondari ya Minyughe na Wembere huku akiwaasa walimu kumpa nguvu rais dokta John Pombe Magufuli kwa kuzitunza ili zidumu na kama sehemu ya kuunga mkono jitihada zake za kuwatumikia wananchi.

Nyumba hizo zimejengwa kupitia mpango wa serikali wa kuendeleza shule za sekondari(SEDEP II) uliogharimu shilingi milioni 300 hadi kukamilika kwake.

Akikabidhi nyumba hizo Mtaruru alimshukuru rais dokta Magufuli kwa dhamira yake njema ya kuwahudumia watanzania ili wawe na maisha mazuri ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)ya mwaka 2015 iliyoeleza uboreshaji wa elimu ikiwemo mazingira ya kufundishia.

“Tukio hili ni ushahidi tosha wa namna ilani ya CCM inavyotekelezwa kwa vitendo,nyumba hizi zitasaidia kuwasogeza walimu karibu na mazingira ya shule na hivyo kuwapa utulivu wa kuandaa masomo yao hali itakayosaidia kuongezeka kwa ufaulu kama moja ya maazimio ya mkutano wa wadau wa elimu uliofanyika mwezi disemba mwaka jana lakini pia itaondoa kero ya walimu kuhangaika mitaani,”alisema Mtaturu.

Aliwataka walimu kuendelea kuiamini serikali wakati inaendelea kushughulikia kero,stahili na madai yao na kuwapongeza kwa ushirikiano walioutoa kwa wakandarasi uliorahisisha mradi huo kukamilika kwa wakati.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri Ally Mwanga alisema uamuzi wa kupeleka mradi huo kwenye shule hizo aliufanya kwa kushirikiana na madiwani baada ya kata hizo kuwa na mazingira magumu ya kukosekana hata nyumba za kupanga na kuwapongeza wataalam kwa kukamilisha ujenzi kwa wakati na kwa kiwango bora.

“Tunaishukuru serikali yetu kwa kuwajali walimu kwa kuhakikisha wanapata makazi bora lakini pamoja na upatikanaji wa nyumba hizi bado kuna uhaba wa makazi ya walimu ambapo mahitaji ni nyumba 524 na zilizopo ni 60 tu,”alisema Mwanga.

Mkuu wa shule ya Minyughe mwalimu Augustino Nkhotya akizungumza kwa niaba yaw engine alisema kukamilika kwa nyumba hizo ni ukombozi mkubwa kwa kuwa awali walikuwa na nyumba mbili hali iliyowalazimu walimu kupanga umbali wa zaidi ya kilomita mbili na hivyo kupunguza tija ya ufundishaji.

Nae mwenyekiti wa CCM wilaya Hassan Tati aliipongeza serikali kupitia mkuu wa wilaya kwa utekelezaji mzuri wa ilani ya CCM ambayo kipindi cha kampeni waliinadi na wananchi waliichagua na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali na wananchi katika kuboresha maisha yao.

Mradi wa SEDEP II ulitengewa jumla ya shilingi milioni 777 kwa wilaya ya Ikungi ikiwa ni ujenzi wa madarasa,nyumba za walimu na matundu ya vyoo miradi ambayo yote imekamilika

No comments: